Kufuatia kuibuliwa kwa biashara ya binadamu nchini, Serikali imemfukuza mfanyabiashara Altaf Hussein anayetuhumiwa kuhusika na biashara hiyo.
Aidha, imewatimua watu wote walioingizwa nchini na mfanyabiashara huyo kwa kutumia Kampuni yake ya Altaf & CO.PK ambao walikuwa wakifanyakazi nchini kinyume na sheria.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili hivi karibuni, Ofisa wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Hamis, alisema amri hiyo imeanza kutekelezwa toka siku ya Jumatatu ya wiki hii ambapo watu wote walitakiwa kuondoka katika muda wa saa 24.
Alisema kutokana na utata uliokuwepo kwa watu ambao wana uraia wa Pakistani, ofisi yake imebaini watu wote walioingizwa nchini kwa kutumia Kampuni ya Altaf&CO.PL hawakuwa na vibali halali na walikuwa wakifanya kazi kinyume na utaratibu wa nchi.
“Tumeamua kuwapa masaa 24 kuondoka nchini, tumefuatilia kama amri hii imetekelezwa kikamilifu na naweza kusema wameondoka chini ya uangalizi maalum,” alisema Hamis.
Alisema katika kundi la watu 43 waliokuwa wakifanyakazi kwenye makampuni ya kutengeneza nondo ya Iron Steel, Simba Steel vyote vya jijini Dar es Salaam na Nyakato Still cha jijini Mwanza walikuwa hawana vibali halali vya kuishi nchini.
Alisema hata viongozi wa viwanda hivyo walipohojiwa juu ya utata huo, walikiri kuwaajiri watu hao bila kuwa na vibali vinavyoruhusu kuishi na kufanya kazi hapa nchini.
“Tumechukua hatua kali baada ya kuhakikisha hata uongozi wa viwanda hivi unakiri kufanya kosa hilo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi,” aliongeza.
Akizungumzia upande wa Altaf, mtu ambaye amejihusisha kikamilifu na biashara hiyo na kujiingizia mamilioni ya pesa, alieleza kuanzia sasa hataruhusiwa kukanyaga ardhi ya Tanzania na endapo akionekana sehemu yoyote nchini atakamatwa na kufunguliwa mashtaka.
Alisema Hussein ambaye pia ana uraia wa Pakistani alikuwa akifanyakazi kinyume na utaratibu pamoja na kufanyabiashara hiyo inayopigwa vita duniani kote.
“Hussen ndio mzizi wa tukio hili, tunawashukuru sana ninyi NIPASHE kwa kuliweka wazi jambo hili, hivyo Uhamiaji imemtaka kutokanyaga ardhi ya Tanzania na kama akionekana tutamkamata kwa kuvunja sheria,” alisema.
Hamis alisema Hussen aliishi nchini kwa kutumia kibali cha daraja B kinachomruhusu kufanya kazi ya ufundi na hakuruhusiwa kufungua Kampuni yake kama alivyofanya.
Hussein alituhumiwa kwa kipindi cha miaka miwili 2010-2011 kutumia kampuni yake kuwaingiza raia 43 kutoka nchini Pakistani na kujizolea Sh. milioni 430.
Kwenye biashara hiyo haramu, Hussen alikuwa akitumia vibali bandia vya kuishi nchini pamoja na kuwatumikisha raia hao kwenye viwanda hivyo kwa njia ya kitumwa.
Hata hivyo, Uhamiaji imewatahadharisha wamiliki wa viwanda hivyo kuacha mara moja kufanya mbinu yoyote ya kuwarudisha nchini na kuwataka kuwaajiri wafanyakazi wengine ambao watakuwa na vibali halali vya kuishi na kufanya kazi.
Awali gazeti hili kwa wiki tatu mfululizo ilitoa taarifa ya kuwepo kwa biashara hiyo ambayo ilikuwa ikimuhusisha mfanyabiashara hiyo na baadhi ya maofisa wa Uhamiaji wasiokuwa na nia njema kuwaingiza nchini watu hao na kujiingizia mamilioni ya pesa.
No comments:
Post a Comment