NI Liberata Mulamula, Balozi na mtoto wa Mwalimu Novati Rutageruka (Kada) aliyewahi kuwa
Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, miaka mingi iliyopita.
Ni mama msikivu na mcheshi anayetoka katika familia ya wasomi sita waliolelewa katika mazingira ya uhuru uliowafanya wawe wepesi kuelewa mambo yanavyobadilika kila kukicha kwenye dunia hii yenye mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia.
Ana kimo cha kati na ngozi halisi ya Mwafrika isiyo na madoido yoyote ya dukani. Kwa kizungu, anaweza kuitwa Natural African Woman. Unapozungumza naye utagundua kuwa ni mwanamke msikivu na mdadisi kutokana na shauku yake ya kuuliza pindi anapoona umuhimu wa kufanya hivyo.
Umakini alionao pia humsukuma kutaka kujua endapo anayezungumza naye ameelewa. Maisha katika familia alipozaliwa Kwa kuwa hupenda kuzungumza ukweli, Balozi Mulamula
hakuhofu kueleza bayana kuwa anatoka katika familia ya wazazi wasomi waliojibidisha katika
kazi, kiasi cha kuepuka umasikini.
Anasema,“Ni jambo jema la kumshukuru Mungu kwa kuwa wazazi wangu walikwenda shule
na kutumia elimu waliyoipata kuhangaikia maisha bora. Hawakubweteka.Wamekuwa
wachakarikaji na kuniwezesha mimi na wenzangu kuishi maisha bora yenye furaha.”
Anasema kuwa baba na mama yake walihakikisha familia hiyo inajenga utamaduni wa kupenda
elimu na kujisomea, kwa kuwa walifahamu umuhimu wa nyenzo hizo katika kuleta maisha bora.
“Si hilo tu, wazazi wetu na hasa baba yangu aliamini sana katika elimu, kujiamini na
mazungumzo, hivyo alitaka wanafamilia tujijenge katika misingi hiyo, ndio maana ukisikiliza
historia yangu utagundua kuwa imetokana na maandalizi ya wazazi. Sikuamka nikawa nilivyo,
walinitengeneza nikawa mimi unayenihoji sasa,”anaeleza.
Kwa maelezo yake, uwezo wa usuluhishi aliokuwa nao haukuja tu kama upepo bali ulitengenezwa na wazazi wake waliogundua kipaji hicho ndani yake, akiwa na umri wa miaka sita. Waliishi na wazazi wao kama marafiki waliokataa nidhamu ya woga.
“Unajua tumezaliwa sita katika familia yetu na mimi nina pacha wangu anayefanya kazi UNDP
(Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa). Kati yetu, wanne ni wanawake na wawili ni wanaume.
Malezi yetu yalikuwa ya uhuru usio na madhara kwa sababu wazazi walituruhusu kufanya
mambo waliyoamini yangetupa furaha huku wakifuatilia mienendo yetu… “…Walifuatilia kila tulichofanya kwa sababu ya ukaribu wao kwetu na kugundua uwezo na udhaifu wa kila mmoja wetu.
Njia hiyo ndio iliyoibua uwezo wangu katika usuluhishi ambao hata hivyo, waliuendeleza kwa njia mbalimbali na kuniwezesha kujiamini na hata kuweza kutekeleza jukumu la Maziwa Makuu nililokabidhiwa miaka mitano iliyopita.
Niliandaliwa mapema, namshukuru Mungu nimekamilisha kazi vizuri bila kuwaangusha Watanzania,” Balozi anasema na kuongeza; “Baba aligundua sikuwa mchangamfu na mwenye nguvu kama pacha wangu na ndugu wengine, hivyo alitumia ujanja kunilinda nisionewe pale ilipolazimu.
Pamoja na mama, walilea uwezo wangu wa kupatanisha wenzangu kwa kuwa waliniona
nikijaribu kufanya hivyo ulipotokea msuguano,” anasimulia. Anasema baba yake ndiye
aliyegundua uwezo huo wa kusuluhisha kutokana na umahiri aliokuwa nao (Balozi) katika kuhoji juu ya mambo, mfano sababu za mmoja kumpiga mwingine na kupendekeza suluhisho.
“Kwanza mimi nilidhani ningekuwa mwanahabari kutokana na udadisi wangu lakini wazazi
waligundua nilikuwa na uwezo zaidi wa kusuluhisha ndio maana wakanichagua kuwa mpatanishi wa pale nyumbani wakati wenzangu wakiwa wamegawiwa majukumu mengine tofauti kulingana na uwezo wao. Hawakugawa kazi kwa kuzingatia jinsi kwa kuwa walifahamu kumpa mtu kazi anayoiweza na kuipenda ndio kumwezesha aifanikishe.”
Uhuru wa ‘kujirusha’ na kufurahi Anasema wazazi wao hawakuwalea ‘kifungwa’ kwa
sababu waliwaamini. Waliwapenda na kuhakikisha kuwa wamezungumza nao kuwaeleza juu ya mambo mazuri na mabaya, ili wafanye uchaguzi wa lipi la kufuata.
“Naweza nisieleweke katika hili lakini napenda kuwaambia wazazi kuwa kumchunga sana mtoto na kumnyima uhuru wa kuchanganyika na wenzake ni kumharibu. Kumzuia mtoto kufurahi ni kumjengea woga utakaompotezea uwezo wa kujiamini hata atakapokuwa na familia yake binafsi baadaye…”
“Nilijirusha sana enzi zangu ingawa nilifanya hivyo kwa adabu. Hisabati ‘ilinigonga’ sana darasani lakini sikuacha kwenda disko usiku kufurahi na wenzangu,”anasema na kuweka
wazi kuwa wazazi wao ndio waliokuwa wakiwapeleka kwenye kumbi za disko na kuwafuata pindi muziki unapokwisha kwa ajili ya kuwarudisha nyumbani.
