PATA HABARI MOTO MOTO, ZA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA HAPA, TUPE MAWAZO YAKO TUYAFANYIE KAZI, TUPE HABARI ZOZOTE ULIZO NAZO TUTAZIWEKA HAPA,KWA MWENYE PARTY AINA YOYOTE INAYOHUSIANA NA MAMBO YA MUSIC, TAFADHARI ONGEA NA PAPAYA KUPITIA NAMBA HII..07501 202029..YUPO MACHO 24/7 BEI MAELEWANO.

Saturday, 8 October 2011

SHIRIKA LA NYUMBA MOTO


  Sasa lasulubu wizara wadaiwa
Baadhi ya vifaa vya Ofisi ya Wizara ya Habari Michezo na Utamaduni kitengo cha Idara ya Habari (Maelezo) vikiwa nje ya ofisi hiyo.
Idara tatu zilizopo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo jana zilishindwa kufanya kazi baada ya vifaa vyake vyote kutolewa nje na ofisi kufungwa kutokana na kushindwa kulipa kodi ya pango la Sh. milioni 391.4 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Pango hilo ni malimbikizo ya kodi ya miaka ambalo inadaiwa wizara na idara hizo kwa miaka mitatu.
Kwa mujibu wa Meneja wa Kitengo cha Kukusanya Madeni cha NHC, Japhet Mwanasenga, mbali na idara hizo, wizara yenyewe inadaiwa deni la zaidi ya Sh. milioni 253. Idara yake ya Habari (Maelezo) ikidaiwa zaidi ya Sh. milioni 47.
Idara ya Utamaduni inadaiwa zaidi ya Sh. milioni 87 wakati na Bodi ya Filamu inadaiwa zaidi ya Sh. milioni 3.
Zoezi hilo lilianza jana majira ya saa 3:00 asubuhi katika Idara ya Utamaduni.
Wakati vifaa mbalimbali vikiondolewa na kuchukuliwa na NHC, kulitokea mvutano kwa baadhi ya watumishi wa idara hiyo wa kung’ang’ania baadhi ya vifaa wakidai si mali ya serikali bali ni mali zao binafsi.
“Toeni vifaa ambavyo ni mali ya serikali hivi vingine ni vya kwetu wenyewe,” alisema mmoja wa watumishi wa idara hiyo huku akiwa ameng’ang’ania kompyuta ya mkononi.
Licha ya kujitetea, maofisa wa NHC waliwakatalia na kuwaambia kuwa mali hizo wanazichukua na kama ni mali zao binafsi watawasilikiza baadaye ikiwa wataonyesha stakabadhi
MKUTANO WA MAELEZO WAVUNJIKA
Kabla ya maofisa wa NHC na wafanyakazi wa kampuni ya udalali ya Mzizima waliopewa kazi hiyo, kufika Idara ya Maelezo baada ya kukamilisha zoezi hilo Idara ya Utamaduni, kulikuwa na mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na kituo cha kulea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na yatima, lakini baada ya kufika ulivunjika.
Baadaye ulikuwa umeandaliwa mkutano mwingine wa waandishi wa habari ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS). Mkutano huo nao uliahirishwa.na waandaaji.
Mmoja wa maofisa waandamizi wa Maelezo, Fabian Rugaimukamu, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa msemaji ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Sethi Kamuhanda.
Alipoulizwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na hatua hiyo ya NHC, Kamuhanda alisema atalitolea tamko rasmi suala hilo baadaye.
Mwanasenga alisema kabla ya hapo, waliwapa notisi ya siku thelathini kwa ajili ya kulipa deni hilo, lakini hawakutekeleza na ndipo walipoamua kutoa kazi hiyo kwa Mzizima ili kuwafuatilia zaidi.
Pamoja na hatua hiyo, alisema wizara ilishindwa kulipa deni hilo licha ya Mzizima kuwaongezea muda zaidi wa siku 14.
“Tumejitahidi kufuata utaratibu wa kisheria katika kudai deni kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa sababu tulipoona tumedai na hatujalipwa, tukawaachia kampuni ya udalali ya Mzizima, lakini nao hawakuwalipa licha ya kwamba waliongeza notisi nyingine,” alisema.
“Mbali na hivyo, walituambia kwamba wangeweza kulipa deni hilo baada ya kupitishwa bajeti, lakini cha kushangaza bajeti imepita na deni hawajalipa,” aliongeza kusema Mwanasenga.
NIPASHE ilishuhudia wafanyakazi wa idara hizo wakiwa wamekaa nje kwa vikundi hawaelewi cha kufanya huku ofisi hizo zikiwa zimefungwa.
Aidha, Mwanasenga alieleza kwamba bado serikali inadaiwa deni lingine la Sh. bilioni 2 na NHC huku sekta binafsi zikidaiwa bilioni 2.2.
Zoezi hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mpango maalum wa kukusanya madeni yote yanayodaiwa na shirika hilo kutoka kwa wapangaji wake.
Tayari ofisi na wizara kadhaa za serikali na zile za binafsi zimekwisha kukumbwa na zoezi hilo ikiwemo Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ambayo Idara yake ya Ukulima wa Kisasa Jumatano wiki hii kwa kuondolewa katika jengo la shirika hilo kwa kulimbikiza deni la Sh. milioni 30 na vifaa vyake kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa Mwanasenga, NHC itazipiga mnada mali zote za wadaiwa ikiwa watashindwa kulipa madeni.

No comments:

Post a Comment