Mfungwa aliyepewa msamaha wa parole baada ya kutumikia theluthi ya kifungo chake cha miaka 15 kuua bila ya kukusudia, amekuwa kinara wa gurudumu la maendeleo katika Kijiji cha Mbirikili Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Hayo yalibainishwa na wakazi wa kijiji hicho wakati mfungwa huyo, Chacha Kerenge, alipotembelewa na wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Rarole nyumbani kwake ambako alifanyiwa tafrija ya kukubalika kijijini hapo na kuonyesha msukumo wa maendeleo kwa jamii tangu atoke gerezani .
Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Mwita Ngoka, alisema kuwa Kerenge alipofika kijijini hapo, amekuwa mfano mzuri kwa jamii hususani vijana kwa kile alichodai kuwa hufanya kazi kwa juhudi katika kujitafutia riziki na maendeleo ya familiya yake.
Ngoka alisema kwa sasa katika kijiji hicho hakuna kijana anayetafuta maendeleo kwa bidii na kasi ya ajabu kama mfungwa huyo.
Alisema mfungwa huyo anamiliki mbuzi 54 na ng’ombe 16 na shamba la mazao lenye ukubwa wa hekari tatu.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika sherehe hizo ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Taifa, Ben Kaijage, aliiasa jamii kuwapokea wafungwa pale wanapopewa misamaha au wanapomaliza kutumikia vifungo gerezani kwa moyo mmoja na kuwapa ushirikiano.
“Mfungwa anapofungwa gerezani si kwamba hatakiwi kurudi tena kwa jamii la hasha, gerezani ni sehemu ya mfungwa kujutia makosa yake na kupata elimu ya kuishi vema katika jamii,na ndo maana wafungwa hupewa mafunzo mbalimbali wakiwa gerezani, ”alisema Kaijage.
Kaijage alisema mfungwa huyo alifungwa Septemba 25, mwaka 2003 katika Gereza la Butimba Mwanza na kuhamishiwa Gereza la Kilimo Mgumu Septemba 20, mwaka huo ambako alitumikia kifungo kwa miaka sita na kupata bahati ya kuchaguliwa kuingia katika msamaha huo wa parole.
Alisema mfungwa huyo alipewa msamaha wa parole mwaka 2009 na kuiasa jamii kuwakubali wafungwa kwa kile alichodai kuwa kuna baadhi wanapata bahati ya kuingia katika msamaha hiyo ili waende wakamalizie kifungo uraiani wakiwa na familiya zao.
Naye mfungwa huyo, alisema anaishukuru jamii kwa kumpokea kwa mikono miwili na kumpa moyo wa matumaini ya maendeleo yake.
Kerenge alisema anaiomba bodi hiyo ilegeze masharti ya msamaha wa parole kwa kile alichodai kuwa wapo wafungwa wengi waliopo gerezani wamekwisha kujutia makosa yao lakini hawana haki ya kujaza fomu ya kuomba parole kwa kuwa makosa waliyotenda hayaruhusiwi kupewa msamaha.
Alisema wapo wafungwa wengine wamefungwa kwa makosa ya kusingiziwa na makosa hayo ni moja wapo ya makosa ambayo hayana msamaha, hivyo kumnyima haki ya kupewa msamaha wa parole ni kumnyima haki ya msingi mfungwa.
“Mfano mzuri ni mimi,nilifungwa miaka 15 kwa kosa la kuuwa bila kukusudia lakini nilikuwa sijauwa ila nilifungwa bila kosa,kwa vile mauwaji hayo yalipokuwa yakifanyika nilikuwa katika eneo la tukio,na cha kushangaza nilikuwa nashtakiwa mimi peke yangu kuwa ndiye niliyeuwa,ila namshukuru mungu kwa kupata msamaha,” alisema Kerenge
No comments:
Post a Comment