Thursday, 29 September 2011


El Amrani Katibu Mkuu mpya Caf

El Amrani
Hicham El Amrani
Hicham El Amrani amethibitishwa kuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Soka barani Afrika Caf.
Uamuzi huo umechukuliwa na kamati kuu ya Caf kwenye mkutano uliofanyika mjini Cairo, Misri.
El Amrani mwenye umri wa miaka 32, alijiunga na shirikiho hilo mwezi Machi 2009 kama naibu katibu mkuu.
Amrani amekuwa akikaimu nafasi hiyo tangu mwezi Oktoba mwaka jana, baada ya kuondoka kwa Mustapha Fahmy aliyekwenda Fifa kuwa mkurugenzi wa mashindano.
Alikuwa mkuu wa idara ya masoko katika shirikisho la soka la bara Asia kabla ya kujiunga na Caf

Sunderland yamsimamisha Bramble

Klabu ya mpira inayocheza katika Ligi kuu ya England, Sunderland, imemsimamisha beki wake Titus Bramble baada ya mchezaji huyo kukamatwa akishukiwa kuwa na dawa ya kuongezea nguvu pamoja na kosa la ubakaji.
Bramble
Titus Bramble
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ambaye hapo zamani alichezea klabu ya Newcastle na Wigan alihojiwa kabla ya kuachiliwa kwa dhamana hapo jana.
Taarifa ya klabu imesema kuwa: "Titus Bramble amesimamishwa wakati majibu ya upelelezi yakisubiriwa.
Taarifa hiyo imeongezea kusema kuwa "mchezaji huyo hatoshiriki mazowezi ya timu au kuwa tayari kuchaguliwa kwa ajili ya kushiriki mechi yoyote kwa wakati huu."
Titus Bramble alianza kucheza soka katika klabu ya mji alikozaliwa wa Ipswich, kabla ya kuhamia Newcastle United kwa kitita cha pauni milioni sita.
Baada ya hapo akajiunga na klabu ya Wigan Athletic kabla ya kurejea kaskazini mashariki alipojiunga na Sunderland mwaka uliopita.
Beki huyo aliyechaguliwa mara kumi kuichezea Timu ya vijana wa England wenye umri ulio chini ya miaka 21, alishiriuki mchuano wa klabu yake ilipofungwa na Norwich 2-1 mnamo siku ya jumatatu.

Fifa tayari kuchukua hatua


Makamu mwenyeki wa shirikisho la soka duniani,FIFA Bw.Jim Boyce amesema kua ikiwa itathibitishwa kua mchezaji Carlos Tevez alikataa kushiriki mechi dhidi ya Bayern Munich kama alivyotakiwa na kocha wake, basi anaweza kuwekewa kikwazo asishiriki mchezo huo kote duniani.
Carlos Tevez
Tevez na bintiye
Boyce ambaye hapo zamani alikua Rais wa chama cha mpira cha Ireland, amesema kua tukio hilo halipendezi.
Aliongezea kusema kua, 'nadhani Fifa iwe na uwezo wa kumuadhibu mchezaji asishiriki kwa njia yoyote ile mchezo wa soka.
Wakati huo huo, klabu ya Manchester city imemsimamisha mchezaji huyo kwa kipindi cha wiki mbili.
Kocha Roberto Mancini
Kocha Roberto Mancini
Katika kipindi hicho cha majuma mawili, mawakili wa klabu hiyo wanachunguza vipengele vya kumfungulia mashtaka endapo mkataba wake utasimamishwa.
Lililo bayana hata hivyo ni kwamba endapo itathibitishwa kwamba mchezaji huyo alikataa kucheza licha ya mwenyewe kukana madai hayo, atakua amekiuka mkataba na hivyo klabu ya Manchester City inaweza kuchana mapatano ya mshahara mkubwa wa pauni lakini mbili kwa kila wiki.
Adhabu ya chini ambayo inaweza kumfika Tevez ni kutozwa faini ya mshahara wa wiki mbili, kama ilivyokubaliwa chini ya makubaliano ya chama cha wacheza mpira wa kulipwa.
Tatizo jingine linalojitokeza ni kwamba kuurarua mkataba wa Tevez ili kupunguza gharama za mshahara mkubwa, miongoni mwa mishahara mikubwa inayolipwa wacheza soka, wakiwepo watatu duniani wanaolipwa mishahara mikubwa' huenda kukamaanisha kupoteza hadi pauni milioni 40 kwa kumfuta kazi mchezaji huyo.
Kuhusu uwezekano wa Fifa kumchukulia hatua, Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Jim Boyce amesema ikiwa mchezaji huyo amefanya kama ilivyodaiwa, na kama klabu yake itamuachisha kazi na ifahamishe Fifa, basi hatua zitachukuliwa kuona kwamba anawekewa kikwazo asishiriki wala kujihusisha na masuala ya soka kote duniani.

