Monday, 10 October 2011

HUYU NDIO LUCY KOMBA, MWIGIZAJI ALIYEWAIBUA MZEE CHILO, IRENE UWOYA

KILA kukicha tasnia ya uigizaji wa filamu hapa nchini imekuwa ikikua, wengi wa wasanii hualikwa au kuitwa kushiriki, lakini tofauti na msanii Lucy Komba ana uwezo wa kutunga, kuigiza kwa kuvaa uhusika na ana kampuni yake aliyodhamiria kufika mbali katika sanaa hiyo.

Si kwamba ana vipaji vya kuigiza, kucheza sarakasi, uchoraji na hata kuimba pekee, bali pia Lucy ni miongoni mwa vipaji ambavyo vimeweza kuibua vipaji vingine katika filamu, tena ndani ya muda mfupi.

Huwezi kuamini kuwa, Lucy aliyezaliwa miaka 29 iliyopita, ndiye aliyewaingiza kwenye ulimwengu wa filamu nyota mahiri wa sasa kama Mzee Chilo (Ahmed Olotu), Irene Uwoya na mwigizaji mahiri wa vichekesho, Mkwele.

Katika mazungumzo yaliyozaa makala haya, Lucy anasema kwamba, ndoto yake ya kuzama katika filamu ilipata nguvu baada ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2002, msukumo mkubwa ukitokana na kipindi cha Mambo Hayo kilichokuwa kinarushwa na kituo cha ITV, kwa kiasi kikubwa akivutwa na Waridi, msanii wa kike aliyetamba sana wakati huo. “Nilikuwa najisemea kuwa ‘ninatamani kuwa kama yule dada (Waridi), tena niwe zaidi yake.”

Anasema kwamba, Tuesday Kihangala “Mr. Tues” ndiye aliyeifanya ndoto yake kuwa kweli, kwani alikutana naye njiani, huku wote wakiwa hawafahamiani, lakini mazungumzo yao yaliishia kwa Lucy kuingia katika kambi ya kurekodi igizo.

“Nilikutana naye njiani, nikimpeleka rafiki yangu saluni, baada ya kukutana naye akaniambia nina sifa za kuwa mwigizaji, nikamwambia siwezi kwa kuwa nina aibu, ingawa nilitamani.

“Alinishawishi, akanipeleka kuangalia walivyokuwa wanarekodi Kinondoni pale kwa Manyanya. Baada ya kuangalia kazi iliyofanyika, hapo ndipo nilipoona kuwa nina uwezo wa kuigiza, tena bila aibu.

“Niliamua kujitosa katika fani ya uigizaji, baada ya kuona kuwa kuna changamoto nyingi ambazo ningeweza kuzifanyia kazi, na hatimaye kuzirekebisha kabisa na hivyo kuifanya sanaa ya Tanzania sio tu kutumika kama ajira, bali kama njia mojawapo ya kuingiza pato kwa serikali.”

Haikumchukua muda, akajikuta akiwa miongoni mwa wasanii waliounda kundi la Fukuto Arts ambako kazi yake ya kwanza ilikuwa kutengeneza igizo la Valentine’s Day ambayo ilikuwa ya wiki nne, aliyoigiza akiwa na wasanii wengine kama Ndende (Khamis Mussa) na Semolina.

“Siku ya kwanza naonekana kwenye runinga, nilijisikia furaha kwa sababu niliona ndoto yangu imeshatimia, hata familia yangu ilifurahia pia na mama yangu ananipa moyo mpaka kesho, naamini kama baba angekuwa hai angefurahia pia.”

Lucy anasema kuwa alifuatia kuigiza katika tamthiliya ya Rangi ya Chungwa ambayo aliigiza kama msichana wa kazi wa Mr Tues ambapo Ndende, “ wakati huo tukiigiza na msanii Winta aliyekuwa mchumba wa Tues na hapo palitokea patashika kutokana na mimi kutomkubalia matakwa yake.”

Lakini kutokana na maslahi kuwa duni, Lucy na wasanii wenzake, akiwamo Frank (Mohammed Mwikongi) walijiengua na kuanzisha kundi la Dar Talents. “Tulianza kwa kurekodi vichekesho, lakini tatizo la maslahi liliendelea kutuandama, ndipo rafiki yangu Mage aliniambia tuhame, lakini mimi nilimtaka tuvumilie kuliko kuhamahama. Lakini siku moja tukiwa tunarekodi komedi yetu ya kwanza tulikutana na Chrisant Mhenga ambaye aliturekodia na baadaye kutushauri tuhamie Kaole.

