|
Michezo mbalimbali inafanyika. Miongoni mwake ni mchezo wa bao; uliopendwa na Mwalimu Nyerere. Michezo mingine ni mbio za baiskeli, riadha na kukimbiza kuku. Wabunifu wa sanaa za mikono, kama vile Mkazi wa Kijiji cha Nyanza, Musoma Vijijini, Charles Magigi wananadi maarifa na ubunifu wao. Magigi anaonesha viti anavyotengeneza kwa kutumia mkonge.
Yote hayo yanafanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Yamefanyikia kijijini Butiama kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyezaliwa kijijini hapo mwaka 1922 kabla ya kufikwa na mauti mwaka 1999.
“Sote tunafahamu kwamba wakati tunapata uhuru mwaka 1961 sekta za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hazikuwa na maendeleo yoyote ya kujivunia. Wakoloni walizidumaza kwa makusudi,” hii ni kauli ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. John Nchimbi wakati akizindua maadhimnisho hayo yanayohitimishwa kesho.
Dk. Nchimbi anaendelea kusema, “ndani ya miaka 50 ya Uhuru kuna mambo mengi ya kujivunia katika sekta hizi. Kwa mfano hivi sasa Tanzania inaongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa Waziri, mwaka 1961 kulikuwa na kituo kimoja tu cha redio lakini sasa vipo vituo vya redio 73, vituo vya televishen 26 na magazeti yaliyopata usajili 71. Kwa upande wa vyuo vya taaluma ya uandishi wa habari vipo 12 ambavyo kati yake, vinne ni vyuo vikuu.
Kwa upande wa sekta ya vijana, Waziri Nchimbi akaainisha mafanikio ikiwa ni pamoja na serikali kufanikisha kusajili vikundi 5,000 vya kundi hilo vinavyonufaika na programu mbalimbali za uwezeshaji.
Uanzishwaji wa vituo vya maendeleo ya vijana katika maeneo ya Ilonga mkoani Morogoro, Marangu mkoani Kilimanjaro na Sasanda mkoani Mbeya ni hatua nyingine ya maendeleo.
“Hivi sasa tupo mbioni kuanzisha Benki ya Vijana itakayotumika katika kuwapatia vijana mitaji ya kuanzisha miradi ya maendeleo ili kuwakomboa kiuchumi,” Dk. Nchimbi anasema.
Katika sekta ya utamaduni, taarifa ya Waziri inaonesha uanzishwaji wa asasi tano zinazosimamia tasnia hiyo ni hatua kubwa ya kuhakikisha kuwa mambo yote yanayohusu
utamaduni yanapewa msukumo.
Vivyo hivyo kwa upande wa michezo, Wizara inasema katika kipindi cha miaka 50, Serikali mefanikiwa kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000. Vile vile upo uwezo wa kuandaa mashindano makubwa kama ya CECAFA kwa kutumia uwanja huo.
Vilevile imeanzishwa asasi zinazosimamia maendeleo ya michezo ambazo ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya.
Baada ya Waziri Nchimbi kufungua rasmi maonesho hayo mwanzoni mwa wiki hii, watu wamejitokeza kwa wingi kwenye mabanda mbalimbali ya taasisi zilizo chini ya Wizara kuhakiki ukweli juu ya taarifa hiyo ya Serikali.
Wakazi wengi wa Butiama wanasifu uamuzi wa Wizara kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika kijijini hapo na kukiri kwamba huo ni moyo thabiti wa kumkumbuka Mwalimu Nyerere na wakati huo huo kushirikisha watu wa vijijini katika shughuli kubwa za kitaifa kama hiyo. Wanasema kupitia maonesho hayo, wamefumbuka juu ya mambo mbalimbali.“
Mdogo wake Mwalimu Nyerere, Jackton Nyerere (80) , akiwa katika banda la Idara ya Habari, MAELEZO akaeleza kufurahishwa na picha mbalimbali za maktaba zinazomwonesha mwalimu katika matukio tofauti.
“Nimefurahi sana kuona picha ambazo zimenikumbusha mbali sana… napongeza sana kutukumbuka sisi wana Butiama kwa kuja kuonesha shughuli zenu,” anasema Jackton.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo, Raphael Hokororo anasema ni watu wengi waliotembelea banda lao huku wengi wakivutiwa na picha za maktaba zinazoonesha matukio mbalimbali ya kuanzia harakati za kupigania ukoloni.
