Monday, 10 October 2011

BRAZIL KUISAIDIA TANZANIA TATIZO LA UMEME


Braazil imeahidi kuisaidia Tanzania kondokana moja kwa moja na shida ya umeme kwa kutoa teknolojia na uwezo wake chini ya uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Madini na Nishati wa Brazil, Edson Lobao katika mazungumzo rasmi ofisini kwake mjini Brasilia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,  ambaye anaitembelea nchi hiyo.
Lobao alisema Brazil ina uzoefu mkubwa katika teknolojia ya kufua umeme na akasema ataliagiza Shirika la Nishati ya Mafuta la Brazil, PETROBRAS, kuangalia namna gani ya kushirikiana na Tanzania katika eneo hilo.
PETROBRAS, ambayo pia inashughulikia uzalishaji wa umeme kwa nguvu ya maji, tayari inatafuta mafuta na gesi nchini Tanzania kwenye pwani ya Mtwara.
Brazil tayari imeonyesha nia ya kuisaidia kiufundi Tanzania katika ujenzi wa kinu kikubwa cha kufua umeme kwa nguvu ya maji kwenye eneo la Stegler’s Gorge, kwenye mto Rufiji. Juzi Waziri Mkuu Pinda pia alikuwa na mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Mifugo wa Brazil, Jorge Alberto Portanova Mendes Ribeiro Filho, na Waziri wa Maendeleo Vijijini, Afonso Florence.
Jana Pinda alitarajia kutembelea kituo cha Utafiti wa Kilimo cha EMBRAPA na leo atatembelea Jiji la Rio de Janeiro.
Tayari alikwishatembelea Sao Paulo ambako, pamoja na mambo mengine, alitembelea Makao Makuu ya Kampuni ya ABIMAQ inayotengeneza zana za Kilimo na kiwanda cha sukari cha Costa Pinto ambacho pia hutengeneza kutokana na miwa kemikali ya Ethanol inayotumika kwa nishati.
waziri mkuu, mizengo pinda

No comments:

Post a Comment