Majibizano ya risasi yaua mmoja Cameroon

Rais Paul Biya
Watu wenye silaha wamefyatua risasi katika mji mkuu wa kibiashara nchini Cameroon, Douala, na kuua mtu mmoja katika maandamano ya kupinga serikali.
Taarifa zinasema watu hao walikuwa wamevaa sare za kijeshi na walibeba mabango yanayomtaka Rais Paul Biya kuachia madaraka.
Bw Biya anatarajiwa kushinda uchaguzi wa rais utakaofanyika Oktoba 9.
Amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30 na ni mmoja kati ya marais wa Afrika wanaaongoza kukaa madarakani kwa muda mrefu.
Mwaka 2008 alibadili katiba na kuondoa vipengele vinavyoweka kikomo cha urais na kusababisha vurugu nchi nzima.
Katika tukio hilo la Alhamis, watu hao wenye silaha waliweka vizuizi umbali wa maili moja katika daraja la Wouri na kuwaruhsia risasi polisi kwa saa kadhaa.
"Kulikuwa na majibizano makali ya risasi na mmoja wa wenye silaha alitumbukia katika mto Wouri. Haijulikani kama amezama’ alisema Itah Robert mtu aliyeshuhudia.
Mtu mwingine ameliambia shirika la habari la AP kuwa watu hao walibeba mabango yenye maandishi:"Paul Biya lazima aondoke kwa gharama yoyote" na "Paul Biya dikteta".
Vikosi vya usalama vimewakamata baadhi ya watu hao.
Kurushiana risasi kuliweza kusikika kwa saa kadhaa baadaye na askari wenye silaha wamesambazwa katika mji wa Douala kutafuta magari hayo.
Wagombea ishirini na wawili wanashindana na Bw Biya mwenye umri wa miaka 78 akiwemo John Fru Ndi, mgombea mzoefu kutoka chama cha upinzani cha Social Democratic Front (SDF).
Jumanne, chama cha SDF kilikosoa utaratibu wa upigaji kura.
"Kuna mlima wa matatizo kwa ujumla," Evariste Fopoussi, msemaji wa chama cha upinzani cha SDF aliliambia shirika la habari la AFP, akielezea kuandikishwa mara mbili na kukosekana kwa baadhi ya majina katika orodha ya wapiga kura.

Afrika Kusini kuandaa Kombe Afrika 2013

Shirikisho la Soka Barani Afrika (Caf) limetangaza Afrika Kusini itaandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya Soka mwaka 2013 badala ya Libya.
Uwanja wa Cape Town
Uwanja wa Cape Town
Libya imeichia nafasi ya kuandaa mashindano hayo kutokana na hali kutokuwa shwari nchini humo.
Badala yake Libya itaandaa mashindano ya mwaka 2017, ambayo ilikuwa awali yafanyike nchini Afrika Kusini.
Kubadilishana huko ni makubaliano baina ya nchi hizo mbili ambayo yalifahamika wiki mbili zilizopita.
Wakati huo Caf ilisema tangazo hilo limetolewa mapema mno, huku Nigeria na Algeria pia zilionesha nia ya kuandaa.
Nigeria ilitajwa kuwa nchi itakayosubiri wakati Caf ilipotoa tangazo la awali kuhusu wapi mashindano ya kuuanzia mwaka 2010 - 2014 yatakapofanyika.
Lakini uamuzi wa kufanya mashindano hayo Afrika Kusini, uliidhinishwa na mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Caf unaofanyika mjini Cairo.
Afrika Kusini pia itachukua nafasi ya Libya kuandaa michezo ya mwaka 2014 ya Mataifa ya Afrika, kwa wachezaji wanaotimua ligi za nyumbani.
Mapema mwaka huu waliandaa pia mashindano ya vijana ya Afrika chini ya miaka 20, ambayo Libya ilishindwa kuandaa.
Caf pia ilitangaza nchi mbalimbali zitakazoandaa mashindano kadha makubwa.
Namibia itandaa mashindano ya Wanawake ya mwaka 2014 ya Ubingwa wa Afrika na Niger itachukua jukumu la kuandaa mashindano ya mwaka 2015 chini ya umri wa miaka 17 .
Senegal itakuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2015 chini ya umri wa miaka 20, wakati Madagascar itakaribisha nchi nyingine katika kuwania ubingwa wa mashindano ya umri wa chini ya miaka 17 ya mwaka2017.

