PATA HABARI MOTO MOTO, ZA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA HAPA, TUPE MAWAZO YAKO TUYAFANYIE KAZI, TUPE HABARI ZOZOTE ULIZO NAZO TUTAZIWEKA HAPA,KWA MWENYE PARTY AINA YOYOTE INAYOHUSIANA NA MAMBO YA MUSIC, TAFADHARI ONGEA NA PAPAYA KUPITIA NAMBA HII..07501 202029..YUPO MACHO 24/7 BEI MAELEWANO.

Tuesday, 15 November 2011

ELIMU YA MSINGI KUWA MIAKA SITA


SERIKALI inakusudia kubadili mfumo wa elimu nchini ambapo kuanzia mwakani, elimu ya msingi inapendekezwa kuwa miaka sita badala ya saba kama ilivyo sasa huku elimu ya sekondari kuwa ya lazima.

Pamoja na hilo, wanafunzi wanaopata mimba hawatafukuzwa shule na badala yake wataendelea na masomo baada ya kujifungua na kumaliza likizo ya uzazi na watakaowapa ujauzito watachukuliwa hatua za kisheria.

Akiwasilisha rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo jana kwa wabunge kwa ajili ya kutoa maoni yao jana Dodoma, Mchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Calistus Chonya alisema rasimu hiyo inapendekeza mwanafunzi atakayeanza darasa la kwanza awe na miaka sita tofauti na sasa, miaka saba.

Akifafanua hilo kwa gazeti hili, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema sera hiyo itaanza kutumika mara mchakato wake utakapokamilika na mategemeo ya Serikali ni ianze mwakani.

Akifafanua zaidi juu ya lugha ya kufundishia, Dk. Kawambwa alisema kwa elimu ya sekondari na msingi itakuwa Kiswahili na Kiingereza tofauti na sasa ambapo kwa upande wa sekondari ni Kiingereza pekee. Shule za awali itakuwa Kiswahili na ualimu lugha ya kufundishia ni Kiswahili na Kiingereza.

“Shule nyingine zitatumia Kiingereza na nyingine zitaruhusiwa kutumia Kiswahili kwa upande wa sekondari,” alifafanua zaidi Dk. Kawambwa na kuongeza kuwa shule za msingi zilizopo nchini ni 16,000 na sekondari za Serikali ni 3,000.

Chonya akifafanua zaidi juu ya sera hiyo, alisema watakaoandikishwa elimu ya sekondari itakuwa lazima wamalize na kuondokana na utoro. Kwa maana hiyo, alisema sasa mtoto anapoanza darasa la kwanza lazima amalize kidato cha nne na si la saba na kuwa na hiari ya kuendelea sekondari.

Alisema elimu ya awali itakuwa mwaka mmoja, msingi miaka sita, sekondari miaka minne, sekondari ya juu miaka miwili na elimu ya juu si chini ya miaka mitatu.

“Imeonekana si vema watoto wa shule ya awali ambao wataanza wakiwa na miaka mitano kusoma shule za bweni na wote watasoma kutwa kwa kupatiwa mahitaji muhimu,” alisema Chonya. Mbali na hayo, alisema wanafunzi watakaokuwa na uwezo kiakili wataruhusiwa kuruka darasa na wale wazito kuelewa watapewa nafasi kusoma zaidi na kutoendelea na darasa la mbele.

Alisema msingi wa upataji cheti cha kumaliza elimu itakuwa upimaji mafunzo ya kila siku na mitihani ya mwisho. “Elimu ya maadili, utaifa, uzalendo, ujasiriamali itakuwa sehemu mafunzo ngazi zote na pia michezo itakuwa sehemu ya mitaala katika shule na vyuo,” alisema.

Kwa sasa, Tanzania inatumia Sera ya Elimu ya mwaka 1995; Sera ya Elimu ya Ufundi ya mwaka 1996 na Sera ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999. Sera mpya itatumika kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu.

Mkakati wa kuandaa sera hiyo mpya ulianza mwaka 2008 na miongoni mwa waliopewa kazi hiyo ni mtaalamu mwelekezi, Abubakar Rajabu ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Wakichangia rasimu hiyo, kati ya wabunge 30 waliochangia, 10 wamepinga elimu ya msingi kwa miaka sita na kutaka iwe saba au nane huku Dk. Kawambwa akiahidi suala hilo kuangaliwa kwa undani.

Mbunge wa Bunda, Stephen Wasira (CCM) alisema “sasa kuna wanafunzi wengi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma, nilitegemea mngeongeza miaka, sasa mtoto anamaliza msingi akiwa na miaka 12 ataenda wapi, aende kwa mama yake?”

Naye Mbunge wa Makete, Dk. Benelith Mahenge (CCM), alisema elimu ya msingi iwe miaka minane na sekondari iwe mitatu huku akiituhumu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwa inaua ufundi na kutoa mfano kuwa Ujerumani imewasaidia kwa kujikita kwenye ufundi.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema sera hiyo imeonesha ubaguzi kwa kutoweka mipango kusaidia jamii zilizo nyuma kielimu na kuachana na muda wa miaka sita kwa elimu ya msingi na kuwa saba au nane.
 
