Mawaziri watangaza kujiuzulu Misri
21 Novemba, 2011 - Saa 23:20 GMT
Baraza la mawaziri la Misri limeomba kujiuzulu kufuatia maandamano ya siku tatu kupinga watawala wa kijeshi nchini humo,televisheni ya taifa imeripoti.
Msemaji wa baraza hilo la mawaziri Mohammed Hegazy amesema kwamba ombi lao la kujiuzulu bado halijakubaliwa na baraza la kijeshi linalotawala Misri.
Na wakati msemaji huyo alipokuwa akitoa taarifa,maelfu ya waandamanaji waliendelea kufika katika medani ya Tahrir.
Kufikia sasa zaidi ya watu 30 wameuwawa na wengine wapatao 1,800 kujeruhiwa kutokana na machafuko ya siku tatu yalioshuhudiwa katika mjini Cairo.
Wakereketwa na waandamanaji wamekuwa wakilishinikiza baraza kuu la kijeshi linalotawala kukabidhi mamlaka kwa serikali ya kiraia.
Lakini hatua ya baraza la mawaziri la kutaka kujiuzulu huenda ikaitumbukiza nchi hiyo katika mzozo zaidi wa kisiasa.
Tangazo la kutaka kujiuzulu litatafrisiwa kama ushindi kwa waandamanaji na huenda likawachochea kutoa matakwa zaidi .
Hii pia huenda ikalitatiza baraza kuu la kijeshi.Swali kubwa kwao ni Jee, walirudishe tena baraza hilo lililoomba kujiuzulu au wateuwe baraza jipya? lakini kwa vyovyote vile kutakuwa na shinikizo za kutaka serikali ya kiraia ipewe uwezo zaidi.
Katika kipindi kizima cha maandamano, baraza hilo la kijeshi limekuwa likilaumiwa kwa kujipa madaraka makubwa.
No comments:
Post a Comment