ERIKALI inatarajia wiki ijayo kuzindua kanuni za sheria zitakazoweka utaratibu rasmi utakaobana utengenezaji wa filamu zisizo na ubunifu na zenye kukiuka maadili.
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo alisema sekta ya filamu ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukiukwaji wa maadili, filamu kukosa weledi kiasi cha kutouzika na nyingine kuiga kwa kiwango kikubwa mambo ya nchi za Magharibi ikiwemo uvaaji wa nguo fupi.
Fissoo alisema hayo yamekuwepo kutokana na Sheria Na 4 ya mwaka 1976 kutokuwa na kanuni.
Baada ya serikali kubaini hilo, Mei mwaka huu zimetengenezwa kanuni zitakazozinduliwa Oktoba 13 mwaka huu na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kijijini Butiama.
Alisema hayo jana kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ambayo idara mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo zinafanya maonesho ya shughuli zake katika Kijiji cha Butiama, Musoma Vijijini.
Kwa mujibu wa Fissoo, kanuni hizo zinafafanua sheria ikiwa ni pamoja na kumtaka mtengeneza filamu kuhakikisha anawasilisha maombi ya kibali cha kutengeneza filamu kwa Katibu Mtendaji wa bodi. Itakaguliwa, itapewa daraja na kutangazwa kwenye gazeti la serikali kabla ya kusambazwa.
“Wengi hawawasilishi filamu kwa ajili ya kupewa daraja,” alisema Fissoo na kuongeza kwamba kumekuwepo wimbi la utengenezaji wa filamu ndani ya muda mfupi ambazo nyingi hazina utafiti na ubunifu.
Hakufafanua kwa kina adhabu zitakazowakabili watu watakaokiuka kanuni hizo kwa kusema siku ya uzinduzi ndipo yote yatafahamika.
Aliwahakikishia wadau wa filamu kwamba mchakato wa kutoa vibali hautakuwa na urasimu. Alisema ingawa sheria inasema angalau ndani ya mwezi mmoja mchakato uwe umekamilika, bodi imejiwekea siku saba kuhakikisha kuwa wahusika wanakuwa katika nafasi ya kukamilisha shughuli zao.
Hata hivyo Mtendaji huyo wa bodi alisema katika miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yapo mafanikio makubwa katika sekta ya filamu kutokana na Watanzania wengi kujihusisha na uigizaji kwa kutumia vifaa vyao, kampuni zao za wasambazaji na wasanii wao.
No comments:
Post a Comment