Monday, 26 September 2011


Shamba la Rais wa Burundi lachomwa moto

Watu wamechoma moto kwa makusudi shamba la mananasi linalomilikiwa na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, maafisa wamesema.
Moto huo umeharibu sehemu ya eneo la shamba hilo kwa upande wa Kusini Mashariki mwa eneo la Musongati, wamesema.
Rais Pierre Nkurunziza
Mwandishi wa BBC Prime Ndikumagenge aliyeko mjini Bujumbura, anasema kumekuwa na milipuko ya maguruneti na mashambulizi ya bunduki nchini Burundi tangu Jumapili.
Serikali inashutumu mashambulizi hayo kuwa yanatoka kwa majambazi, lakini watu wengi wana wasiwasi kuwa uasi huenda ukawa umerejea,
Amesema karibu watu 300,000 waliuawa nchini Burundi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika 2005.
Hali tete imejitokeza tena wakati wa uchaguzi mwaka jana huku wapinzani wakidai kuwa ulitawaliwa na kutishiwa pamoja na kukamatwa na udanganyifu.
Kiongozi wa zamani wa waasi Agathon Rwasa alijiondoa katika kinyang'angiro cha Urais na kuikimbia nchi.
Bw Nkurunziza alikuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo.
Mwandishi wa BBC anasema baada tu ya shamba la Rais Nkurunziza kushambuliwa mwalimu wa shule ambaye ni mwanachama wa chama tawala nchini humo alipigwa risasi na kufa eneo la karibu.
Anasema watu wawili pia wameuawa katika shambulio la guruneti kusini magharibi mwa Burundi na gari binafsi kuvamiwa kaskazini mwa nchi.
Hakuna kikundi chochote kulichokiri kuhusika na mashambulizi hayo.

No comments:

Post a Comment