AU yaitambua serikali ya mpito ya Libya
Umoja wa Afrika (AU) umewatambua viongozi wa mpito wa Libya, baraza la mpito la taifa (NTC) ndio serikali ya Libya.
Taarifa hiyo imetolewa huku rais wa Marekani Barack Obama akisema balozi wake alikuwa akielekea mjini Tripoli kufungua upya ubalozi wake.
Baada ya wiki kadhaa ya kukataa kutoa ahadi yoyote, umoja wa Afrika sasa unasema Baraza la taifa la mpito ndio linalowakilisha wananchi wa Libya.
Hadi sasa umoja huo umekuwa ukisema serikali mpya ya Libya inapaswa kujumuisha makundi yote.
Umoja wa Afrika pia ulishikilia msimamo wake wa kutowatambua watu walioshikilia madaraka kwa nguvu.
Katika taarifa iliyotolewa na umoja huo wa Afrika kando na mkutano wa baraza kuu la umoja wa mataifa mjini New York ;umesema umehakikishiwa kwamba NTC imeazimia kuendelea na mshikamano wake na bara la Afrika.
Pia walitilia mkazo umoja wa kitaifa na kuwalinda wafanyakazi wa kigeni nchini Libya wakiwemo wahamiaji kutoka nchi za Afrika.
Taarifa ya AU pia imesema inamatumaini makubwa ya kuzaliwa taifa jipa la kidemokrasia la Libya.
Wakati huo huo kiongozi wa Libya aliyeondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi ametoa ujumbe mwingine uliorekodiwa, wakati huu akiwaonya wapinzani wake kuwa ulinzi wanaopata kutoka majeshi ya NATO hautadumu daima.
Katika ujumbe huo uliotangazwa katika televisheni moja nchini Syria, Kanali Gaddafi anasema mfumo wa utawala alioujenga kwa zaidi ya miaka arobaini iliyopita ulijikita katika misingi ya matakwa ya wananchi na hauwezi kung'olewa.
No comments:
Post a Comment