MAPENZI KIZUNGUZUNGU


Mwanamama mmoja nchini Brazil alituma mtu akamuue mwanamke aliyekuwa akitembea na mume wake, lakini kwa bahati mbaya au nzuri muuaji huyo akajikuta akipendana na mtu anayetakiwa kumuua.
Mwanamama huyo alihisi kuna mwanamke anayemchukulia mume wake, na hivyo kutafuta mtu atakayemuua mwanamke huyo.
Mke huyo mwenye wasiwasi alitafuta mtu wa kazi, lakini bwana huyo aliyepewa jukumu la kuua, alipendana ghafla na mwanamke anayetakiwa kumuua.
Ili kumaliza sakata hilo bwana huyo aliamua kumpaka rangi nyekudu iliyofanana na damu na kumpiga picha mwanamke huyo na kuituma kwa mwanamama aliyemtuma. Bwana huyo alimwambia tayari amekamilisha kazi.
Hata hivyo mwanamama aliyeagiza mauaji kufanywa aliwafuma mitaani na kwenda kushtaki polisi. Polisi wamewakamata watatu hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

MIAKA 41 BADO HARITAKI KUHAMA KWA WAZAZI


MTOTO KWA MAMA HAKUI?

Bwana mmoja na mkewe nchini Italia wametafuta msaada wa kisheria ili kumshawishi mtoto wao mwenye umri wa miaka 41 kuhama na kutafuta makazi yake mwenyewe.
Wazazi hao ambao hawakutajwa majina, wamesema mtoto wao wa kiume ambaye anafanya kazi amegoma katakata kuhama nyumbani kwa wazazi wake, na bado anataka kufuliwa nguo zake na kupikiwa chakula na wazazi wake. Wazazi hao sasa wametafuta ushauri wa kisheria.
Mwanasheria Andrea Camp amesema wametuma barua kwa mtoto huyo na kumtaka ahame katika kipindi cha siku sita, la sivyo atakabiliwa na hatua za kisheria. Iwapo atagoma kuhama, wanasheria wataomba mahakama mjini Venice kutoa amri ya kuwalinda wazazi hao dhidi ya mtoto wao.
"Tumechoka, na mambo haya" amekaririwa baba wa bwana huyo.
"Yaani ana kazi nzuri lakini hataki kuhama na kuanza maisha yake" amesema mzee huyo. Mzee huyo amesema mtoto wao huwataka wafue nguo zake, na kuzipiga pasi na pia kumtayarishia chakula.
"Nadhani hana nia ya kuhama" amesema baba wa mtoto huyo mwenye miaka arobaini. Hata hivyo wanasheria wamesema familia nyingi nchini himo zinakabiliwa na tatizo hilo.

USIOGOPE SIMU


Serikali ya Nigeria imetoa tangazo kuwahakikishia wananchi wake kuwa hawawezi kufa kwa kupokea simu.
pOKEA
Pokea simu...
Mawaziri katika serikali ya Nigeria wametoa tangazo hilo kufuatia ujumbe mfupi wa maandishi kusambazwa nchi humo, ukisema watu watakufa papo hapo, iwapo watapokea simu iliyopigwa na namba 09141.
Tume ya mawasiliano ya Nigeria imesema "ni jambo lisiloweza kufikirika kuwa mtu atakufa kwa kupokea simu".
Msemaji wa tume hiyo Rueben Muoka amesema "Ni watu wanaodanganywa kirahisi ndio wanaweza kuamini uvumi huu."

