TANZANIA imesaini mkataba wa makubaliano ya kuanzisha kampuni ya ubia itakayosimamia miradi miwili mikubwa ya kuzalisha umeme na chuma ya Liganga na Mchuchuma yenye thamani ya dola za Marekani bilioni tatu sawa na Sh trilioni 4.3.
Miradi hiyo ambayo uanzishwaji wake ulisimama kwa muda mrefu, sasa inatarajiwa kuzalisha megawati za umeme 600 kwa kutumia makaa ya mawe eneo la Liganga na kuzalisha chuma tani milioni tatu kwa mwaka katika eneo la Mchuchuma, yote mkoani Iringa.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, alisema ubia huo baina ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya China ya Sichuan Hongda, una maana kubwa kwa Watanzania
kutokana na mradi husika utakuwa chachu ya kuimarika kwa uchumi na viwanda nchini.
“Nafahamu kuwa miradi hii ya umeme na chuma itasaidia kuifungulia fursa Tanzania katika maeneo ya biashara ya chuma, lakini pia katika maeneo ambako miradi hii iko, miundombinu kama vile Bandari ya Mtwara, reli na barabara vitaimarika,” alisema Bilal.
Alisema kutokana na ukweli huo, utekelezwaji wa miradi hiyo ni chachu ya uchumi wa Tanzania na kwamba sasa Watanzania wengi watapata fursa nzuri ya kuondokana na umasikini, hivyo Serikali itahakikisha inasaidia kwa hali na mali utekelezaji wake bila kuruhusu ulimbikizaji au urasimu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk. Chrisant Mzindakaya, alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni muendelezo wa mchakato wa zabuni ulioanza tangu mwaka 2007 ambapo Sichuan Hongda iliibuka mshindi kati ya kampuni 48 za kimataifa zilizojitokeza kuomba zabuni hiyo, kutokana na historia yake ya uzoefu katika masuala ya nishati na madini lakini pia uwezo kifedha.
Alisema pamoja na mkakati huo kuchukua muda mrefu, mbia huyo ambaye kwa pamoja na NDC wameunda Kampuni ya Tanzania China Minerals Resources Ltd, itaanza mara moja kazi ya kufua umeme na chuma kwa kutumia makaa ya mawe na chuma iliyobainika kuwepo kwa wingi eneo la Liganga na Mchuchuma.
Alisema utafiti uliofanywa umebaini utajiri wa kutosha katika maeneo hayo ambapo Mchuchuma, chuma imeonekana kuwapo mpaka mita 500 kwenda chini hivyo kuwezesha uzalishaji wa tani milioni tatu kwa mwaka wakati mahitaji ya chuma Tanzania ni tani 250.
Alisema kupitia mkataba huo, miradi hiyo ikianza kazi Tanzania itapata mgawo wa asilimia 20 na baada ya kampuni ya ubia kumaliza muda wake, Serikali inaweza kununua hisa za asilimia 49.
No comments:
Post a Comment