|
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya kukutana naye alipojumuika na ujumbe wa Waziri Mkuu unaofanya ziara nchini hapa, Maximo alisema ingawa anafanya mazungumzo na timu ya hapa ambayo hakutaka kuitaja, lakini mapenzi yake makubwa yako kwa Taifa Stars.
“Najua Tenga (Leodegar-Rais wa TFF), hana uwezo wa kuniita kwa sasa kwa sababu ana mkataba na kocha mwingine (Jan Poulsen), lakini kama Kikwete au Pinda watasema, bila shaka nitatekeleza,” alisema Maximo huku akijawa na furaha kubwa kukutana na Watanzania jijini hapa.
Hata hivyo, alikosoa utaratibu wa sasa wa kutoinua vijana na badala yake kuita katika timu ya Taifa wachezaji wakongwe kwa sababu tu wanaishi Ughaibuni.
“Angalia hivi sasa mnaacha wachezaji vijana ambao wanahitaji kunyanyuliwa na badala yake mnaingiza wachezaji wenye umri mkubwa (anatoa mfano) ambao wana miaka miwili tu ya kucheza soka,” alisema kocha huyo.
Alishangaa kusikia kuwa hivi sasa Mrisho Ngassa anakalishwa benchi katika timu ya Taifa na kuingia baadaye, wakati ni mchezaji mahiri na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuua kiwango chake.
“Tunapaswa kuangalia uwezo wa vijana wadogo na kuwainua, angalia mimi ndiye niliyemuibua Mbwana Samatta na kumuingiza Taifa Stars… angalia sasa, anacheza soka la kulipwa nje ya nchi, hayo ni matunda ya kuibua vijana,” alitamba.
Alisema si vibaya kubadilisha wachezaji, lakini ni mbaya kukiuka filosofia ya soka, ambayo inataka soka kuanzia kwa vijana wadogo na kuwakuza kivipaji.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Pinda na ujumbe wake walitembelea uwanja mkubwa wa soka kuliko yote duniani wa Maracana, ambapo alishuhudia ukikarabatiwa kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2014.
Alijionea pia kumbukumbu mbalimbali za uwanjani hapo, ikiwa ni pamoja na nyayo za wachezaji maarufu wa nchi hii akiwamo Mfalme wa Soka Duniani, Edson Arantes dos Nascimento-Pele na wengineo.
Pia aliona mpira ambao Pele alifungia bao lake la 1,000 mwaka 1969, lakini pia wavu ambao siku hiyo ulikaa katika milingoti alimofunga bao hilo. Kivutio kingine ni sanamu ya Zico ambaye alifunga jumla ya mabao 500 katika uwanja huo wa Maracana
No comments:
Post a Comment