Wednesday, 28 September 2011

Hawana jipya wachapwa na Bayern munich 2-0
Waikandamiza Ajax 3-0

Tuesday, 27 September 2011


Handsome wa Kijiji

Director : 
 Vicent Kigosi
Producer: 
 RJ Company
Stars : 
 Vicent Kigosi, Irene Paul, Vaileti Nestory, Flora Mvungi
Story: Vicent Kigosi
Written: Ally Yakuti
Camera Man: Lusubilo Mwanguku
Sound Man: Saidi Barghash
Light Man: Steven Shoo
Edited: Vicent Kigosi
Make Up: Mwasiti Mohamed
Produced: Brandina Chagula
Handsome wa Kijiji ni Filamu iliyokuwa ikisubiria kwa hamu na wadau wengi hapa nchini, yenye mazingira ya kijiji na imeingia sokoni rasmi juzi.
Filamu hiyo inapatikana kwenye maduka yote ya kuuzia kanda hapa nchini, wadau pateni Copy zenu Original ili upate kuona nini Rj Company walichokifanya kwa muda wote huo.

Mauaji yatokea katika maandamano Guinea

Takriban waandamanaji watatu waliuawa kwenye mji mkuu Conakry nchini Guinea, baada ya majeshi ya usalama kuvunja maandamano ya upinzani.
Ripoti zinasema majeshi ya usalama yametumia mabomu ya kutoa machozi na marungu dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe mjini humo.
Guinea
Walitawanya maandamano yaliyokuwa yamepangwa na wanaounga mkono waandamanaji dhidi ya namna serikali inavyojiandaa kwa uchaguzi wa wabunge.
Raia wa Guinea walipiga kura ya uchaguzi wa rais Novemba iliyopita kwa mara ya kwanza tangu kupata uhuru mwaka 1958.
Lakini wanaofuatilia wanahofia kwamba demokrasia ya nchi hiyo inaweza ikawa hatarini.
Uchaguzi wa wabunge ulitakiwa ufanyike katika kipindi cha miezi sita lakini kwa sasa umepangwa kufanyika mwezi Desemba 29 na mamlaka husika pamoja na tume huru ya taifa ya uchaguzi (CENI).
Viongozi wa upinzani wanasema wanahofia uchaguzi utakuwa kama sarakasi.
Mkuu wa upinzani Cellou Dalein Diallo, ambaye alishindwa kwa kura chache katika uchaguzi mwaka jana, amemshutumu Rais Alpha Conde kwa kuweka ushirika wa karibu na mkuu wa CENI na kujaribu kuvuruga daftari la usajili wa wapiga kura.

Ferguson aelezea nguvu za TV katika soka

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema television zina nguvu kupita kiasi katika soka ya Uingereza.
Sir Alex Ferguson
Sir Alex Ferguson

Amedai vilabu vimepoteza udhibiti wa ratiba hali inayoathiri timu zinazocheza soka Ulaya.

Katika mahojiano yake ya kwanza na BBC tangu alipofuta kususia mahojiano na kituo hicho, Sir Alex amesema kwa sababu ya kiasi kikubwa cha pesa ambacho vituo vya televisheni huweka katika michezo, sasa wanaonekana kudhibiti kila kitu.

Alipoulizwa iwapo televisheni kwa sasa zina nguvu sana katika mchezo, alisema "Hakika - unaposhikana mikono na shetani huna budi kujiandaa na yatakayokukabili. Amevifananisha vituo vya televisheni sawa na Mungu kwa wakati huu na kumalizia kusema - ni wafalme.

Sir Alex pia alidai vilabu havina budi kupewa pesa zaidi kutoka vituo vya televisheni. Amesema wasimamizi wa Ligi Kuu ya soka ya England wameuza mechi kwa nchi 200 na akaongeza " unapofikiria hayo sidhani kama tunapewa fedha za kutosha".

