SERIKALI inakusudia kubadili mfumo wa elimu nchini ambapo kuanzia mwakani, elimu ya msingi inapendekezwa kuwa miaka sita badala ya saba kama ilivyo sasa huku elimu ya sekondari kuwa ya lazima. Pamoja na hilo, wanafunzi wanaopata mimba hawatafukuzwa shule na badala yake wataendelea na masomo baada ya kujifungua na kumaliza likizo ya uzazi na watakaowapa ujauzito watachukuliwa hatua za kisheria. Akiwasilisha rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo jana kwa wabunge kwa ajili ya kutoa maoni yao jana Dodoma, Mchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Calistus Chonya alisema rasimu hiyo inapendekeza mwanafunzi atakayeanza darasa la kwanza awe na miaka sita tofauti na sasa, miaka saba. Akifafanua hilo kwa gazeti hili, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema sera hiyo itaanza kutumika mara mchakato wake utakapokamilika na mategemeo ya Serikali ni ianze mwakani. Akifafanua zaidi juu ya lugha ya kufundishia, Dk. Kawambwa alisema kwa elimu ya sekondari na msingi itakuwa Kiswahili na Kiingereza tofauti na sasa ambapo kwa upande wa sekondari ni Kiingereza pekee. Shule za awali itakuwa Kiswahili na ualimu lugha ya kufundishia ni Kiswahili na Kiingereza. “Shule nyingine zitatumia Kiingereza na nyingine zitaruhusiwa kutumia Kiswahili kwa upande wa sekondari,” alifafanua zaidi Dk. Kawambwa na kuongeza kuwa shule za msingi zilizopo nchini ni 16,000 na sekondari za Serikali ni 3,000. Chonya akifafanua zaidi juu ya sera hiyo, alisema watakaoandikishwa elimu ya sekondari itakuwa lazima wamalize na kuondokana na utoro. Kwa maana hiyo, alisema sasa mtoto anapoanza darasa la kwanza lazima amalize kidato cha nne na si la saba na kuwa na hiari ya kuendelea sekondari. Alisema elimu ya awali itakuwa mwaka mmoja, msingi miaka sita, sekondari miaka minne, sekondari ya juu miaka miwili na elimu ya juu si chini ya miaka mitatu. “Imeonekana si vema watoto wa shule ya awali ambao wataanza wakiwa na miaka mitano kusoma shule za bweni na wote watasoma kutwa kwa kupatiwa mahitaji muhimu,” alisema Chonya. Mbali na hayo, alisema wanafunzi watakaokuwa na uwezo kiakili wataruhusiwa kuruka darasa na wale wazito kuelewa watapewa nafasi kusoma zaidi na kutoendelea na darasa la mbele. Alisema msingi wa upataji cheti cha kumaliza elimu itakuwa upimaji mafunzo ya kila siku na mitihani ya mwisho. “Elimu ya maadili, utaifa, uzalendo, ujasiriamali itakuwa sehemu mafunzo ngazi zote na pia michezo itakuwa sehemu ya mitaala katika shule na vyuo,” alisema. Kwa sasa, Tanzania inatumia Sera ya Elimu ya mwaka 1995; Sera ya Elimu ya Ufundi ya mwaka 1996 na Sera ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999. Sera mpya itatumika kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu. Mkakati wa kuandaa sera hiyo mpya ulianza mwaka 2008 na miongoni mwa waliopewa kazi hiyo ni mtaalamu mwelekezi, Abubakar Rajabu ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo. Wakichangia rasimu hiyo, kati ya wabunge 30 waliochangia, 10 wamepinga elimu ya msingi kwa miaka sita na kutaka iwe saba au nane huku Dk. Kawambwa akiahidi suala hilo kuangaliwa kwa undani. Mbunge wa Bunda, Stephen Wasira (CCM) alisema “sasa kuna wanafunzi wengi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma, nilitegemea mngeongeza miaka, sasa mtoto anamaliza msingi akiwa na miaka 12 ataenda wapi, aende kwa mama yake?” Naye Mbunge wa Makete, Dk. Benelith Mahenge (CCM), alisema elimu ya msingi iwe miaka minane na sekondari iwe mitatu huku akiituhumu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwa inaua ufundi na kutoa mfano kuwa Ujerumani imewasaidia kwa kujikita kwenye ufundi. Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema sera hiyo imeonesha ubaguzi kwa kutoweka mipango kusaidia jamii zilizo nyuma kielimu na kuachana na muda wa miaka sita kwa elimu ya msingi na kuwa saba au nane. | ||||||||
No comments:
Post a Comment