PATA HABARI MOTO MOTO, ZA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA HAPA, TUPE MAWAZO YAKO TUYAFANYIE KAZI, TUPE HABARI ZOZOTE ULIZO NAZO TUTAZIWEKA HAPA,KWA MWENYE PARTY AINA YOYOTE INAYOHUSIANA NA MAMBO YA MUSIC, TAFADHARI ONGEA NA PAPAYA KUPITIA NAMBA HII..07501 202029..YUPO MACHO 24/7 BEI MAELEWANO.

Friday, 14 October 2011

DR BILAL KUZINDUA SHERIA ZA FILAMU

MAKAMU wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal leo anazindua rasmi kanuni mpya za sheria ya filamu na michezo ya kuigiza ya mwaka 2011.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa alisema juzi kwamba Dk Bilal atafanya uzinduzi huo mjini Musoma kabla ya kesho kuongoza sherehe za kuzindua mbio za Mwenge kijijini Butiama.

Kuzinduliwa kwa kanuni hizo kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, kutawezesha kuwabana wanaotengeneza filamu zisizo na ubunifu na zenye kukiuka maadili. Alisema Sheria namba 4 ya bodi ya mwaka 1976 haikuwa na kanuni za utekelezaji kuiwezesha tasnia kuwa na tija ipasavyo.

Tasnia hiyo inatajwa kuwa kutokana na kukosekana kanuni, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukiukwaji wa maadili, filamu kukosa weledi kiasi cha kutouzika na nyingine kuiga kwa kiwango kikubwa mambo ya nchi za Magharibi ikiwemo uvaaji wa nguo fupi.

Baada ya serikali kubaini hilo, Mei mwaka huu ikaamua zitengenezwe kanuni zinazozinduliwa leo ambazo pamoja na masuala mengine, zinaainisha adhabu zinazostahili kwa watu watakaozikiuka katika utayarishaji filamu.

Wakati Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ikiadhimisha miaka 50 ya Uhuru kijijini Butiama, mkoani Mara, kuzinduliwa kwa kanuni hizo kunatajwa kuwa sehemu ya mafanikio ya wizara kwa upande wa sekta ya utamaduni.

Kwa mujibu wa Fissoo, miongoni mwa mambo yanayoelekezwa ndani ya kanuni hizo ni pamoja na kumtaka mtengeneza filamu kuhakikisha anawasilisha maombi ya kibali cha kutengeneza filamu kwa Katibu Mtendaji wa bodi ambapo itakaguliwa, itapewa daraja na kutangazwa kwenye gazeti la serikali kabla ya kusambazwa.

Kanuni hizo zitasaidia pia kudhibiti wimbi la utengenezaji wa filamu ndani ya muda mfupi ambazo kwa mujibu wa Bodi, nyingi hazifanyiwi utafiti na ubunifu wa kutosha. Hata hivyo bodi imewahakikisha wadau wa filamu kwamba mchakato wa kutoa vibali hautakuwa na urasimu.

Alisema ingawa sheria inasema angalau ndani ya mwezi mmoja mchakato uwe umekamilika, bodi imejiwekea siku saba kuhakikisha kuwa wahusika wanakuwa katika nafasi ya kukamilisha shughuli zao.

Pamoja na kasoro hizo ambazo bodi inaamini kwamba zitatatuliwa kutokana na kanuni hizo, Mtendaji wa bodi, Fissoo anasema wanaridhishwa na mafanikio kutokana na Watanzania wengi kujihusisha na uigizaji kwa kutumia vifaa vyao, kampuni zao za wasambazaji na wasanii wao.

No comments:

Post a Comment