“Hata kuleta marafiki nyumbani sisi tuliruhusiwa na hiyo ilitufanya tusifanye mambo yetu kwa
kificho. Baba na Mama walipenda mazungumzo nasi, hivyo tuliishi kama marafiki. Aliyekuja na rafiki yake wa kike au wa kiume aliweza kumtambulisha kwa wazazi na kuwa naye karibu.
Sikusikia au kuona mmoja wetu akichapwa kwa hilo. Walituamini ndio maana hatukupotoka kutenda ndivyo sivyo hadi kila mmoja alipoondoka nyumbani na baraka zote. Wakuolewa aliolewa na wakuoa alioa kwa heshima,”anaeleza.
Maisha ya kushurutishana Balozi anasema atawasifu wazazi wake siku zote kwa sababu
hawakuwa na mfumo jike wala dume. Katika maisha ya utoto, ujana wao hadi kifo cha wazazi
wao, hawakuwahi kushuhudia mmoja wao akimpiga mwingine au kumtolea lugha chafu kwa jambo lolote lile.
“Labda kama walifanya hivyo chumbani kwao, mimi wala ndugu zangu hatukuwahi kuona hayo yakiwatokea wazazi wetu ndio maana habari ya mfumo jike na dume inakuwa kichefuchefu kwangu.
Sitaki wala sitamani mtu aumizwe na mifumo hiyo isiyo na utu, Mungu asaidie mikakati tuliyoiandaa katika Maziwa Makuu ifanikiwe. Inasimamia haki kwa kila jinsi,” anasema.
Mama huyo wa watoto wawili anaendelea kueleza kuwa familia yao haikuwa na utaratibu wala kanuni ya kulazimishana kufanya jambo kwa kuwa aliyetakiwa kutekeleza shughuli fulani alikuwa na nafasi ya kujitetea na kusikilizwa.
Anasema, “Si baba wala mama, kati yao hakuna aliyekuwa na tabia ya ku-command (kulazimisha jambo), walitutuma lakini walikuwa tayari kusikiliza utetezi kwa aliyeona dalili za kushindwa kutekeleza wajibu huo. Eti ni lazima ufanye hiki au kile!, hapana.
Kwetu hakukuwa na utaratibu huo na ni vema mtu akafanya kitu anachomudu kulingana na uwezo wake vinginevyo ataboronga, wazazi walipenda tujaribu na si tuharibu”. Nafasi ya mumewe katika mafanikio yake “Sijaona mwingine kama Profesa George Mulamula.
Huyu ndiye mume wangu aliyeniwezesha kufanikisha majukumu yangu katika Sekretarieti ya Ukanda wa Maziwa Makuu. Nampenda sana na Mungu amzidishie busara,” anasema Mulamula.
Anafafanua zaidi kuwa, pengine majukumu yake kama Katibu Mtendaji katika Sekretarieti hiyo yangemshinda endapo mumewe angeamua ‘kumkomalia’ atekeleze majukumu yote anayompasa mke kwa wakati unaofaa kama vile kuhudumia watoto na kuangalia familia kwa karibu sana.
“Nafurahi amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ninafanikiwa. Hata nilichokuwa nimesahau kukifanyia kazi kama binadamu wa kawaida alinikumbusha bila kuchoka. Alihakikisha mawasiliano yangu kwa njia ya kompyuta yapo sawa wakati wote na ilipotokea hitilafu alikuwa ni kimbilio langu. Siunajua ni Profesa wa IT yule!!
Mungu amzidishie busara maana angeweza kunikwamisha pia kama angetaka,”anasisitiza.
Anasema pia kuwa mume wake alikuwa mlezi mkuu wa watoto wake wakati wote alipokuwa
Burundi akitekeleza majukumu yake kimataifa.
Kadhalika ndiye aliyekuwa akijituma zaidi kubadilisha watoto pampas (nepi za kisasa) nyakati za usiku wakati yeye (Balozi) akiwa amelala fofofo kwa uchovu kutokana na uzazi. “Hasa nilipojifungua mtoto wangu wa pili, George alikuwa ndiye anayeamka usiku mtoto anapolia na kumbadilisha pampas.
Ndiye aliyekuwa akimpa maziwa na kuniandalia kifungua kinywa kabla hata msichana wa
kazi hajaamka. Ni kujitoa kwa pekee huko kwa sababu hakukuishia hapo tu bali hata wakati nimeripoti kazini. Alihakikisha kazi ndogondogo hazinicheleweshi. Alinisaidia kuzifanya,”
anasema.
Balozi Mulamula aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu mwaka
2006. Alitumia nafasi hiyo kushawishi taasisi hiyo kuimarisha amani utulivu na maendeleo
na kutumia mazungumzo ya amani kama njia ya usuluhishi na kuimarisha amani katika nchi hizo.
Harakati zake za kujiunga na kundi la wanadiplomasia zilianza mwaka 1981 baada ya kujiunga na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Umahiri wake katika masuala
ya kimataifa ulimuwezesha kuchaguliwa kuwa Balozi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa nafasi aliyoshikilia mwaka 1985 hadi 1992 na mwaka 2002-2003.
Pia alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada kati ya mwaka 1999-2002 na mwaka 2003 hadi
2006 Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
No comments:
Post a Comment