Saturday, 10 March 2012

NAIBU WAZIRI AIBIWA MAMILIONI HOTELINI, MOROGORO


WATU wasiofahamika wamemwibia Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, katika chumba alichopanga kwenye hoteli ya kitalii ya Nashera mjini hapa.

Wizi huo ulifanyika usiku wa kuamkia jana ambapo chumba kilivunjwa na kuibwa mabegi matatu yenye kompyuta mbili ndogo, simu tatu za mkononi na vitu vingine mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya jumla ya kati ya Sh milioni 13 na 15.

Pia kwenye mabegi hayo, zilikuwamo fedha taslimu Sh milioni 1.5 na dola taslimu 4,000 za Marekani na pasipoti yake. Polisi inashikilia walinzi watatu wa hoteli hiyo kwa ajili ya mahojiano zaidi ili kubaini wezi hao.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa, Hamis Selemani jana alithibitisha kutokea kwa wizi huo ambao ulifanyika saa 10.45 alfajiri, katika chumba namba 125 alimokuwa amepanga Naibu Waziri.

Akizungumzia tukio hilo, Selemani alisema dirisha la chumba hicho lilivunjwa na wezi kuingia na kuiba mabegi hayo zikiweamo kompyuta hizo aina ya Dell zenye thamani ya jumla ya Sh milioni 5.5.

Kwa mujibu wa Selemani, Naibu Waziri aligundua kuvunjwa kwa dirisha na kuibiwa vitu hivyo, baada ya kuingia ndani akitokea sebuleni alikokuwa amejipumzisha awali baada ya kurejea kutoka kwenye shughuli zake.


“Naibu Waziri baada ya kuingia ndani kutoka sebuleni, aligundua kuvunjwa kwa dirisha na alibaini kuwa mabegi matatu yaliyokuwa na vitu yameibwa,” alisema Mkuu huyo wa Upelelezi.

Alivitaja vitu vingine vilivyokuwa ndani ya mabegi hayo kwamba ni vinasa sauti vitatu vyenye thamani ya Sh milioni moja, simu tatu aina tofauti zenye thamani ya jumla ya Sh milioni 1.3, pete mbili za fedha zenye thamani ya jumla ya Sh milioni 2.5 kadi za benki ‘ATM’ na kofia aina ya baghashia yenye thamani ya Sh 50,000.

Kwa mujibu wa Selemani, wezi hao mbali na kuiba mabegi hayo, waliacha bastola moja na bunduki chumbani humo wakati walipovunja dirisha.

“Upelelezi unaendelea, lakini baada ya kutokea wizi huu na sisi kuanza kufanya kazi yetu, mchana wa leo (jana) askari walipata begi moja lililotelekezwa mashambani mbali na hoteli na tumemwomba Naibu Waziri aende kituoni kulitambua na vilivyomo,” alisema.

Kwa upande wake, Malima, alikiri kuibiwa na kusema aliporudi kutoka kwenye mkutano na wadau wa sekta ya madini, saa 4.30 usiku, alifika hotelini hapo na kwenda kujipumzisha sebuleni na aliingia ndani saa saba usiku na kuweka simu, silaha na simu mbili na kujiandaa kwenda kuoga.

Alisema wakati anajiandaa kuswali, alisikia kwenye televisheni taarifa ya habari ikizungumzia wananchi wa Urusi kususia uchaguzi na wakati huo kila kitu akiwa amekiacha chumbani anamolala.

“Niliangalia taarifa ya habari nikaona ni vema nikaandika baadhi ya maazimio niliyoyatoa kwenye mkutano wangu na wadau wa sekta ya madini,” alisema Naibu Waziri na kuongeza:

“Nikiwa pale nilipitiwa na usingizi, nikiwa naangalia taarifa ya habari na nikashituka saa 10.45 alfajiri … na kawaida muda huo usingizi huniruka kwa sababu ya kuamka kwenda kuswali… nilishituka nikajiuliza simu zangu ziliko na kubaini kuwa niliziacha chumbani,” alisema Naibu Waziri.

“Nilipoingia chumbani sikuziona simu zangu na hata barazani hazikuwapo …huku na huko mabegi nayo sikuyaona, moja la laptops na lingine la majalada,” alisema. Alisema chumbani alibaini alama za nyayo za matope na alipoangalia kitandani akaona bastola na bunduki yake.

“Huyu mtu amekuja kuiba, lakini silaha ameniachia …kwa hivyo nimeibiwa mabegi yangu matatu, moja lina kompyuta, mawili yana nyaraka …nilitoka kwenda kuwaarifu watu wa Mapokezi kuwa nimeibiwa na aliarifiwa Meneja anayeishi hotelini hapo,” alisema.

Hata hivyo alisema, alimwomba simu ili awafahamishe wasaidizi wake juu ya tukio hilo, na baadaye waliarifiwa polisi na kufika hotelini hapo na kufanya uchunguzi na kuchukua maelezo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, Katibu Tawala wa Mkoa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama walishuhudia jambo hilo na kutoa pole wakati juhudi za uchunguzi ikiachiwa Polisi.

“Wameiba vitu vya thamani, laptops mbili, simu, pia pete mbili hizi zina thamani, moja nimeachiwa na marehemu baba yangu, hiyo kwangu ina thamani sana …haina thamani ya fedha ila na mimi nikiondoka duniani ni urithi wa familia… nyingine ni ya mke wangu,” alisema Naibu Waziri.

Meneja wa Hoteli, Eustus Mtua, alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea na limewasikitisha na wanaiachia Polisi ifanye uchunguzi wake ili kubaini wahalifu hao.
 
   
 
Jumla Maoni (4)
   
Maoni pole muheshima nina hakika walotenda kitendo hiko mungu atawaazibu.
   
Maoni Nampa pole sana naibu waziri kwa tukio hilo.kumuibia kiongozi nyaraka zake na vitendea kazi ni kujirudisha nyuma sisi wenyewe kwani yalioko ndani ya vitendea kazi hivyo ni kwa manufaa ya watanzania wote.Jeshi la polisi wahakikishe waaliofanya Wizi huo wanawatia mboroni haraka iwezekanavyo
   
Maoni Pole sana Mh.Naibu Waziri,watu wanaibiwa sana mahotelini ila wewe kwa sababu ya wadhifa ulio nao ndiyo vyombo vya habari vimetangaza.Bora umeona hali halisi ilivyo huku mitaani.Polisi fanyeni kazi yenu hao ni vijana tu wa vijiweni,wavuta unga,wahuni, wakishirikiana na walinzi wa hoteli.Yangekuwa majambazi yale sugu yasingeacha hivyo 'vitendea kazi' viwili
   
Maoni Pole sana Mheshimiwa kwa kuibiwa. Vyombo vinavyohusika ni wakati wao kulishughulikia hili kikamilifu na pia ni vyema Mawaziri walindwe vyema maana kuibiwa kwa nyaraka si kitu kidogo na huenda kukaigharimu nchi. Nawaomba Polisi walichukue hili kwa uzito mkubwa!

No comments:

Post a Comment