Taifa Stars yataja kikosi chake

Tanzania
Taifa Stars

Tanzania imetangaza kikosi kitakachopambana na Morrocco katika michuano ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani.
Taarifa iliyotolewa na chama cha soka cha Tanzania TFF imesema Taifa Stars ambayo inafundshwa na Jan Poulsen itaondoka Oktoba 6 kwenda Morrocco, na kujitupa uwanjani Oktoba 9 mjini Marrakech.
Kikosi hicho cha wachezaji 23 ni:

Makipa:

Shabani Dihile (JKT Ruvu Stars)
Juma Kaseja (Simba)
Shabani Kado (Yanga)

Mabeki:

Shadrack Nsajigwa (Yanga)
Erasto Nyoni (Azam)
Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya)
Amir Maftah (Simba)
Aggrey Morris (Azam)
Juma Nyoso (Simba)
Victor Costa (Simba)

Viungo:

Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway)
Nurdin Bakari (Yanga)
Shabani Nditi (Mtibwa Sugar)
Jabir Aziz (Azam)
Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada)
Mrisho Ngassa (Azam)
Ramadhan Chombo (Azam)

Washambuliaji:

Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam
Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC)
Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam)
Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden)
John Bocco (Azam)
Hussein Javu (Mtibwa Sugar)
Tanzania iko kundi D, pamoja na Algeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Morrocco.
Tanzania ina pointi 5 baada ya michezo mitano na kushinda mmoja, sawa na Algeria. Morrocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati zinaongoza kundi hilo zikiwa na pointi 8.
Chanzo: bbc swahili

Monday, 26 September 2011


Dr Besigye wa Uganda akamatwa tena

Dr Kiiza Besigye
Kiongozi wa upinzani wa Uganda Kiiza Besigye amekamatwa karibu na nyumba yake baada ya kudhamiria kujiunga na maandamano mapya kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Wiki iliyopita pia alikamatwa kutokana na kampeni ya "kutembea kazini" kwa makundi na kupigwa risasi mkononi baada ya kuibuka ghasia baina ya polisi na wafuasi wake.
Viongozi wengine wa upinzani nao wamekamatwa kutokana na maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika kila Jumatatu na Alhamis.
Mwishoni mwa juma, Rais alielezea mpango huo kuwa wa "kipumbavu" na kinyume cha sheria.
Dr Besigye alishindwa na matokeo yake Rais Yoweri Museveni aliibuka mshindi katika uchaguzi wa mwezi Februari huku akidai uchaguzi huo ulifanyiwa hila.
Ameshindwa mara tatu na Bw Museveni katika uchaguzi wa rais, akiwa ameongeza asilimia 26 zaidi ya asilimia 68 za rais huyo mwezi Februari

Shamba la Rais wa Burundi lachomwa moto

Watu wamechoma moto kwa makusudi shamba la mananasi linalomilikiwa na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, maafisa wamesema.
Moto huo umeharibu sehemu ya eneo la shamba hilo kwa upande wa Kusini Mashariki mwa eneo la Musongati, wamesema.
Rais Pierre Nkurunziza
Mwandishi wa BBC Prime Ndikumagenge aliyeko mjini Bujumbura, anasema kumekuwa na milipuko ya maguruneti na mashambulizi ya bunduki nchini Burundi tangu Jumapili.
Serikali inashutumu mashambulizi hayo kuwa yanatoka kwa majambazi, lakini watu wengi wana wasiwasi kuwa uasi huenda ukawa umerejea,
Amesema karibu watu 300,000 waliuawa nchini Burundi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika 2005.
Hali tete imejitokeza tena wakati wa uchaguzi mwaka jana huku wapinzani wakidai kuwa ulitawaliwa na kutishiwa pamoja na kukamatwa na udanganyifu.
Kiongozi wa zamani wa waasi Agathon Rwasa alijiondoa katika kinyang'angiro cha Urais na kuikimbia nchi.
Bw Nkurunziza alikuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo.
Mwandishi wa BBC anasema baada tu ya shamba la Rais Nkurunziza kushambuliwa mwalimu wa shule ambaye ni mwanachama wa chama tawala nchini humo alipigwa risasi na kufa eneo la karibu.
Anasema watu wawili pia wameuawa katika shambulio la guruneti kusini magharibi mwa Burundi na gari binafsi kuvamiwa kaskazini mwa nchi.
Hakuna kikundi chochote kulichokiri kuhusika na mashambulizi hayo.