“Kwa kuwa wakati huo tulichokuwa tukijali ni maslahi, tulikubaliana na ushauri wake na kuhamia katika kundi hilo tukiwa wengi akiwemo Frank na hapo hasa ndipo nyota yangu ilipoanza kung’ara, kwani kupitia tamthiliya mbalimbali niliweza kufanya vizuri zaidi na kujulikana.

Lucy ambaye kwa sasa ni mwajiriwa wa Wizara ya Sheria na Katiba, akiwa Katibu Muhtasi katika Mahakama Kuu ya Tanzania tangu mwaka 2003, akiwa Kaole aliweza kuigiza katika Jahazi na Dira ambako aliigiza kama msichana mshamba, nafasi ambayo anasema anaipenda kutokana na kutohitaji mbwembwe, zaidi ya uhalisia wake.

Lucy alilazimika kuhamahama kusaka mafanikio kisanii na maslahi, je hali ilikuwaje Kaole? Anasema: “Kusema kweli nikiwa Kaole hakukuwa na maendeleo, kwani kwenye vikundi hakuna hela, utakuja na nauli yako na kama huna basi utashindwa kutokea na kama ndio hufanyi kazi na mzazi hana uwezo, basi ndio shida inazidi.

“Lakini kwa upande wangu nashukuru Mungu nilikuwa nakwenda kila wakati na kufanikiwa kushiriki katika tamthiliya kadhaa, lakini kwa waliokwama, hawakumudu kwa sababu hata pesa ya kula ilikuwa haitolewi.”

Hata hivyo anasema kwamba, licha ya kupenda sanaa, hakujisahau sana, kwani aliendelea na masomo katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Magogoni jijini Dar es Salaam na baada ya kuhitimu aliajiriwa Mahakama Kuu, akiwa Katibu Muhtasi.

Na kidogo alichokipata alikitumia kujiendeleza kimasomo, safari hii akiibukia katika masuala ya Teknolojia ya Habari (IT) na baada ya kuhitimu, alikipa kisogo kikundi cha Kaole na kuamua kujiajiri. “ Niliona hakuna haja ya kurudi kwenye kikundi , hasa kutokana na kuwa nilipokuwa chuoni niliandika hadithi ambayo ndiyo iliyozaa filamu ya Utata.

“Nilipeleka ile hadithi kwa (William) Mtitu, alipoiangalia aliisifia kuwa ni nzuri na alinishauri niiandikie script, alikuwa hajui kama mimi najua kuandika alijua kuwa ningeomba anisaidie au niipeleke kwa mtu mwingine.

Baada ya kuikamilisha nilimpelekea tena akasema nimeandika vizuri. Hapo aliniuliza ‘je, una fungu?’ mimi nilimwambia ninalo. Anapozungumzia filamu ya Utata aliyoitoa mwaka 2006, Lucy anasema: “ Kwa vile nilikuwa naaza niliwatumia akina Thea (Ndumbangwe Misayo), Chekibudi (Nurdin Mohammed) na Mzee Chilo (Ahmed Ulotu) ambaye ndio alikuwa anaingia kwenye nyanja ya filamu kwa mara ya kwanza.

“Ninashukuru kuwa mpaka sasa Utata inafanya vizuri kwenye soko, hii imetokana utengenezaji wangu, kwani najitahidi kuwaongoza wasanii waegemee kwenye kufanya uhalisia wa mambo wanayoigiza hususan yenye maadili na tamaduni.

Anasema mara baada ya kutoa Utata mwaka uliofuatia alitoa filamu ya Yolanda sehemu ya kwanza na pili ambayo inahusu manyanyaso wanayopata wanawake wajane baada ya kufiwa na waume zao, filamu hizo zilipendwa na kukubalika katika jamii kutokana na hadithi kugusa maisha ya kawaida ya jamii.

