.
NYANI dume, maarufu kwa jina la ‘House boy’, amevuta hisia za wengi na kuacha kumbukumbu kubwa kwenye Maonesho ya Nanenane ya Nyanda za Juu Kusini mwaka huu mjini Mbeya.
Maonesho hayo yalishirikisha mikoa ya Rukwa, Ruvuma, Iringa na Mbeya na yalifungwa na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo. Uwapo wa nyani huyo dume, ulivutia mamia ya watu, kwani nyani huyo amefunzwa kuwa mlinzi na msaidizi wa nyumbani, yaani ‘house boy’.
Mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, kuzuru banda la Wilaya ya Namtumbo, alizungumza na mmiliki wa nyani huyo na kuvutiwa na namna anavyowatunza wanyama, wakiwamo mbwa na paka.
Maelezo ya mmiliki wa nyani huyo, Ramadhani Rehani (32) kwa Dk. Ishengoma katika maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu ‘Kilimo Kwanza: Tumethubutu, Tumeweza na Tunasonga mbele’, yalivutia wengi na kuanza kupashana habari kuhusu nyani huyo.
Wananchi karibu wote walioingia katika maonesho hayo kwenye Viwanja wa John Mwakangale, hawakuacha kufika katika banda la Kilimo la Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, kujionea wenyewe kuhusu nyani huyo anayeitwa Igo, mwenye umri wa miaka 26.
Rehani akizungumza na gazeti hili kwenye maonesho hayo hivi karibuni, alisema anamfuga nyani huyo pamoja na mbwa wawili na paka mmoja ambao hushirikiana katika kuimarisha ulinzi shambani na nyumbani.
Wakati akizungumza nami, watu waliendelea kupiga picha na nyani huyo kwa kumlipa Sh 2,000 huku akisisitiza watu waulize maswali bure ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusu nyani huyo ambaye anadai mtu mshirikina, aliyetoa mimba na mwenye roho mbaya, hapokei zawadi yake ya chakula na hata akipokea, hali na humnyooshea mtu huyo mkono kwa ishara kueleza kuwa si mtu mwema.
Nikiwa eneo la banda hilo, dada mmoja alimrushia chungwa nyani huyo lakini aliligusa na kuliacha, lakini mtoto aliyekuwa hapo pia alimrushia chungwa na alilichukua na kuanza kulila na alipomaliza alimwendea na kumshika mguu huku Rehani akisema anatoa shukrani kwa chungwa la mtoto huyo.
“Hajaonesha ishara kwa nini hakupenda kula chungwa alilopewa na yule dada (wakati huo hakuwepo eneo hilo) lakini kama angekuwepo hapa bado, pengine ningefahamu kulikoni, ila hapendi mtu mwenye roho mbaya au nia mbaya moyoni,” alifafanua Rehani, mkulima wa mazao mchanganyiko.
Rehani anaendelea kueleza, “Ukimwita anaitika na kuja, lakini kama una roho mbaya, muuaji ama mwizi, hakuitikii wala kukusogelea, ni mlinzi mzuri pale nyumbani kwangu, mwizi hakaribii shambani wala nyumbani, huwa tunampa maharage anamenya kisha sisi tunayaosha na kuyapika tu, ni msaidizi na mlinzi mzuri kuliko mbwa,” anabainisha Rehani.
Akieleza namna alivyompata, Rehani anasema alimkamata miaka 20 iliyopita akila mahindi katika ghala la nje nyumbani kwake Mtaa wa Rusenti na kumtunza kwa lengo la kutaka kujua kwa nini nyani hawaachi kula mahindi na kugundua kuwa wanakula kwa sababu ya dhiki ya njaa.
“Sasa hivi haibi mahindi kwa sababu anashiba, nimemfundisha baadhi ya kazi na sasa anazifanya, unaweza kumpa mtoto ambebe na akambeba ila watu wengi wanamwogopa, nina shamba la hekari 200 lakini ninalima hekari 20 pekee za mazao mchanganyiko kama mahindi, mbaazi na viazi vitamu na yeye ndiye mlinzi wangu, siku hizi hata nyani wengine hawasogei,” anasema Rehani.
Ishengoma akiwa katika banda hilo, alitumia fursa hiyo kuitaka Halmashauri kumfuatilia kijana huyo anayemfuga nyani huyo na kumwezesha kukuza ubunifu wake kwa njia sahihi hasa kutokana na kumweleza kuwa amekuwa akitumiwa na Halmashauri katika kampeni mbalimbali na baadhi ya wanasiasa wakati wa uchaguzi mbalimbali.
Nilipomuuliza kwa nini asimrejeshe katika hifadhi yoyote ya wanyama, alisema yeye alimkamata kama mhalifu lakini kwa kuwa anapenda wanyama, aliamua kumfanyia uchunguzi nyani ili kujua tabia yake ya wizi kama inaweza kuisha na ikiwa mtu atamtaka nyani huyo mwenye mke na watoto, anamuuza kuanzia Sh milioni 200.
Anasema anakula saa 24 ingawa anaridhika na mlo anaopewa na pia ana uwezo wa kunywa bia kreti nne kwa siku bila kulewa na pia ana uwezo wa kumtambua adui na mgeni wa aina yoyote na tofauti na nyani wengine kuchukia wanawake, yeye anawaheshimu.
Rehani anasema kupitia kampeni anazofanya na Igo, ameweza kujenga nyumba, kununua pikipiki na ikiwa mtalii anataka kumnunua nyani huyo atamuuza kwa Sh milioni 800 ili alipe kodi kwa Serikali; na kwa Mtanzania anamuuza kwa Sh milioni 200.
“Kama watafiti mbalimbali na wasomi wameweza kutumia mbwa na panya kutegua mabomu, hata nyani anaweza kufunzwa, Polisi wanaweza kuwatumia kwa ulinzi na uchunguzi maana wana akili kama mtu na uwezo mkubwa wa kumtambua mhalifu, naomba watafiti wawachunguze nyani kwa nyanja hiyo,” anasena
Anasema wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana (2010), alimtumia na kupata zaidi ya Sh milioni 30 kwa mwaka mzima na katika hali ya ajabu kuna baadhi ya wagombea alimpa ishara kuwa hawashindi ni waongo na wenye nia mbaya na kweli hawakushinda uchaguzi huo.
“Huyu si mganga wa kienyeji, watu wasije kujaa kwangu kutaka waaguliwe, bali nimemfundisha baadhi ya mambo na ni mwepesi kushika, nilichogundua ni kwamba anaiba mahindi na kula mazao kwa sababu ya njaa na pia ana akili ya pekee yenye kufahamu maadui wa watu wema” anasema.
No comments:
Post a Comment