TUNGEKUA NA WAZEE KAMA HUYU 30 AU 20 AFRICA INGEKUA MBALI KIMAENDELEO


26th September 2011
Chapa
Maoni
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, akisalimiana na wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari ya Wazo Hill, jijini Dar es Salaam. Mengi alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za mahafali ya pili ya shule hiyo yaliyofanyika juzi.
Watanzania wametakiwa kuacha kulalamika kuhusiana na vitendo vya rushwa vinavyoendelea nchini, badala yake wachukue hatua ili kupambana navyo.
Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, katika mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya sekondari ya Wazo Hill.

Alisema katika kupambana na vitendo vya rushwa, wananchi wanatakiwa kusimama imara na kuvipiga vita badala ya kulalamika siku zote.

Aliwaasa wanafunzi hao wa kidato cha nne kuacha tabia ambazo zinaweza kuwaingiza katika kutenda maovu.
Mengi aliahidi kuwajengea wanafunzi kibanda maalum kwa ajili ya kuanikia nguo zao baada yakubainika kwamba hivi sasa wanazianika nje.

Msaada mwingine alioahidi kuipatia shule hiyo ni kompyuta 20, kuwasaidia ujenzi wa maabara pamoja na Sh. milioni mbili kwa ajili ya kusaidia upandaji wa miti shuleni hapo.

Alisema utoaji wa kompyuta hizo ni mwanzo na kwamba siku za usoni kila mwanafunzi anatakiwa kuwa na  ya kwake.

Aliahidi kila mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha nne atamzawadia Sh. milioni moja na kuwaahidi kula nao chakula cha mchama Oktoba 18, mwaka huu.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Radislaus Riwa, alimshukuru Mengi kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo pamoja na misaada aliyotoa kwa shule hiyo.

TIBAIJUKA AZIDI KUWASHUPALIA WAVAMIZI WA MAENEO YA WAZI


Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Profesa. Anne Tibaijuka, amesema mchakato wa kuwafutia hati wavamizi wa maeneo ya wazi uko mbioni kuanza, na kwa kuanzia serikali itabandika mabango ya kuwajulisha wavamizi hao kuondoka la sivyo sheria itachukua mkondo wake.
Profesa Tibaijuka aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara ya wizara hiyo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Prof Anna Tibaijuka akiangalia mfano wa ramani ya mji wa kisasa utakao jengwa Kigamboni katika mipango miji wakati wa Maonesho ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru kwa wizara hiyo ambaye Alisema tayari ana orodha ya baadhi ya wavamizi wa maeneo mbalimbali nchini na atawataja mara baada ya zoezi hilo kuanza.
Msiwe na haraka, mtawafahamu wavamizi hao siku chache tu. Haina haja ya kuwataja hapa kwenye maadhimisho, tutamuondoa mvamizi hata kama ameshajenga katika eneo hilo,” alisema Tibaijuka.
Katika hatua nyingine, Profesa Tibaijuka amewataka wananchi wasijenge katika maeneo ambayo hayajapimwa ili kupunguza migogoro ya ardhi isiyoisha.
Alisema serikali itaongeza juhudi za kupanga miji na kuwezesha upatikanaji wa makazi yaliyopangwa mijini ili kupunguza ongezeko la makazi holela mijini.
Aidha, alisema hadi Juni 2011, jumla ya nyumba 301,961 zilitambuliwa kuwepo kwenye maeneo yaliyojengwa bila kupangwa katika miji ya ya Mwanza, Dar es Salaam, Moshi, Dodoma na Tanga.
Profesa Tibaijuka alisema kuwa sekta ya nyumba inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi na wadau kuhusu sheria, kanuni na miongozo kuhusu masuala ya ardhi.
CHANZO: NIPASHE

