Wednesday, 26 October 2011

TAASISI ZA KIISLAMU ZAISAFISHA CHADEMA


TAASISI ya Kiislamu ya Islamic Peace Foundation (IPF) kwa kushirikiana na Baraza la Mikutano ya Kiislamu (BATAMIKI), zimesema Chadema si chama cha kidini.

Tamko hilo walilitoa jana kwa vyombo vya habari na kudai kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na dhana waliodai imeenezwa katika jamii ya Watanzania na Waislamu nchini kuwa Chadema ni chama cha kidini.

“Tunatoa mwito kwa Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla kuipuuza dhana hii na kuwapuuza wale wanaoieneza ili tuwaunge mkono watu wote wanaotetea maslahi ya wanyonge na rasilimali za taifa letu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa IPF, Shehe Sadik Godigodi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi wa taasisi hizo baada ya kutafakari dhana hiyo na hatima ya Taifa, wamebaini kuwa hakuna ukweli wowote wa jambo hilo bali ni propaganda.

Taarifa hiyo pia imewataka Watanzania kupuuza propaganda hiyo kwa kile ilichodai kuwa haikuanzia Chadema, bali katika Chama cha Wananchi (CUF).

Shehe Godigodi alidai kuwa CUF ilidaiwa ni ya kikabila na kidini (Uislamu) na kuleta athari kubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

“Hali kama hiyo sasa tunaiona inajitokeza ndani ya Chadema ambacho mwanzo kiliitwa cha kikabila kwa maana ya chama cha Wachaga.

“Lakini baada ya chama hicho kuimarika katika uchaguzi wa mwaka 2010 kama ilivyokuwa kwa CUF, kikabadilishiwa wimbo na kuwa chama cha udini yaani Ukristo,” ilieleza taarifa hiyo.

Viongozi wa taasisi hizo katika taarifa yao hiyo wamedai kuwa udini ndani ya Chadema haupo kwa kuwa chama hicho kama vilivyo vyama vingine kina Waislamu, Wakristo na wasio na dini.

Waliwataka Waislamu kutowabagua wenzao walio katika chama hicho kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha matakwa ya dini ya Kiislamu.
 
   
 
Jumla Maoni (4)
   
Maoni hakika nawapongeza gwiji la habari nyie ni jogoo la habari maana mnaandika hata habari za kuwajenga wapinzani kuliko magazeti mengine yanayolenga kujenga upande mmoja.hongera sana.
   
Maoni Propaganda katika chama chochote cha siasa sio kitu kizuri. Umoja na mshikamano ndio kituo muhimu katika jamii na taifa kwa ujumla.
   
Maoni Kwa pamoja tushirikianane kulijenga taifa letu,hasa taasisi za kidini kwasababu nchi yetu ni wamoja hatukujengeka ktk udini&ukabila ht Mwlm Nyerere alpnga vikali mambo hayo,Mungu Ibark Tanzania
   
Maoni Uzalendo wa namna hii ndio utakao tukomboa Watanzania. Tusikubali kuyumbishwa na propaganda za wanasiasa.. Bg up IPF & BATAMIKI.

Mungu ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment