PATA HABARI MOTO MOTO, ZA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA HAPA, TUPE MAWAZO YAKO TUYAFANYIE KAZI, TUPE HABARI ZOZOTE ULIZO NAZO TUTAZIWEKA HAPA,KWA MWENYE PARTY AINA YOYOTE INAYOHUSIANA NA MAMBO YA MUSIC, TAFADHARI ONGEA NA PAPAYA KUPITIA NAMBA HII..07501 202029..YUPO MACHO 24/7 BEI MAELEWANO.

Wednesday, 21 September 2011

WAUZA SUKARI, WAVUNA WALICHOPANDA

UPUNGUFU wa sukari nchini unazidi kugonga vichwa vya wanasiasa na watendaji nchini, baada ya Jeshi la Polisi kuibuka na kuanza kusaka wafanyabiashara wanaotuhumiwa kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi.

Wakati Polisi wanapambana na upungufu huo, Waziri Mkuu amefichua siri nyingine, akisema kuna mbinu za kifisadi zilizoandaliwa ili kuhujumu vibali vya sukari inayotaka kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Serikali imeeleza nia yake ya kuagiza tani 120,000 za sukari kutoka nje ya nchi ili kufidia nakisi inayotokana na kuadimika kwa sukari nchini, hatua inayofanya bei ya bidhaa hiyo kuwa juu.

Akiwahutubia wakazi wa mji wa Mugumu wilayani Serengeti juzi usiku, Pinda alisema amepata taarifa za siri kwamba wapo wafanyabiashara waliojitokeza kuomba vibali vya kuagiza sukari kutoka nje, lakini hawana uwezo huo, bali wametumiwa na wenzao wakubwa ili baadaye wawauzie vibali hivyo.

Alisema baada ya kuligundua hilo amemuagiza Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe kuwafuatilia ili kuwachunguza wafanyabiashara wote walioomba vibali vya kuagiza sukari ili kujua wanaagiza sukari hiyo kutoka nchi gani, wataiuza lini na mahali watakapoiuza.

“Hatukutaka sukari iagizwe na wafanyabiashara wachache tukasema kila mfanyabiashara apewe kibali cha kuagiza tani 5,000 tu za sukari. Sasa kuna mtu kanivujishia siri kwamba wapo watu walioomba vibali hivyo, lakini hawana uwezo wa kuagiza kiasi hicho.

“Wanachokifanya wafanyabiashara hao ni kuchukua vibali vile na kwenda kwa wafanyabiashara wakubwa na kuwauzia ili wao ndio waagize sukari hiyo.

“Hatua hii itamfanya mfanyabiashara huyu mkubwa baada ya kuingiza sukari hiyo nchini kuiuza kwa bei ya juu ili kufidia ile pesa aliyonunulia kibali kutoka kwa yule mtu wa kati. Hili hatutalikubali,” alisema Pinda.

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limetangaza kuanza operesheni kwa kushirikiana na Bodi ya Sukari ya kudhibiti uvushaji wa sukari kwenda nje ya nchi.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu Pinda kulituhumu jeshi hilo kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kuipeleka nje ya nchi, hivyo kuchangia uhaba wake nchini.

Akitangaza uamuzi huo Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Robert Manumba, alisema operesheni hiyo iliyoanza juzi, imelenga kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.

Alisema mbali na operesheni hiyo katika maeneo yote ya mipaka ya nchi, pia wataendesha msako katika maghala yanayotumika kuhifadhia bidhaa hiyo kwa lengo la kujua kama kuna wafanyabiashara walioificha.

Kuhusu askari waliolalamikiwa na Pinda, Manumba alisema Polisi inaendelea kuzifanyia uchunguzi taarifa hizo na kuahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu wahusika watakaobainika kuhusika na matukio hayo.

Kwa upande wake, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imesema kuanzia sasa kila kiwanda cha sukari kinatakiwa kuwasilisha serikalini na katika Bodi ya Sukari, uzalishaji wake wa kila siku.

Aidha, wawasilishe taarifa za kila mnunuzi, jina la kampuni namba ya simu ya mkononi ya mwenye kampuni na kiasi alichouziwa kwa siku hiyo.

Waziri Profesa Jumanne Maghembe pia ameagiza wawasilishe namba za magari yaliyopakia sukari, mwenye gari, wilaya atakayosambaza sukari hiyo na tarehe itakayofika wilayani.

Katika taarifa yake kuhusu hali ya sukari nchini iliyosomwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Geoffrey Kirenga, Profesa Maghembe alisema makatibu tawala wa wilaya zote wanatakiwa kupeleka taarifa wizarani kila siku kuhusu sukari iliyoingia kwao.

“Mfanyabishara ye yote atakayekiuka utaratibu huo atafutiwa leseni yake mara moja na kuchukuliwa hatua za ziada kama itaona inafaa,” alisema Maghembe.

Alisema sukari ni adimu nchini kutokana na kushuka kwa uzalishaji katika nchi za Kenya, Uganda na Burundi kupanda bei na kuuzwa kati ya Sh 3,500 na 6,000 jambo lililosababisha wafanyabiashara wenye tamaa nchini kuisafirisha katika nchi hizo.

Alisema mahitaji ya sukari kwa kila mwaka ni takribani tani 384,000 za sukari inayotumika majumbani na tani 100,000 ya viwandani huku matarajio ya uzalishaji wa ndani mwaka huu ni tani 306,000.

No comments:

Post a Comment