Baadhi waupongeza kuwa mzuri
Uteuzi wa wabunge waendelea kupingwa
Uteuzi wa wabunge waendelea kupingwa
Wasomi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida, wametoa maoni yao kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya, huku baadhi wakisema kuwa ni mzuri, wengine wakipinga mbunge kuwa mkuu wa mkoa na wengine wakishangazwa na wale waliokosa ubunge kupewa nafasi hiyo.
Maoni hayo yametolewa na wadau hao kwa nyakati tofauti jana, ikiwa ni siku moja baada ya uteuzi wa wakuu hao wa mikoa uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, kutangazwa jana.
DK. BENSON BANA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema uteuzi wa wakuu wa mikoa uliofanywa na Rais Kikwete juzi, ni mzuri kwani walioteuliwa siyo wageni katika utumishi wa serikali.
Hata hivyo, alisema uteuzi huo una sura ya mpango mkakati wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa faida ya chama hicho.
Alisema mpango mkakati huo umedhihirika kutokana na uteuzi huo kulenga zaidi makada wa CCM.
Hata hivyo, alisema mbali na hayo, uteuzi huo unaonyesha wenye vyeo vya kijeshi wanazidi kupungua katika nafasi hizo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
DAVID KAFULILA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema Kikatiba, haoni umuhimu wa kuwapo kwa wakuu wa mikoa nchini, kwani kuwapo kwao kunafanya gharama kutumika katika mfumo ambao hauna tija.
Vilevile, alisema suala la mbunge kuwa mkuu wa mkoa nalo pia ni tatizo.
Alisema mkuu wa mkoa ni mhimili wa serikali wakati mbunge ni mhimili wa Bunge, hivyo kwa mtu mmoja kuwa na nyadhifa mbili kwa wakati mmoja, kunasababisha mgongano wa kimaslahi.
“Kwa sababu mbunge, ambaye ni mkuu wa mkoa anawezaje kuihoji serikali wakati yeye pia ni serikali? Suala hilo limekuwa likilalamikiwa muda mrefu, lakini CCM na serikali yake leo wanarudia makosa yale yale. Hapa kuna dharau na kutokujali,” alisema Kafulila.
Alisema suala hilo halina tofauti na waziri kuwa mbunge, kwani kunasababisha udhaifu wa kiutendaji.
Pia alisema tatizo lingine linaloonekana katika uteuzi wa wakuu wa mikoa, ni utamaduni uliozoeleka wa kuteua wanajeshi kushika nafasi hiyo, wakati masuala ya utawala hayahusiani na jeshi.
ANANILEA NKYA
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya, akitoa maoni yake kuhusiana na uteuzi huo wa wakuu wa mikoa, alionyesha kukerwa na hatua ya mtu mmoja kupewa kazi mbili kwa wakati mmoja.
Kutokana na hilo, alishauri Katiba mpya itakayotungwa, iainishe namna Watanzania watakavyoweza kupata viongozi, kama vile wakuu wa mikoa na wilaya.
Alisema jambo hilo liende sambamba na Katiba kuainisha chombo mahsusi kitakachokuwa na mamlaka ya kufanya uteuzi ikiwa ni pamoja na kuweka vigezo na sifa za watu wanaostahili kuteuliwa kuwa viongozi serikalini.
MOROGORO
Mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Omary Kunga, alisema uteuzi wa kuwapandisha wakuu wa wilaya ni sawa, lakini ameshangazwa na baadhi ya wale waliokosa ubunge kupewa nafasi hiyo.
“Kama walishindwa nafasi ya ubunge, ambako ni watu wachache, iweje leo waweze kuongoza mkoa ambao una idadi ya watu wengi?” alihoji Kunga.
Alisema kuna watu wengi, ambao wana uwezo wa kufanya kazi hizo, lakini wameachwa na kurudishwa viongozi hao, ambao tayari wananchi walishawakataa katika nafasi ya ubunge.
Richard Peter, ambaye ni mkazi wa Kilakala alihoji uteuzi wa mkuu wa mkoa wa Morogoro na kusema kutokana na ukubwa na umuhimu wake, alipaswa kuwekwa mtu mwenye uwezo.
“Wapo wakuu wa wilaya wenye uwezo katika mkoa huu wangepewa nafasi wao sio kutuletea huyu wa sasa,” alihoji.
Athuman Mwijuma, mkazi wa Uwanja cha Ndege, aliuponda uteuzi huo na kueleza kuwa umefanywa kwa kujuana na kuacha watu wenye uwezo wa kufanya kazi hizo.
MOSHI WAMTAKA GAMA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI
Wananchi wa mjini Moshi, wameupokea uteuzi wa wakuu hao wa mikoa kwa hisia tofauti, huku wengi wao wakimuomba mkuu wa mkoa mpya wa Kilimanjaro, kutatua migogoro ya ardhi inayoshika kasi pamoja na uonevu unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia.
Martin Ngowi, Joseph Charles na Tamia Mndeme, walisema wanamshukuru Rais Kikwete kwa kumteua Leonidas Gama kuwa mkuu wa mkoa huo, ambao umekaa kwa takriban miaka miwili bila mkuu wa mkoa.
Ngowi alisema hali hiyo ilisababisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali kukwama na kuufanya mkoa kuanza kurudi nyuma kimaendeleo.
Alisema kwa sasa kuna migogoro ya ardhi, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa utawala wa sheria na kumuomba mara atakapofika kuhakikisha anasimamia suala hilo ili kila mwananchi aweze kunufaika na raslimali zilizopo.
Mndeme alisema wana imani kwamba, kiongozi huyo atasikiliza kero mbalimbali za wananchi na kukabiliana nazo katika kuendeleza mkoa huo.
MBEYA WASHUKURU MWAKIPESILE KUSTAAFU, WAMPONDA KANDORO
BAADHI ya wakazi wa Jiji la Mbeya, wamepokea kwa hisia tofauti tukio la kustaafu kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, pamoja na ujio wa Mkuu mpya wa Mkoa huo, Abbas Kandoro.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti jijini hapa jana, baadhi ya wananchi hao wamedai kuwa kuondoka kwa Mwakipesile huenda kukawa kumehitimisha siasa za makundi, ukabila na ubabe wa kutoa maamuzi aliokuwa nao Mkuu huyo wa Mkoa.
Steven Jonas, ambaye ni mkazi wa Mbalizi, nje kidogo ya Jiji la Mbeya, alisema Mwakipesile alikuwa ni kiongozi anayefanya kazi kwa kuendekeza ukabila na siasa za makundi, hivyo kuondoka kwake ni nafuu kubwa kwa watu wanaopenda maendeleo ya Mbeya.
“Tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa, baadhi ya wabunge wa majimbo yaliyo ndani ya mkoa huu hawajawahi kuhudhuria vikao vya maendeleo kama vile kikao cha bodi ya barabara, kikao cha maendeleo ya mkoa (RCC) na kikao cha Kamati ya ulinzi ya mkoa, ambavyo mwenyekiti wake kisheria ni mkuu wa mkoa. Hii ni kwa sababu ya kiongozi huyo kupenda maamuzi ya kibabe na siasa za makundi,” alisema Jonas.
Mkazi mwingine wa Jijini Mbeya, George Chanda, alisema Mwakipesile hana analojivunia kwa miaka zaidi ya sita aliyokuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya kwa kuwa hakuwa na maamuzi yanayozingatia maslahi ya wana-Mbeya.
Alisema pamoja na uteuzi mpya alioufanya jana Rais Kikwete, mkoa wa Mbeya haujapata nafuu yoyote kwa kuwa mkuu wa mkoa anayeondoka alikuwa na upungufu mwingi na huyo anayekuja pia ana matatizo yake.
Alisema Mwakipesile alikuwa na tatizo la kukumbatia ukabila na maamuzi yasiyozingatia maslahi ya mkoa, hivyo kumfanya aondoke madarakani akiwa hana jambo kubwa alilowasaidia wakazi wa Mbeya.
Alisema pamoja na kujengwa kwa viwanda vichache mkoani Mbeya, Mwakipesile ameshindwa kabisa kuwasaidia wakazi wa Mbeya kupata ajira, badala yake wawekezaji hao wamekuwa wakiajiri hata wafagiaji kutoka mikoa mingine.
Akizungumzia ujio wa Kandoro, Chanda alisema ni kiongozi anayependa kuzungumza na kutoa maagizo mengi bila kuwapo na ufuatiliaji wa karibu.
“Kandoro sio mfuatiliaji wa maagizo yake na ndio sababu aliboronga alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na hivi sasa anaondoka Mwanza akiacha mgogoro mkubwa unaosababisha umwagikaji wa damu katika Halmashauri ya Geita, mkoani Mwanza, kutokana na kutokuwa mfuatiliaji wa maagizo yake. Naamini Mkoa wa Mbeya utamsumbua na huenda akajimaliza mwenyewe,” alisema Chanda.
Athanas Wakisole, mkazi wa Mwanjelwa, alisema kuondoka kwa Mwakipesile ni pigo kwa mkoa, kwa kuwa kiongozi huyo alikuwa mtu mwenye msimamo thabiti na anayechukia watendaji wavivu.
IRINGA WASHANGAZWA WABUNGE KUWA WAKUU WA MIKOA
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Iringa, wamepokea kwa hisia tofauti uteuzi wa wakuu wapya wa mikoa 15, huku wengi wao wakidai kushangazwa na hatua ya Rais Kikwete kuendelea kuteua wabunge kuwa wakuu wa mikoa.
Mmoja wa wabunge hao, ni Mhandisi Stella Manyanya (Mbunge wa Viti maalum-Ruvuma), ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Walisema hawakutarajia kama uteuzi wa safari hii, wakuu wa mikoa wenye kofia mbili hasa wabunge wangechomoza katika nafasi hizo kutokana na tatizo la kiufundi alilolifanya Rais katika miaka mitano iliyopita.
Saimon Sanga, mkazi wa Kitwiru, Manispaa ya Iringa, alisema: “Jamani Mheshimiwa Rais ni vyema akaliangalia upya jambo hili la kuwateua watu, ambao tayari walikuwa na kofia ya ubunge. Kwa kweli kuwajazia watu vyeo, wakati wako wenye uwezo wa aina hiyo, haileti maana kwa sababu mwaka 2010, waliokuwa wabunge na wakati huo huo wakuu wa mikoa, waliiacha mikoa yao wazi bila ya kuwa na kiongozi na kukimbilia kugombea ubunge na hatimaye kuangushwa.”
Cresensia Mwalongo, alisema uteuzi alioufanya Rais Kikwete, umelenga kuziba mapengo yaliyokuwa wazi kwa muda mrefu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Katika uteuzi huo, Dk.Christine Ishengoma, ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa akitokea mkoa wa Ruvuma. Alikaimu nafasi hiyo mkoani hapa kwa zaidi ya miezi mitatu.
ARUSHA WADAI UTEUZI UMEFANYWA KISIASA
Baadhi ya wananchi mkoani Arusha, wamesema kustaafishwa kwa mkuu wa mkoa wa Arusha na kupelekewa mkuu wa mkoa mpya, Magesa Mulongo, kwamba kunahusiana na siasa.
Mkazi wa Arusha, eneo la Kwa Mbauda, Veronica John, alisema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Isidori Shirima, alikuwa kiongozi mwenye kujali utu na alikuwa anasikiliza matatizo ya watu, lakini anadhani kuhamishwa kwake ni kwa sababu za kisiasa.
“Mimi nadhani huyu ameondolewa kwa sababu ameachia jimbo hili likaenda upinzani na si vinginevyo. Lakini jimbo lingekwenda CCM asingetolewa wala kustaafishwa, ila siyo suala zuri,” alisema Veronica.
Alisema Shirima alikuwa Mkuu wa Mkoa ambaye ni tofauti na wakuu wa mikoa mingine, hivyo aliposikia katika taarifa ya habari alistuka na anahofia mkuu mpya anayekuja atakuwaje.
Musa Hassan, mkazi wa Kimandolu, alisema anaona vizuri serikali kufanya mabadiliko kwa sababu Shirima alikuwa amezeeka, kiasi kwamba, baadhi ya mambo yalikuwa hayaendi.
Alisema kitu kikubwa wanasubiri kuona utendaji wa kazi wa mkuu mpya, lakini kama nye siyo mchapakazi atajulikana siku chache kwa sababu Arusha ni mkoa wa pekee, ambao unahitaji mkuu wa mkoa mchapakazi na siyo mtu mvivu au legelege.
“Hapa ni eneo la vitu vingi.Ni mji ulio bize wakati wote kibiashara na hata kikazi. Hivyo, ni vema mkuu mpya ajaye awe mbunifu na kupanga mji katika mpangilio wa miundombinu mizuri tofauti na sasa,” alisema Juma.
Juma alisema mkoa huo utabadilika tu iwapo utapata mkuu wa mkoa mbunifu na hivyo miundombinu yake itabadilika na kuwa tofauti na ya sasa.
TANGA WAMLILIA MEJA JENERALI KALEMBO
Baadhi ya wananchi wa jijini Tanga, wameeleza hisia zao kuhusiana na uteuzi mpya wa wakuu wa mikoa, wakidai bado walihitaji msaada wa mkuu wa mkoa wa aliyestaafu, Meja Jenerali Said Kalembo, kutokana na tabia yake ya kuweka mbele maslahi ya wananchi.
Walisema Kalembo alikuwa ni kiongozi mchapa kazi na aliyeheshimu taratibu za utumishi wa umma kwa kutimiza makusudi yaliyomuweka madarakani.
“Kalembo kusema kweli mwanzo sisi wanatanga tulimwogopa tukawa tunamwona ni mkali na nini. Lakini baada ya kujua dhamira yake kwa maslahi ya wananchi na maendeleo ya Tanga kweli tulimpenda kwani aliwapa gwaride wafanyakazi na walilazimika kutimiza wajibu wao. Hakukuwa na longolongo za kiutendaji kwenye ofisi za serikali,” alisema Rajabu Juma, mkazi wa jijini Tanga.
Walisema kiongozi huyo alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa shughuli za maendeleo ya wananchi hazitekelezwi kisiasa hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kusukuma gurudumu la maendeleo la mkoa wa Tanga.
“Kalembo tutamkumbuka kama kiongozi asiye na upendeleo, mtetezi wa mali za wananchi na kiongozi mwenye msimamo na asiyekubali kuyumbishwa. Alifanya kazi na kuweka pembeni itikadi za chama. Hakusita kumwajibisha mtendaji yeyote aliyezembea kazini. Kwa hilo tutamsifu siku zote,” alisema Judith Mwaimu.
Hata hivyo, walisema wanaamini Mkuu wa Mkoa, Chiku Galawa, atafuata nyayo zake kama alivyokuwa Kalembo baada ya kukabidhiwa mkoa huo na Mohamed Abdul Aziz.
DODOMA WAMKUMBUKA MSEKELA
Wakazi kadha wa Manispaa ya Dodoma walisema kuwa uteuzi huo kwa kiasi unaweza kuleta mabadiliko kwa kiasi fulani.
Mmoja wa wakazi hao, Daniel Msangya, kuwa Mkuu wa mkoa huo, Dk. James Msekela, alikuwa ni mtendaji mzuri na hakuwa msemaji.
“Msekela alikuwa ni mtendaji na mtaalamu, lakini hakuwa msemaji sana ndio maana hata waandishi wengi walikuwa wanasema katika mikutano yake hawapati cha kuandika,” alisema.
Alisema kuwa mkuu mpya wa mkoa huo, Rehema Nchimbi, naye pia ni mtaalamu, lakini ni msemaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilayani Chamwino, Amani Msanga, alisema Msekela alikuwa ni mchapakazi na ni mfuatailiaji katika mambo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment