Majibizano ya risasi yaua mmoja Cameroon
Watu wenye silaha wamefyatua risasi katika mji mkuu wa kibiashara nchini Cameroon, Douala, na kuua mtu mmoja katika maandamano ya kupinga serikali.
Taarifa zinasema watu hao walikuwa wamevaa sare za kijeshi na walibeba mabango yanayomtaka Rais Paul Biya kuachia madaraka.
Bw Biya anatarajiwa kushinda uchaguzi wa rais utakaofanyika Oktoba 9.
Amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30 na ni mmoja kati ya marais wa Afrika wanaaongoza kukaa madarakani kwa muda mrefu.
Mwaka 2008 alibadili katiba na kuondoa vipengele vinavyoweka kikomo cha urais na kusababisha vurugu nchi nzima.
Katika tukio hilo la Alhamis, watu hao wenye silaha waliweka vizuizi umbali wa maili moja katika daraja la Wouri na kuwaruhsia risasi polisi kwa saa kadhaa.
"Kulikuwa na majibizano makali ya risasi na mmoja wa wenye silaha alitumbukia katika mto Wouri. Haijulikani kama amezama’ alisema Itah Robert mtu aliyeshuhudia.
Mtu mwingine ameliambia shirika la habari la AP kuwa watu hao walibeba mabango yenye maandishi:"Paul Biya lazima aondoke kwa gharama yoyote" na "Paul Biya dikteta".
Vikosi vya usalama vimewakamata baadhi ya watu hao.
Kurushiana risasi kuliweza kusikika kwa saa kadhaa baadaye na askari wenye silaha wamesambazwa katika mji wa Douala kutafuta magari hayo.
Wagombea ishirini na wawili wanashindana na Bw Biya mwenye umri wa miaka 78 akiwemo John Fru Ndi, mgombea mzoefu kutoka chama cha upinzani cha Social Democratic Front (SDF).
Jumanne, chama cha SDF kilikosoa utaratibu wa upigaji kura.
"Kuna mlima wa matatizo kwa ujumla," Evariste Fopoussi, msemaji wa chama cha upinzani cha SDF aliliambia shirika la habari la AFP, akielezea kuandikishwa mara mbili na kukosekana kwa baadhi ya majina katika orodha ya wapiga kura.
No comments:
Post a Comment