WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesifu utaalamu na teknolojia iliyotumika katika ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo katika makutano ya mitaa ya Shaaban Robert na Garden, jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake unakaribia kumalizika.
Akizungumza na wataalamu wa Kampuni ya China inayojenga ukumbi huo kabla ya kukagua
maendeleo yake, Pinda pamoja na kueleza kuridhishwa na kiwango cha ubora wa ujenzi pia alisema ukumbi huo utaongeza hadhi ya Jiji la Dar es Salaam.
Alisema Serikali itafanya kila liwezekanalo kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Ushirikiano wa
Kimataifa na kwa kampuni inayojenga ukumbi huo ili kuhakikisha kuwa unakamilika mapema
na kuanza kutumika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema ukumbi huo ulio chini ya wizara hiyo utakuwa na uongozi unaojitegemea kama ilivyo kwa Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Alisema awali ujenzi ulioanza mwaka 2010 ulitarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu lakini
umekwama kutokana na vikwazo kadhaa vikiwemo wizi wa vifaa unaofanywa mara kwa mara,
uchelewaji wa ufungaji wa mkongo wa mawasiliano na kuchelewa kuagizwa kwa kifaa
maalumu cha kudhibiti umeme.
Alisema hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu, ukumbi huo sasa unatarajia kukamilika Agosti mwaka huu hatua itakayowezesha Jiji la Dar es Salaam kupata ukumbi mkubwa na wa kisasa na kuongeza hadhi ya Jiji hilo.
Meneja Mradi, Huan Meiluan alisema ukumbi huo ambao sasa umeanza kuwekewa mapambo
mbalimbali ukiwa katika hatua za mwisho, una thamani ya dola za Marekani milioni 30.
Jengo hilo lina kumbi nne, wa kwanza ukiwa na viti 1,002, wa pili mahususi kwa ajili ya mikutano na waandishi wa habari ukiwa na viti 200, wa tatu ukiwa na uwezo wa kuchukua watu 100 na wa nne ukichukua watu 56.
No comments:
Post a Comment