Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema ipo haja sasa kujadili kwa kina namna ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato iliyopo kati ya maskini na matajiri kwani ni hatari kwa amani ya nchi.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye.Alisema hayo kwenye viwanja vya Sokoni Igoma jijini Mwanza, wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM katika ziara ya baadhi ya viongozi wa chama hicho mkoani hapa.
Nape alisema nchi nyingi duniani zimekuwa zikikumbwa na machafuko kutokana na kuachiwa kukua kwa tofauti kubwa ya kipato kati ya maskini, ambao ndio wengi na matajiri wachache.
“Ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji… Heri kuziba ufa kuliko kujenga ukuta. Ni muhimu leo wapenda amani wa nchi hii tujadili kwa kina namna bora ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato nchini kwani ikiachwa hivi baada ya muda, nchi hii itachafuka,” alisema Nape.
Alisema vijana ndio wenye nguvu, ambao kila kukicha wamekuwa wakilumbana juu ya siasa tu vijiweni bila kutafakari na kujituma kupunguza tofauti hiyo kubwa ya kipato kati ya maskini na matajiri nchini.
Alisema vijana ndio waathirika wakubwa kwani wataishi leo na kesho.
Alisisitiza kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini mara kadhaa wamekuwa wanatokea watu ambao si waaminifuwanapewa dhamana ya uongozi wanautumia vibaya na matokeo yake rasilimali zinatumika kuneemesha watu wachache.
Akatoa wito kwa vijana kuwa makini kuhusu masuala yanayohusu matumizi mabaya ya rasilimali za umma, akisema lazima waende mbali zaidi ya mipaka ya itikadi, akiwataka washikamane na kutosahau kuwa wana dhamana ya leo na kesho.
“Hivi uzalendo leo uko wapi? Unaweza kukuta Mtanzania, tena kijana anashabikia watu kutumia watakavyo rasilimali za nchi hata kuhujumu nchi na bado akaonekana ni shujaa! Tusipoamua kubadilika tutakuwa tunabomoa nchi kwa mikono yetu wenyewe,” alisema Nape.
Aidha, Nape aliitaka wizara ya Uwezeshaji chini ya Dk. Mary Nagu, kuhakikisha wanaowezeshwa kwa sehemu kubwa ni vijana wazalendo wa kitanzania kwani hiyo ni njia mojawapo ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato kati ya maskini na matajiri.
“Lengo la wizara ile ni kuhakikisha wazalendo wa kitanzania wanawezeshwa kuumiliki uchumi wao, sasa isije wakawa wanaongezewa uwezo matajiri tu na vijana maskini wa kitanzania wanaachwa wakitoa macho, hiyo haitakuwa sawa. Tutaomba wizara itoe takwimu kila mara za Idadi ya wanaowezeshwa na ni kina nani," alisisitiza Nape.
Naye Katibu wa NEC wa Uchumi na Fedha, Lameck Nchemba Mwigulu, alihoji ugonjwa gani unawaingia Watanzania leo kiasi kwamba muda wote wanawaza uchaguzi tu mpaka wamesahau hata kufanya shughuli za maendeleo.
“Siku hizi ni rahisi kukuta watumishi wengi hata serikalini wanajadili Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 utadhani ni kesho, kama vile wameagana na Mungu watakuwa hai. Wanajadili kiasi cha kusahau hata kuwajibika, nani katuloga sisi?" alihoji Nchemba.
Ziara hiyo ya viongozi wa CCM taifa Kanda ya Ziwa itaendelea kwenye Wilaya ya Geita na Ukerewe, lengo likiwa ni kuamsha ari ya wanachama hasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambapo CCM inaonekana kutofanya vizuri kama ilivyokuwa mwaka 2005.
Mbali na Nape, ziara hiyo iliwajumuisha Katibu wa Uchumi na Fedha wa NEC, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Mtera na mjumbe wa NEC, Livingstone Lusinde na Katibu Msadizi Mkuu wa Idara ya Itikadi, Sixtus Mapunda.
No comments:
Post a Comment