PATA HABARI MOTO MOTO, ZA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA HAPA, TUPE MAWAZO YAKO TUYAFANYIE KAZI, TUPE HABARI ZOZOTE ULIZO NAZO TUTAZIWEKA HAPA,KWA MWENYE PARTY AINA YOYOTE INAYOHUSIANA NA MAMBO YA MUSIC, TAFADHARI ONGEA NA PAPAYA KUPITIA NAMBA HII..07501 202029..YUPO MACHO 24/7 BEI MAELEWANO.

Monday, 10 October 2011

WAMASAI KILOSA WAPANIA KUTOKOMEZA MILA POTOFU

Image
MSAMIATI wa ‘mfumo dume’ au ‘mila potofu’ umekuwa ukitekelezwa na baadhi ya makabila
nchini kwa karne nyingi. 

Katika dunia ya sasa ya Sayansi na teknolojia, inayoifanya dunia kuwa kijiji , mfumo huo hauna nafasi tena na umepitwa na wakati.

Kwa sasa makabila mengi yameondokana na kukumbatia mila potofu, ambazo zilichangia kukwamisha maendeleo yao,ukiwemo mfumo dume uliowanyima watoto wa kike kupata haki yake ya msingi ya elimu.

Lakini, pamoja na mila na desturi hizo kupungua katika makabila mengi , bado baadhi ya wafugaji wa Jamii ya Kimasai, wamekuwa kikwazo cha kuondokana na mila hizo.

Katika makala haya, wanaharakati wa jamii ya wafugaji wa Kimasai wa vijiji vya Parakuyo, Twatwatwa na Ngaite Tarafa ya Kimamba Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, wameamua
kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya kupambana na wazazi wenye tabia ya kuwaozesha wanafunzi wa kike wenye umri ndogo kwa baadhi ya wazee wa kimasai.

Wanaharakati hao wanasema, Wazazi wenye watoto wa kike wanaosoma shule za msingi na Sekondari katika vijiji vya wafugaji ndani ya Wilaya ya Kilosa na mkoa wa Morogoro,
huwaachisha masomo watoto wao wa kike na kwenda kuwaozesha kwa njia ya siri kwa ndoa za kimila, wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji na wa kimila kuandika taarifa za uongo.

Taarifa hizo ni pamoja na zinazoeleza magonjwa sugu na matatizo ya kifamilia. Wengine hudiriki kuandika taarifa hewa za vifo vya watoto, huku watoto hao wakipelekwa katika vijiji
vingine na kuozeshwa pamoja kufanya njama za kuwaombea uhamisho hewa wa shule , jambo ambalo linawarudisha nyuma jamii hizo katika kutetea haki za watoto wa kike.

Pamoja na hayo wanafichua juu ya mtandao wa kuwahujumu watoto wa kike wanaosoma shule kwa wazazi na viongozi wa vijiji na wa kimila, kuwarubuni walimu wakuu wa shule za msingi na Sekondari, wakidai kuwa mstari wa mbele katika kupokea fedha kwa ajili ya kutoa taarifa za uongo, juu ya kuacha shule kwa watoto hao wa kike wa jamii ya wafugaji.

Mambo mengine ambayo wanaharakati hao wameamua kupambana nayo ni unyanyasaji unaofanywa kwa mtoto wa kike, wakiozeshwa wakiwa watoto wadogo kwa wazee wa jamii hiyo kuwa wake wadogo, kutokana na wazee hao kuwa na wake zaidi ya wawili.

“Jamii yetu imekuwa ikiwakosea sana watoto wa kike, huku tukizidi kujilaumu kuwa mila hizi zinazoonekana ni mbaya zaidi wa mtoto wa kike, mbali na kuozeshwa wakiwa na umri mdogo pia wanaozeshwa kwa wazee walio na wake zaidi ya wawili, na kuwafanya wakizidi kuwa watumwa kwenye ndoa zao kutokana na kuwa na umri mdogo,” wanaelezea jambo hilo.

Wanaharakati hao wa kijiji cha Parakuyo na Twatwatwa, wanasema kuwa watoto hao mara nyingi wanaolewa na wazee ambao wana mali nyingi na mifugo mingi.

Wazee hao hukosa watu wa kuhudumia mifugo hiyo hususani ndama, hivyo huamua kuoa watoto wadogo ambao jukumu lao ni kuangalia ndama huku wake wengine wakubwa wakipangiwa majukumu mengine, kama kuchota maji, kuangalia ng’ombe, kukamua maziwa na kupika.

