WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameelezea hofu aliyoipata kwa mara ya kwanza alipoitwa Ikulu
na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwenda kuwa msaidizi katika ofisi binafsi ya Rais.
Pinda ambaye amezuru kaburi la Hayati Mwalimu Julius Nyerere kijijini Butiama, mkoani Mara alisema ilikuwa mwaka 1978 alipoitwa Ikulu na Mwalimu Nyerere na kusema aliingiwa hofu akidhani pengine alikuwa amepokea rushwa bila kufahamu katika kazi aliyokuwa nayo ya
Wakili wa Serikali.
Akiwa kijijini Butiama ambako alisalimiana na familia ya Nyerere ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Mara, Pinda alisema hofu aliyokuwa nayo ilitokana na ukali aliokuwa nao Mwalimu Nyerere wakati huo kwa mfanyakazi wa serikali anayegundulika kuwa amepokea
rushwa.
Alisema alidhani pengine Mwalimu alikuwa amepewa taarifa zinazomhusu yeye na kusababisha kuitwa kwake.
Alisema pamoja na kushindwa kula na kulala, aliuona umbali wa kutoka geti la Ikulu hadi mlango wa kuingia ndani ya jengo hilo sawa na umbali wa kutoka Butiama hadi Musoma
Mjini kutokana na woga uliosababisha miguu kutetemeka.
“Mwaka 1974 nilimaliza kozi yangu ya Shahada ya Sheria pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwaka 1975/76 nilipangiwa kazi ya kuwa Wakili wa Serikali katika mikoa ya Mwanza na Mara.
Mwaka 1978 nilihamishiwa mkoani Mtwara lakini nikiwa ndio naanza kazi nilipigiwa simu ya Polisi kwamba naitwa Ikulu Dar es Salaam,” alisema.
Aliendelea kusema, “Nilishikwa na hofu ambayo sijawahi kuipata tangu nizaliwe. Nilijiuliza maswali mengi sana… nilijiuliza nimekosa nini hadi naitwa Ikulu? Nikajiuliza lakini mbona mimi bado ni mdogo hilo kosa nimekosa lini?
Nikajiuliza pia au katika kupitapita huku na huko katika kazi yangu ya Wakili wa Serikali nimepokea rushwa? Lakini nikasema hapana.”
“Nilikaa na hofu hiyo hadi nilipofika Dar es Salaam. Nilipofika geti la Ikulu hofu ilizidi kuongezeka nilikuwa natetemeka sana.
Nilipoingia nilikwenda kwanza katika ofisi ya sekretari wake. Alinikaribisha akaniuliza nikupe
soda nikamwambia hapana. Akasema au nikupe maji nikamwambia nimeshiba.”
“Nilikaa katika ofisi ile hadi baadaye nilipoingizwa kwenye ofisi ya Mzee Joseph Butiku, nilipoingia na yeye aliniuliza kama anipe soda kwanza nilikataa lakini baadaye alinitoa woga… alinieleza nisiwe na hofu kwani nimeitwa ili niwasaidie kazi katika ofisi yao, hapo hofu
ilipungua kidogo nilipopewa soda nikanywa tena yote sikubakiza hata kidogo,” alisema Pinda.
Alisema hata hivyo hakuweza kuripoti katika ofisi hiyo kuanza kazi hadi mwaka 1982 baada ya kumaliza pilikapilika mbalimbali zikiwemo za kujifunza misingi ya kazi na maadili
No comments:
Post a Comment