“ Yolanda ndio niliyomtoa msanii Irene Uwoya, nilimshawishi kuingia na ilikuwa ni filamu yake ya kwanza, lakini aliweza kufanya vizuri.” Lucy anasema kuwa mwaka huo huo, alitoa mfululizo wa Komedi ya Vice Versa na kufuatiwa na filamu ya Zako Ama Zangu aliyoitoa mwaka 2008 na pia ndio filamu iliyowaibua wasanii Jacqueline Wolper na Home Joshi.

Mwaka 2008 pia alitoa filamu ya Kipenzi Changu ambayo aliwashirikisha Jacqueline Wolper na OM, Joshi na Tito na mwaka 2009 alitoa filamu ya Cleopatra sehemu ya kwanza na ya pili na ndiyo iliyomtambulisha Sahara Juma aliyeigiza Cleopatra katika ulimwengu wa filamu.

“Filamu ya Cleopatra ilikuwa na sehemu mbili, lakini kila moja ikiwa na hadithi yake, yaani filamu ndani ya filamu na Nani kama Mama. Pamoja na kuwa na hadithi mbili tofauti na zimewavutia sana watu kutokana na kuigusa jamii,” alisema.

Lucy alisema kuwa pia alitengeneza filamu ya Fedheha sehemu ya kwanza na ya pili ambayo kwa sasa iko sokoni kwa takribani wiki mbili au tatu. “Lakini kwa sasa kuna filamu mbili, Zaidi ya Rafiki ambayo muda wowote nitaipeleka sokoni baada ya mambo fulani kukamilika na pia nimeshaanza maandalizi ya kuandaa filamu ya Twiniter Show.

“Katika filamu hizo ambazo ziko jikoni pia nimewashirikisha wasanii chipukizi na nadhani ni wasanii ambao watatikisa katika ulimwengu wa filamu kutokana na uwezo wao wa kubeba uhusika,” alisema.

“Mimi napenda kuibua wasanii wapya na sio kwamba kila siku unakuwa na watu walewale, nina imani kuwa filamu zangu zinauza kwa sababu watu wananijua, hivyo hata kama nitachezesha watu sio maarufu filamu zangu zitauzwa, kwa sababu nina kipaji cha kuwaibua watu wapya.”

Wengine anaoringia kuwaibua ni pamoja na Mkwele wa kikundi cha Mizengwe, Dino, Godliver Vedasto, Mohammed Sultan na Hemed Kavu. Changamoto alizokutana nazo Lucy anasema: “Nilipokuwa Kaole nilikutana na watu maarufu, si unajua asilimia kubwa ya wasanii maarufu wamepitia kwenye kundi hilo, hapo nilikutana na wanaume wenye tamaa ambao wakimuona binti mpya, basi kazi yao ni kutongoza.

Nashukuru Mungu nilijiunga na kundi hilo nikiwa nina uzoefu nikiwa nimetokea vikundi vingine hivyo haikuwa rahisi kudanganyika. “Ila pia uwoga ulikuwepo kwani niliona naweza kupigwa chini, kwani palikuwa na watu wenye vipaji, nilipopata nafasi nilifanya kweli, tamthiliya ya kwanza tu niliweza kung’ara pamoja na kuwa nilianzia katikati.

Anaongeza: “Nakumbuka katika filamu hiyo nilicheza kama mpenzi wa Dk. Cheni (Mahsen Awadh) ambaye nilikuwa changudoa niliyefugwa na Bi Hindu (Chuma Suleiman) nashukuru nilicheza vizuri na niligusa hisia za watu na walinikubali.“

Anapozungumza kujipanga na majukumu ya kazi, familia na ya kiusanii, Lucy anasema kuwa kutokana na kuwa na nia katika fani hiyo inamlazimu kujipanga na kutekeleza hayo yote kwa wakati muafaka.

“Ni ngumu hasa ukizingatia kuwa mimi ni mtunzi na naandika mpangilio wa filamu kunakuwa na ugumu, lakini kutokana na kupenda na kuwa na nia mambo yote nayapanga ipasavyo, muda wa kazi nafanya kazi saa 11 ninaporudi nyumbani na kumaliza kumhudumia mwanangu, baadaye nakaa kwenye kompyuta na kuendelea na kazi za sanaa na mara nyingi nimekuwa nachelewa kulala, kila siku nalala saa sita, saa saba.