Boeing kuwasilisha 787 ya kwanza kabisa


Kampuni ya utengenezaji ndege ya Marekani - Boeing - itawasilisha rasmi ndege ya kwanza aina ya 787 Dreamliner kwa shirika la ndege la All Nippon Airways (ANA) la Japan.
Boeing
Dreamliner
Awali Dreamliner ilipangwa kuwa tayari mwaka 2008, lakini Boeing imekumbwa na mflulizo wa vikwazo, ambapo hivi karibuni moto uliwaka ndani ya ndege za majaribio mwezi Januari.
Ndege hiyo isiyotumia mafuta mengi imetengenezwa kwa kutumia malighafi nyepesi.
Boeing inapanga kutengeneza ndege 10 kwa mwezi kuanzia mwaka 2013.
Ndege hiyo itakabidhiwa kwa ANA katika kitongoji cha Everett, Washington kabla ya kuruka na kwenda Tokyo ambapo itawasili siku ya Jumatano.
Dreamliner
Dreamliner
Boeing imesema ndege hiyo yenye safu mbili na ukubwa wa kati ina madirisha makubwa na hali nzuri ya unyevunyevu ndani ya ndege na hewa safi hali ambayo itaruhusu abiria kuwasili wanapokwenda wakiwa katika njema zaidi.
Lakini matatizo ya Dreamliner yameharibu sifa ya Boeing, na kampuni hiyo ina matumaini kuwa uzinduzi wenye mafanikio utasaidia kufuta ucheleweshwaji uliotokea.

Mashaka

Makamu wa rais wa masuala ya masoko wa Boeing, Randy Tinseth ameiambia BBC: "Huu ni mradi ambao umetoka mbali. Tunaamini itakuwa ndege nzuri.
"Hatimaye tunaona matumaini ya maelfu ya 787 katika siku za mbele."
Alipoulizwa sababu za kuchelewa kutoka kwa ndege ya Boeing 787 Bw Tinseth amesema "kuna mashaka katika kila ndege mpya".
Amesema: "Tumetumia fedha zaidi katika ndege hii kuliko tuliyotarajia, lakini kwa mara nyingine tena bado tupo katika nafasi nzuri, tunaamini mradi huu utaendelea kuwa na faida."

Uzalishaji

Uzalishaji wa Dreamliner kwa sasa unatoa takriban ndege 2.5 kwa mwezi.
Mpaka sasa ndege zipatazo 821 aina ya 787 zinatakiwa kununuliwa kutoka Boeing, ambayo inasema inatumia 20% pungufu ya mafuta yanayotumiwa na ndege za kawaida za ukubwa huo.
Dreamliner
Boeing na Airbus
Ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 290 katika ndege yake kubwa ya 787-9, lakini 787 ni ndogo kuliko jumbo jet 747 ya Boeing.
Hata hivyo, Boeing inadhani kuwa 787 itakuwa maarufu katika makampuni ya ndege, kwa kuwa itakuwa na uwezo wa kuruka moja kwa moja kwenda katika viwanja vidogo vya ndege.

Mahasimu

Mahasimu wa Boeing wa Ulaya, Airbus, kwa sasa inatengeneza mshindani wa moja kwa moja wa 787, iitwayo Airbus A350 XWB.
Airbus imepokea maombi ya ununuzi yanayozidi ndege 550 ya A350 XWB, lakini ndege hiyo haitakuwa tayari hadi mwaka 2013.
ANA inatazamia kuanza kutumia ndege ya kwanza aina ya 787 katika safari kutoka Tokyo kwenda Okayama-Hiroshima tarehe 11 Novemba.
Baadaye itaruisha ndege hiyo kimataifa kutoka Tokyo kwenda Frankfurt Ujerumani, mwezi Januari.
"Watu wengi wanasema kuwa ndege hii [787] itakuwa maarufu sana," amesema George Hamlin, rais wa taasisi ya washauri wa usafirishaji ya Hamlin.
Chanzo: bbc swahili

Kaburi la pamoja lagunduliwa Tripoli

Wafungwa wa Abu Salim
Wafungwa katika gereza la Abu Salim
Kaburi la pamoja la mamia ya watu lagunduliwa mjini Tripoli, Libya.
Kaburi la pamoja linaloaminika kuwa na miili 1,270 limegunduliwa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli baraza la mpito la nchi hiyo limesema.
Mabaki hayo yanadhaniwa kuwa ya wafungwa waliouwawa na maafisa wa usalama mwaka wa 1996 katika gereza la Abu Salim.
Uasi dhidi ya Kanali Muammar Gaddafi ulianza kama maandamano kutaka wakili aliyewakilisha familia za wafungwa wa Abu Salim aachiliwe huru.
Uchimbuaji wa kaburi hilo la pamoja unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Baraza la mpito la kitaifa (NTC) liligundua kaburi hilo la pamoja- jangwa lililotawanyika sehemu za mifupa katika uwanja wa gereza la Abu Salim- baada ya kuwahoji walinzi wa gereza hilo waliofanya kazi wakati wafungwa hao waliuwawa baada ya kuadamana dhidi ya hali yao ya maisha.
Baadhi ya sehemu za mifupa na nguo zilizochanika tayari zimepatikana.

'makombora na risasi'

Baadhi ya familia walizuru eneo hilo, miongoni mwao akiwa Sami Assadi, ambaye alipoteza kaka wawili katika tukio hilo.
Alielezwa kaka zake walikufa kutokana na sababu za kawaida miaka mitano iliyopita. Alieleza BBC alivyojihisi alipofika mahali ambapo kaka zake huenda walizikwa.
''Nina hisia tofauti kwa hakika. Sote tulikuwa na furaha kwa sababu mageuzi haya yamefanikiwa lakini, wakati ninaposimama hapa nawakumbuka kaka zangu na marafiki wangu wengi sana ambao wameuwawa, na sababu hasa, ni kwamba hawakumpenda Muammar Gaddafi.''
Mwandishi wa BBC Jonathan Head ambaye alifika katika eneo hilo anasema, hadi hivi majuzi ni habari chache sana ndizo zilijulikana kuhusu mauaji ya wafungwa hao.
Watu wachache walioshuhudia tukio hilo wamelezea kuwa wafungwa hao waliuwawa katika seli zao kwa makombora na kupigwa risasi baada ya kuandamana.
Maafisa katika serikali mpya wanasema watahitaji kufanya uchunguzi wa kisasa kusaidia kujua kilichofanyika katika eneo hilo.

Prof Wangari Maathai afariki dunia

Mtunukiwa wa tuzo ya Amani ya Nobel Prof Wangari Maathai ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 71.
Mwanaharakati huyo mashuhuri wa mazingira na haki za binadamu wa Kenya Profesa Wangari Maathai amefariki dunia mjini Nairobi usiku wa kuamkia , Jumatatu kutokana na maradhi ya saratani.
Prof Karanja Njoroge ambaye ni mkurugenzi wa Green Belt Movement, shirika ambalo Prof Maathai alilianzisha amethibitisha kifo hicho.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Prof Njoroge amesema wakati wa kifo chake Wangari alikuwa na wanafamilia na marafiki.
Marehemu ameacha watoto watatu, wawili wakiume na mmoja wa kike.
Profesa Wangari Maathai alipata tuzo la amani ya Nobel mwaka 2004, kufuatia juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.
Mbali ya kuwa Mwanaharakati wa Maswala ya Mazingira na haki za binadamu , Wangari Maathai pia alikuwa mwanasiasa shupavu. Amewahi kuhudumu kama Mbunge na Naibu waziri wa Mazingira nchini Kenya.
Prof Maathai pia katika uhai wake alipata tuzo mbalimbali za kimataifa kwa kutambua mchango wake.
Prof. Wangari Muta Maathai alianzisha vuguvugu la Green Belt mnamo mwaka 1977, ambapo alifanya kazi na wanawake kote nchini kuboresha maslahi yao na kuhifadhi mazingira.
Alikuwa mtetezi mashuhuri wa matumizi bora ya mali asili . Shughuli zake zilitambuliwa mara kwa mara kote duniani
Chanzo bbc swahili: