Monday, 26 September 2011


Prof Wangari Maathai afariki dunia

Mtunukiwa wa tuzo ya Amani ya Nobel Prof Wangari Maathai ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 71.
Mwanaharakati huyo mashuhuri wa mazingira na haki za binadamu wa Kenya Profesa Wangari Maathai amefariki dunia mjini Nairobi usiku wa kuamkia , Jumatatu kutokana na maradhi ya saratani.
Prof Karanja Njoroge ambaye ni mkurugenzi wa Green Belt Movement, shirika ambalo Prof Maathai alilianzisha amethibitisha kifo hicho.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Prof Njoroge amesema wakati wa kifo chake Wangari alikuwa na wanafamilia na marafiki.
Marehemu ameacha watoto watatu, wawili wakiume na mmoja wa kike.
Profesa Wangari Maathai alipata tuzo la amani ya Nobel mwaka 2004, kufuatia juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.
Mbali ya kuwa Mwanaharakati wa Maswala ya Mazingira na haki za binadamu , Wangari Maathai pia alikuwa mwanasiasa shupavu. Amewahi kuhudumu kama Mbunge na Naibu waziri wa Mazingira nchini Kenya.
Prof Maathai pia katika uhai wake alipata tuzo mbalimbali za kimataifa kwa kutambua mchango wake.
Prof. Wangari Muta Maathai alianzisha vuguvugu la Green Belt mnamo mwaka 1977, ambapo alifanya kazi na wanawake kote nchini kuboresha maslahi yao na kuhifadhi mazingira.
Alikuwa mtetezi mashuhuri wa matumizi bora ya mali asili . Shughuli zake zilitambuliwa mara kwa mara kote duniani
Chanzo bbc swahili:

No comments:

Post a Comment