PATA HABARI MOTO MOTO, ZA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA HAPA, TUPE MAWAZO YAKO TUYAFANYIE KAZI, TUPE HABARI ZOZOTE ULIZO NAZO TUTAZIWEKA HAPA,KWA MWENYE PARTY AINA YOYOTE INAYOHUSIANA NA MAMBO YA MUSIC, TAFADHARI ONGEA NA PAPAYA KUPITIA NAMBA HII..07501 202029..YUPO MACHO 24/7 BEI MAELEWANO.

Tuesday, 15 November 2011

SERIKALI KUPANGA ADA SHULE ZOTE


KUANZIA Januari shule zote nchini zitalazimika kutoza ada mpya itakayopangwa na Serikali.

Hatua hiyo inatokana na Serikali kuahidi kabla ya mwisho wa mwezi ujao, kutoa waraka wa ada mpya za shule binafsi na za Serikali.

Kwa sasa waraka unaotumika ni namba 19 wa mwaka 2002 ambao ulipanga ada kwa shule binafsi za bweni za sekondari kuwa Sh 380,000 kwa mwaka na za kutwa Sh 150,000.

Hata hivyo, kutokana na muda mrefu kupita na mazingira kubadilika, shule hizo zimekuwa zikijipangia ada bila kufuata waraka huo.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alitoa maelezo hayo jana wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kassim Ahmed (CUF).

Rukia alihoji sababu za Serikali kutoingilia suala hilo na kuweka viwango elekezi vya ada ili kusiwe na mkanganyiko wa kielimu.

Akijibu swali hilo, Mulugo alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeandaa rasimu ya maoni kutoka kwa wadau ili wapitie na kuamua kwa pamoja juu ya viwango vya ada kwa shule zote za Serikali na za binafsi nchini.

“Wizara yangu itahakikisha viwango vya ada vitakavyowekwa vinazingitia gharama halisi ya kila mwanafunzi na kuweka uwiano katika ulipaji na utoaji ada,” alisema Mulugo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Jakaya Kikwete, akiwa kwenye mahafali ya 11 ya shule za sekondari za FEZA, Dar es Salaam, alisema elimu ni huduma na si bidhaa ya kuuzwa kwa bei ghali, kama zinavyofanya baadhi ya shule binafsi nchini.

“Natoa mwito wa kuangalia upya mifumo yenu ya ada, ili kuwawezesha wazazi wengi zaidi kuwaleta watoto wao katika shule zetu.

Elimu ni huduma si bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine, ambako faida ndicho kichocheo kikubwa cha kuwekeza,” alisema Rais Kikwete katika mahafali hayo.

Kabla ya tamko hilo, Rais Kikwete wakati akikabidhi hati idhini kwa vyuo vikuu tisa nchini mwaka huu, alielezea nia yake ya kuundwa chombo maalumu cha kusimamia viwango vya ada kwa shule binafsi hadi vyuo vikuu, kwa kuwa kiasi kinacholipwa kwa sasa ni kikubwa na hakiendani na maisha halisi ya Watanzania.

Aliwataka wawekezaji katika elimu kuondoa mawazo kuwa shule ni kitega uchumi cha kuwapatia faida kwa kuwa wakifikia hatua hiyo ni hatari kwa ustawi wa nchi.

Alitoa mfano kuwa hivi sasa kuna shule za chekechea zinazotoza ada kubwa hata kuliko inayotozwa na vyuo vya elimu ya juu nchini.

“Kuna haja ya kuunda chombo kama Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji) ambacho kazi yake itakuwa inaangalia viwango vya ada kuanzia shule za chekechekea za binafsi hadi vyuo vikuu.

“Lengo ni kuwawezesha Watanzania wengi wenye kipato cha kawaida kumudu kulipa badala ya hali ilivyo sasa ambapo watu wachache ndiyo wanaofaidi elimu hiyo,” alisema.

Hata hivyo shule nyingi za binafsi hususan zinazomilikiwa na taasisi za kidini, zimekuwa zikikubaliana na utaratibu wa ada elekezi ya Serikali, lakini mara zote zimekuwa zikilalamikia gharama za uendeshaji kuwa kubwa.

Baadhi yao zimekuwa zikiomba Serikali isaidie kuzilipia mishahara ya walimu ili zibakie na majukumu mengine ya uendeshaji ili kuwezesha kutoza ada nafuu.
 
   
 
Jumla Maoni (6)
   
Maoni Nimefurahi sana kusikia habari hizo za serikali ili kila mtanzania aweze kumpeleka mtoto wake shule, lakini hii isiwe ni porojo tu na kuishia kwenye vyombo vya habari. Kwa tamko hili na nia hii ya serikali wengi tumepata matumaini ya elimu kwa watoto wetu. Sasa iwe kweli na itekelezeke maana huwezi muahidi mtu ukwaju kisha asipate atabaki na amejaza mate mdomoni na hii sio nzuri.
   
Maoni Kweli nimefurahishwa na tamko hilo,hiyo itatusaidia wazazi wengi tulio na vipato vidogo kumudu gharama za watoto wetu kwa Elimu bora.Ombi langu,chonde chonde serikali lifanyieni kazi mapema swala hili kusudi tujiandae mapema kabla shule hazijafunguliwa katikati ya jan.2012.
   
Maoni juu ya hili la ada za shule kudhibitiwa na chombo au taasisi ya umma, Rais amenena na anahitaji kuungwa mkono. inasikitisha kuona kuwa kweli ada ya shule kwa chekechea ipo karibu sh. nusu milioni na hiyo shule ambapo alikuwa kwa hayo mahafali ya shule ada zake ni zaidi ya milioni moja Tsh. kweli watoto wengi wanakosa nafasi za kujiendeleza na kuendeleza Taifa kutokana na hao wachache walio na ulafi na pesa, ambao wamefanya shule kuwa miradi ya kitega uchumi, badala ya kujua kuwa shule ni huduma ya jamii ya msingi kwa ajili ya maendeleo ya msingi ya binadamu. Inasikitisha kuona kuwa hata shule za mission ambazo kimsingi nia zao njema ni kuisaida jamii hasa wale wasio na uwezo, baadhi ya taasisi za dini wameingia ktk mtego wa kuwa na ada kubwa ambazo ni vigumu kwa mtu wa kawaida kuzimudu. sambamba na hilo, ningelipenda kumshauri waziri wa elimu na wizara yake kutoa waraka kuhusu shule. hivi sasa unaweza kukuta eti inaitwa shule au mtu amefanya madarasa ya shule, nyumba ya kupanga iliyo kwenye mazingira ya watu, haina viunga vya michezo au maeneo ya kupumzikia au hata maabara na vyoo. shule inatakiwa iwe na eneo kubwa la ekari kadhaa kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi ku- interact masomo, michezo, mapumziko, relax na madarasa yanatakiwa yawe na ukubwa karibu wa mita za mraba 60 hata 90 ili kuwa na hewa, mwanga, nafasi na facilities nyingine za muhimu katika darasa. Hili inabidi lipewe kipau mbele kwani kuboresha mazingira kunasaidia kuboresha elimu. pia ukubwa wa mazingira ni kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kuweza kuinteract masomo na kazi za mikono, ufundi stadi au kazi za kilimo au ufugaji hasa wakati huu tunaposisitiza juu ya kilimo kwanza. Asanteni
   
Maoni Hakika kama tamko hili litatekelezwa ni faraja kubwa kwetu sisi wazazi /walezi kwani baadhi ya shule zinatoza ada kubwa kuliko hata mafao ya kustaafu.
   
Maoni Mh.Waziri aamenifurahisa sana. Lakini nina mashaka. Serekali yetu imekuwa ikipanga mambo mazuri,lakini hakuna utekelezaji. Na matokeo yake wananchi tunazidi kuumia kana kwamba nchi hii haina uongozi. Mkuu wa nchi anatoa agizo lakini hakuna kinachofanyika. Sasa kupitia kauli ya Waziri jana,tafadhali tafadhali Waziri aonyeshe Serekali ipo,na ipo kwa ajili ya wananchi. Ni vema angeutoa waraka huo mapema kabla shule hazijafungwa,kwani shule nyingi za binafsi zinafungwa mwishoni mwa mwezi huu wa Nov. Tena awe na kipindi maalum ktk vyombo vyote vya habari ili wananchi wasikie na kuona kwa ukamilifu.
   
Maoni Naliunga mkono suala hili! Ni watoto maelfu walio achishwa masomo ktk shule za binafsi na kuishia mitaani kwa kukoswa ada. Wanangu hadi leo wansuasua mitaani kutokana na uaghari wa ada, suala hili lifuatiliwe kwa haraka na kwa makini kwani wenye shule hizi wengi wao yawezekana kuwa haohao watunga sheria. UDUMU RAIS KIKWETE

No comments:

Post a Comment