   
 
Jumla Maoni (16)
   
Maoni serikali iwalipe walimu mishahara mizuri, naunga mkono miaka 6 msingi. Ni kuboresha tu na zaidi watoto waanze kusomea taaluma tokea msingi. Kama ni sayansi iwe hivyo tu au biashara na michepuo mingine. Elimu ya sasa masomo ni mengi sana. Tuchukue mifano ya wenzetu waliofanikiwa.
   
Maoni Hakika naunga mkono elimu ya msingi kuwa miaka sita ila napendelea lugha ya kufundishia iwe kingereza tokea awali
   
Maoni Daa serikali inashangaza sana.baada ya kuangalia na kutafakari mapungufu yaliyopo wanabadilisha mfumo.hii si sahihi kabisa wanafunzi wa sasa wengi wanamaliza la 7 hawajui kusoma wala kuandika na walipitia darasa la awali.tatizo sio mfumo ni utendaji mbaya wa serikali.walimu mamechoka na wanalipua mashulmen.kufundisha kwa kiswahili sekondari hili nalo tutafakari vya kutosha tumeandaa vifaa na wataalamu?isije ikawa kama ya mungai?
   
Maoni Nafurahi kuona wizara ya elimu inatathimini ubora wa elimu yetu; kwa kweli miaka sita ni sawa kwani dunia ya sasa nyenzo vya kufundishia na vielelezo vimekuwa vya kisasa zaidi; inatakiwa kama nchi za wenzetu angalau mtoto anamaliza chuo kikuu akiwa na miaka 18-19 na hapo anaanza kulitumikia taifa akiwa na nguvu. Ninachoshauri wizara yetu ya elimu pamoja na kupitia miaka ya kuhitimu kuwa sita pia elimu yetu iwe ya vitendo zaidi kuliko hii ya kuwaandaa wasomi wetu kwa "white collar jobs only" kazi za ofisini. Nchi nyingi zilizoendelea wamekazania zaidi elimu ya vitendo. Naomba wizara yetu itilie maanani elimu bora za vitendo/ujasiriamali/kujiajiri n.k. hapo gurudumu la maendeleo litasongambele kuliko wote kubanana kule posta kutafuta kazi maofisini.
   
Maoni mim ninapendekezi Elimu darasa la sita lakini walimu wawawetaiti sio wana mpelaka mwanafuzi darasa la mbele wakati ajuwi kusoma wale kuandika, iyo inakua uzembe wa walimu.

Thanks
sincerely Ally
   
Maoni serikali inatakiwa kuboresha mfumo wa sasa kwanza, ndio iweze kufikria mfumo mwmingine. sasa hivi hamna walimu wa kutosha, vitabu, vifaa vya kufndshia, maabara alafu unafkria mfumo mwingine?
   
Maoni Hii sera inamapungufu na kusema ianze mwakani ni mzaha kwani huwezi kufanya maadalizi ya mabadiliko haya kwa nchi nzima (Tanzania sio Dar tu).

Mapungufu ya sera hii ni haya kufanya elimu ya sekondali ni lazima kwa kila mtu hizo shule za kuwachukua wanafunzi wote watakao maliza darasa la sita siko wapi? Na walimu na vifaa nk ndani ya miaka sita kuanzia mwakani?

Sera nzuri itakayotupatia mhitimu wa chuo kikuu wa miaka 21 au 22 lakini inaharakishwa bila sababu za msingi, sielewi hii haraka ni ya nini?
   
Maoni Hapa waziri amekosea kabisa. haiwezekani kuona elimu ya wanafunzi inashuka na ni mahututi, badala ya kutafuta mikakati ya kuboresha , akafikiria kuiua kabisa. Tuendelee na mfumo tulio nao wa miaka 13 wa elimu ya chini kabla ya kuingia chuo cha mafunzo ya juu au chuo kikuu. mtaala wa miaka 12 utawagharimu sana wanafunzi ambao wakitaka kuingia vyuo vikuu katika nchi za ng'ambo na ulaya itawabidi kwanza kufidia ule mwaka wa 13 ndiyo baadaye waweze kuruhusiwa kufanyiwa usahili wa kuingia vyuo vikuu katika nchi hizo. si mbaya kama hiyo elimu ya msingi, ya lazima kuishia form two. kama mtu anao uwezo kimasomo basi amalizie hiyo miaka minne inayofuata. kama mtu hana uwezo kiakili na adha kubwa kwake, kwa walimu na kwa jamii kumlazimisha mtu kumwegesha shuleni miaka hiyo yote wakati hana uwezo nayo kiakili. si wote wana akili za nadharia. pia mngeimarisha shule za ufundi tuanzie shule mbili kila mkoa kwa lengo la kufikia shule moja ya ufundi stadi kwa kila wilaya kufikia 2020. juu ya mimba mashuleni, hilo wazo lako litachochea watoto kupata mimba wangali wanafunzi. hilo suala liangaliwe upya. Pia ondoeni adhabu za kuchapwa wanafunzi na uonevu wa kijinsia hasa kwa wanafunzi wa kike.
   