Wakazi wengi wa Butiama wanaonesha kuvutiwa zaidi na picha za Mwalimu Nyerere akiwa na viongozi pamoja na baadhi ya wanakijji wenzao. Hokororo anasema uhifadhi wa picha hizo ni sehemu ya mafanikio ya Idara ya Habari.
Anasema Idara imekuwa kiunganishi kikubwa cha Serikali na wananchi na wakati huo huo kiunganishi kwa vyombo vya habari.
Hata hivyo anasema ili kuhakikisha kwamba historia inadumu ndani ya miaka 50 ijayo, ipo haja kwa Serikali kutenga fungu la kutosha kuwezesha uwepo wa vifaa vya kisasa vya kuhifadhia kumbukumbu katika taasisi mbalimbali ili kuwezesha kizazi kijacho kuelewa historia ya nchi.
Katika banda la Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Meneja Matangazo ya Studio na
ya nje, Julius Lucas anasema miongoni mwa mambo ambayo watu wengi wanaolitembelea,
wanaonesha shauku ya kufahamu teknolojia inayotumika katika kurusha matangazo.
Lucas anasema kupitia maonesho hayo, shirika limeuonesha umma wa Watanzania hatua ilizopiga tangu mwaka 1961 hadi sasa. Shirika limetoka kwenye umiliki wa redio yenye idhaa moja na sasa ina idhaa tatu ambazo ni TBC Taifa inayoonesha taarifa za kitaifa, TBC International inaonesha habari za kimataifa na TBC FM ni kwa ajili ya burudani.
Zamani Shirika lilijikita Dar es Salaam pekee lakini sasa kila mkoa una mwandishi. Zipo pia redio za kanda katika miji ya Dodoma, Songea, Lindi na Kigoma. Mitambo ya televisheni inapatikana pia katika mikoa mbalimbali.
Ingawa anasema usikivu wa televisheni ya shirika ni asilimia 60 kwa nchi nzima, Mwandaaji
Vipindi Mwandamizi, Martha Swai anasema hiyo ni changamoto inayofanyiwa kazi ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata matangazo yao.
Kampuni ya magazeti ya Serikali , Tanzania Standard Newspapers (TSN) pia ni miongoni mwa taasisi za wizara zinazonadi mafanikio mbalimbali tangu ianzishwe.
Wanakijiji wakiwemo wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari na msingi wanafurika katika banda la TSN kupata maelezo juu ya shughuli za kampuni hususan uchapishaji wa magazeti ya HabariLeo, HabariLeo Jumapili, Daily News na Sunday News.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Butiama B, Daniel Masiga anasema, “nimenufaika sana na haya maonesho. Nilikuwa sifahamu kama Serikali ina kampuni ya magazeti na isitoshe nimenufaika sana kuifahamu TSN”.
Masiga anasema yapo mambo mengi ambayo amepata nafasi kuyafahamu kupitia maonesho. “Tunashukuru na tunapata elimu kama hii kwa vitu ambavyo tulikuwa hatujawahi kuvipata au kuviona,” anasema.
Anasisitiza kwamba katika banda la Idara ya Maendeleo ya Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) limewaonesha nyasi bandia ambazo alikuwa hajawahi kuziona ana kwa ana isipokuwa kwenye runinga.
Remmy Michael ambaye ni mtembeza wageni katika Makumbusho ya Mwalimu ya Mwitongo, pia anasema amefurahi kuona nyasi bandia huwa naziona kwenye runinga. “Kwenye banda la TFF pia nimeona zulia jekundu ambalo wachezaji hupita wakiingia uwanjani.
Nimeona pia mpira uliotumika katika Kombe la Dunia Afrika Kusini,” anasema Michael.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Butiama, Happy Magesa
anafurahishwa na banda la Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita).
Anasema ameelimishwa umuhimu wa Kiswahili na namna ambavyo Baraza limekuwa likipambana na changamoto za utandawazi ili zisiiathiri lugha hiyo. “Nimeoneshwa vitabu vingi vya sarufi na fasihi.
Vile vile nimeelezwa kuwa Kiswahili kinazidi kupanda chati katika dunia,” anasema Magesa.
Kwa ujumla katika wiki hii ya maonesho, Butiama imekuwa kitovu cha maarifa kutokana na watu mbalimbali waliohudhuria kujifunza masuala mbalimbali kupitia Taasisi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
No comments:
Post a Comment