“ Mila zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya jamii ya wamasai hususani wanawake, kulingana na mabadiliko ya maisha ya kila siku ya mwanadamu, hali ambayo baadae
huwafanya watoto hao kuhangaika na hali ngumu ya maisha,” anasema mwanaharakati mmoja wa kijiji cha Parakuyo.

Katika kupambana na tatizo hilo, wanaharakati hao Septemba 13, mwaka huu, wamewasilisha majina ya wanafunzi wa kike 12 kutoka jamii ya wafugaji wa kabila hilo. Wanafunzi hao walifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kupangiwa kuanza masomo ya kidato
cha kwanza Shule ya Sekondari ya Parakuyo, wameozeshwa ndoa za siri kwa wanaume wajamii ya kifugaji.

Pamoja na kuwasilisha majina hayo, wanaharakati hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi
wameanza kuwafichua wazee wa kimasai, wanaooa wanafunzi wa kike baada ya kupata baraka za wazazi wa watoto hao, akiwemo mfugaji mmoja wa kijiji hicho mwenye miaka 55.

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Parakuyo wa Jamii ya wafugaji, Agnes Mataya, anasema watoto wa kike ndiyo wanaopata shida wanapohitimu darasa la saba , pamoja na kufaulu,
wazazi wamekuwa wakiwatorosha kuwapeleka maeneo ya mbali ili baadaye waozeshwe.

“Hili ni tatizo kubwa katika vijiji vya wafugaji wa jamii yetu, mtoto wakike anapochaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari, njama zinafanyika baadhi ya wazazi ya kuwatorosha
kwenda sehemu za mbali ili baadaye waweze kuonzeshwa kwa wanaume wa jamii hiyo kwa tamaa ya kupata ng’ombe wengi,” anasema Mjumbe huyo.

Watoto wanafaulu sana katika shule zetu za msingi , lakini bado wengi hasa wasichana wanachepuka pembeni , wanatoroshwa na wazazi wao ili waozeshwe na jambo hilo halifuatiliwi
kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kijiji wanahusika nalo.

Kwa upande wake, Mwenyeviti wa Vitongoji vya Kijiji cha Twatwatwa , Samwel Okeshu, aliwasilisha orodha ya majina ya wanafunzi wa kike wa jamaii hiyo mbele ya uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kilosa na Mkoa .

Wanafunzi hao walitakiwa kuanza masomo ya Sekondari Parakuyo mwaka jana ,lakini walitoroshwa na wazazi wao, kwa lengo la kuwaozesha kwa wanaume wa jamii hiyo.

Wanafunzi hao wa kike ni aliyeolewa kuwa mke wa nne na mfugaji aliyetoweka kijijini hapo kutokana na kusakwa na Polisi, na mwingine aliyerejeshwa kuendelea na kidato cha kwanza Sekondari Parakuyo.

Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati hao wa Kabila la kimasai wanaotaka maendeleo ya elimu kwa watoto, walidai kuwa baadhi ya wanafunzi hao wamefichwa kwenye maboma
wakiandaliwa kuozeshwa.

“Watoto wa kike waliochaguliwa kujiunga na Sekondari yetu ya Parakuyo, lakini wazazi wamewahonga ng’ombe baadhi ya viongozi wetu na wamekuwa wakificha taarifa hizo , kesi zinakuandaliwa dhidi ya wanaohusika na jambo hili vinavurugwa na Viongiozi wetu wa vijiji ambao ni wafugaji wa jamii hii,” anasema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wafugaji ya Parakuyo, Andulile Mwasampeta, anasema mwaka 2009 wanafunzi wawili wa kike moja wa darasa la sita na mwingine la saba, walipata mimba wakiwa shuleni na suala hilo liliachwa mikononi mwa Uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Parakuyo na Polisi.

Mwalimu Mkuu huyo shule ya msingi Parakuyo, anasema mwaka huu shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 501 , ambapa 67 wamehitimu darasa la saba. Mkuu wa Shule ya Sekondari Parakuyo, Peter John , anasema, wanafunzi wengi wanaochanguliwa kuanza masomo hawafiki wote .

“Tunapangiwa idadi ya wanafunzi wengi, lakini wanaoripoti ni wachache na wanaokuwepo shuleni mahudhurio yao si mazuri hasa kwa kundi hili la wasichana, wanaathiriwa kwa
wakukaa nyumbani na wanaolewa kutokana na wazazi kulipwa ng’ombe wengi na wavulana ni wachungaji,” anasema Mkuu huyo wa Sekondari.

No comments:

Post a Comment