Maoni sidhani kama kupunguza miaka kutaboresha elimu,ingekuwa sahihi kama wanegefanya elimu ya msingi kuwa miaka 8 ili huo mwaka wa 7 na 8 wakafundishwa zaidi elimu ya ujasririliamali na ufundi mbalimbali wakitoka hapo wajue kujitegemea na kujiajiri.kusema elimu ya sekondary lazima wengi watakimbia shule.serikali iwawezesha walimu wake elimu ya ujasiriliamali na kuwaboreshea maslahi yao.
   
Maoni Maamuzi kama hayo yanapofanywa yawahusishe watalam na wadau wa elimu nasikitika mimi kama mwalimu kuona elimu nchi yetu inapungua ubora siku hadi siku katika ngazi zote tokea elimu ya awali mpaka chuo kikuu tunazalisha wataalam wabovu katika fani zote elimu ya msingi kuwa miaka sita siyo suluhisho la ubora wa elimu angalieni zaidi njia mmbadala ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya walimu na kuthamini fani ya ualimu
   
Maoni Busara kubwa imetumika hapa na kwa hili nadhani serikali inahitaji pongezi. Japo ni uamuzi ambao umechelewa sana, lakini kwa hakika ni uamuzi unaohitajika sana, ili kuondoa swala la vijana wengi kuishia mitaani bila kupata fursa ya kuonyesha vipaji vyao ambavyo wangevionyesha iwapo wangesoma kwa lugha wanayoielewa. Lazima tuelewe kwamba elimu ni elimu, haijalishi lugha uliyojifunzia. Sasa watoto watasoma. Ni vizuri kwamba pia sasa Kiswahili kinapewa heshima yake kama lugha ya kufundishia, nina uhakika, tutakuwa na wasomi wengi sasa kupita wakati mwingine wowote, na hii ndiyo nguvu ya kitaifa kwa maendeleo yetu.
   
Maoni Mabadiliko kama hayo yanapofanywa yazingatie mambo mengi mfano unapowapitisha darasa la sita kwenda sekondari wote je kuna madarasa huko sekondari? elimu ya maadili walimu waliopo wanaweza kufundisha wakipewa semina ila je walimu waliopo wana taaluma ya ujasiriamali?(enterpreneurship) mabadiliko hayo yawahusisheawadau wote wa elimu ikibidi mfanye mijadala kama ya katiba ili iweze kuleta tija kwa taifa na kuboresha ubora wa elimu nchini kuliko ilivyo sasa ubora wa elimu unashuka siku hadi siku kwa ngazi zote


Mwl Geay
MUUNGANO USARIVER SEKONDARI
   
Maoni mnafanyia kazi maoni ya wadau? au ni formality tu
   
Maoni Katika lugha ya kufundishia iwe kiswahili kuanzia elimu ya awali mpaka chuo kikuu na kiingereza kifundishwe kama somo la lazima kuanzia awali mpaka chuo kikuu(lugha ya mawasiliano), elimu za vitendo kuanzia ngazi ya awali hii itawanya wanafunzi kuwa wabunifu na kuwaongezea uwezo zaidi! FIKRA SAHIHI HUJA KWA LUGHA SAHIHI! tumetumia kiingereza kwa miaka mingi lakini hakuna tulichoambulia zaidi ya elimu kuzidi kushuka.Ni wakati wa kutumia lugha yetu kwa maendeleo yetu,baadhi ya nchi zimeweza kwanini sisi tushindwe? mfumo wa 6-4-2-3 upo sawa na ndio unaotumiwa na wengi! Wachina wanatafsiri vitabu vya kiingereza kwenda kichina wanafanikiwa na elimu yao ni bora kwa maisha yao! tuamini tunaweza.Bajeti ya elimu ipewe kipaumbele ili kuboresha miundo mbinu ya elimu.
   
Maoni Mfumo huu hautakuwa mzuri kwa kuwa tutaendelea kutengeneza taifa lisilojua kusoma. afadhali miaka iwe nane na pia waanze wakiwa na miaka sita badala ya saba ya sasa.
   
Maoni Mimi ningependa kuchangia upande wa wanfunzi watakopata mimba, kwa kweli kuwarudisha shuleni si afikiani nalo kwasababu watoto wa kike watafanya makusudi wakijua watarudi shuleni. Ningeshauri watakaopata mimba nao wapewe adhabu kwani nao kwa njia moja ama nyingine kashiriki tendo hilo. Pia wale watakaopata mimba kwa kubakwa kwa mfano ndio wapewe nafasi ya kurudia na likizo ya uzazi. Miaka sita kwa elimu ya msingi haitoshi hili serikali walitazame upya. Kingine kuhusiana na elimu ya sekondari kufundishwa kwa kiswahili, Je wamejiandaaje?

No comments:

Post a Comment