“Inapofika kazi ya kufanya uzalishaji wa filamu basi mara zote natumia siku za mwisho wa wiki wakati wa mapumziko na pia ninapokuwa likizo. Lucy anaeleza changamoto nyingine kuwa uwezo mdogo wa kifedha na wizi wa kazi za wasanii ndio changamoto kuu inayowakwamisha kufukia malengo yao katika uigizaji.

“Wakati mwingine huhitaji gharama kubwa sana kuyafikia maeneo halisi yanayohitajika, hivyo inatulazimisha kutumia maeneo ambayo si sahihi ili kukwepa gharama. Kwa mfano tunatakiwa kuigiza mbugani, lakini kutokana na uwezo mdogo tunaishia kwenda bustani za wanyama za mijini,” anasema.

Lucy anaongeza: “Wakati natengeneza filamu yangu ya kwanza ya Utata kwa kubana nilitumia shilingi milioni 5. Zamani ukitaka kuigiza kwenye hoteli walikuwa hatutozwi fedha kwani walikuwa wanajua wanatangaziwa biashara zao, lakini sasa wanajua kuwa tunapata ndio wanalipisha fedha.

“Kama unataka kumtumia msanii maarufu basi ujue utatumia fedha nyingi ambazo hufikia milioni moja. Siku hizi sanaa ya uigizaji ni biashara, zamani ulikuwa ukimwita anakuja kucheza bure, lakini sasa hivi kwa malipo.”

Mafanikio katika kazi ya sanaa Alisema kuwa sanaa imemsaidia kwa kiasi kikubwa katika maisha yake, “ Imenisaidia kwa kweli, kwa sasa nina uwezo wa kuchagua navaa nini nakula nini, niko kwenye gari langu au la kukodi, nina uwezo wa kupanga nyumba ya bei kubwa, ingawa kwa sasa niko katika harakati ya kujenga nyumba ambayo bado haijakamilika.

Anasema kuwa amefungua Kampuni ya Poyaga Production jijini Dar es Salaam ambayo inatumiwa katika kuzalisha na kusambaza kazi zangu, na filamu zilizotengenezwa kupitia kampuni hiyo kuwa ni Cleopatra, Kipenzi Changu na Zaidi ya Rafiki.

Akizungumza tofauti ya mapato wakati akiwa anafanya kazi zake kwenye kampuni zingine, Lucy anasema mapato ya sasa yameongezeka ukilinganisha na pale alipokuwa akisambaziwa na watu wengine, ingawa wamekuwa wakikumbana na tatizo la kuchelewesha kulipa fedha.

“Kazi unayoisambaza mwenyewe unaimiliki, unaweza kufanya chochote, lakini ukipeleka kwa mtu akusambazie anataka amiliki kila kitu na inakuwa siyo yako tena na wala huwezi kuwa na maamuzi yoyote. Na nimependa kusambaza mwenyewe itasaidia familia yangu, mimi sipo wenyewe watanufaika na kazi zangu,” anasema Lucy anayevutiwa na Genevieve Nnaji wa Nigeria.

Malengo yake ya baadaye Anasema kuwa kwa sasa amejikita kuiboresha Kampuni yake ya Poyaga Production, akiwa na dhamira ya kununua mitambo ya kudurufu mikanda ikiwa ni lengo la kuinua biashara na fani ya filamu nchini.

Historia ya Lucy inaonesha kwamba, alizaliwa Oktoba 24, mwaka 1980 jijini Dar es Salaam, likiwa moja ya matunda ya ndoa ya Francis Komba (sasa marehemu) na mkewe, Marietha ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Polisi. Komba alikuwa mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Lucy alipata elimu ya awali katika Shule ya St. Peter’s, Oysterbay na baadaye kujiunga na elimu ya msingi Shule ya Oysterbay. Na baadaye alimaliza elimu ya kidato cha nne na sita huko Olaleni na Kibosho Sekondari.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alijiunga na Chuo cha Magogoni kwa kozi ya Uhazili na baadaye Chuo cha Learn IT kwa mafunzo ya Kompyuta. Lucy amebahatika kupata mtoto mmoja, Strom Mbasha aliyezaa na mchumba wake, Patrick Mbasha, mdogo wa Emmanuel Mbasha ambaye ni mume wa msanii wa muziki wa Injili, Flora Mbasha. Huyo ndiye Lucy Komba ambaye hivi sasa ni Katibu Muhtasi katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment