Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametamani kungekuwa na utaratibu wa kucharaza viboko watu wanaovunja sheria na kanuni za kutumia barabara nchini.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jana kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya sekta ya ujenzi nchini, Waziri huyo alisema kuna watu wanaegesha magari sehemu yoyote, kama kwenye barabara za kutoa huduma pembezoni mwa barabara kuu (service road), wengine kuzifunga kabisa kwa minyororo, kiasi kwamba huwa anatamani watu kama hao wacharazwe viboko wakiwa ofisini kwao, lakini bahati mbaya nchi hii haina sheria hiyo.
Hata hivyo, alisema kama mkakati wa kulinda barabara na hifadhi yake, wizara yake itaanza kutumia Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kama njia mojawapo ya kupunguza na kuondoa msongamano katika miji na mijiji.
Waziri Magufuli alisema maadhimisho ya miaka 50 ya sekta ya ujenzi, tangu uhuru yatafanyika kwa wiki moja kuanzia leo.
Alisema mrundikano wa magari yanayoingia na kutoka katika miji na majiji hususani mkoa wa Dar es Salaam, unahitaji mpango mahsusi ili kufanikisha zoezi zima.
Alifafanua kwamba kuna kasumba ya baadhi ya watu kuwa wazembe wa kutotii sheria na taratibu mbalimbali za matumizi bora ya barabara na kueleza kuwa hali hiyo ni chazo kikubwa cha msongamano mkubwa wa magari mjini.
“Tunaweza kutunga na kupendekeza njia mbalimbali za kupunguza huu msongamano lakini kama sheria hazitiliwi maanani hakuna tutakachokuwa tunakifanya,” alisema.
“Tumezungumza na IGP juu ya mstakabali wa kukabiliana na jambo hili na hasa kuwashirikisha wenzetu askari katika zoezi zima kwa kuwa askari ni kikosi imara kinachoweza kusimamia sheria,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza kwamba: “Kwa kuzingatia ibara ya 26 kifungu kidogo cha 1 na 2 cha Katiba ya nchi, kinachomwamuru mtu bila kuzingatia umri, sura wala nafasi aliyonayo kufuata sheria za nchi, wizara imedhamiria kuhakikisha kifungu hiki kinasimamiwa na kinatekelezwa na kila mtu.”
Alisema: “Wizara inakusudia kuanzisha kikosi kazi maalumu kitakachojihusisha na masuala ya barabarani kwa kusaidiana na vikosi vingine ambavyo vipo hadi sasa.”
Alitaja njia nyingine ambazo zitachukuliwa na wizara katika kuhakikisha wanaondoa msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, ni kujenga barabara za juu, aliongeza kuwa tayari vituo vitakavyohusika na mradi huo vimekwisha kufanyiwa kazi na kwamba hadi sasa tayari ujenzi unaendelea.
Alisema wizara inategemea kupanua barabara zilizopo na kwamba tayari taratibu za kurekebisha sehemu ya barabara hususani zitakazohusika na mradi wa magari yaendayo kasi umekamilika.
Kadhalika, alisema wizara inakusudia kuanzisha feri (panton), itakayokuwa ikitoka Kigamboni kwenda Bagamoyo na treni kutoka Ubungo hadi Tegeta.
Alitoa onyo kwa wavamizi wa barabara na kutahadharisha kwamba wanaofanya hivyo ‘wanasogelea umaskini’ kwa maana kwamba watavunjiwa nyumba au biashara walizonazo.
“Inabidi ifike hatua tufanye kazi na si kuendekeza siasa…ni heri lawama kuliko fedheha,” alisema.
Aliwataka makandarasi wote kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miiko ya kazi zao.
Kuhusu mafaniko ya sekta ya Ujenzi kwa miaka 50 ya uhuru, alisema mwaka 1961 Tanganyika ilipopata uhuru, ilikuwa na mtandao wa barabara za lami uliokuwa na urefu wa kilometa 1,300, lakini hivi sasa mtandao ni kilometa 6,500 na kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali inatarajia kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 1,154.
No comments:
Post a Comment