Sunday, 8 January 2012

WAHUJUMU UCHUMI WAKIONA CHA MOTO!!

VIONGOZI wanne wa Serikali ya kijiji cha Mkwakwani kilichopo Kata ya Mnyuzi wilayani Korogwe wameswekwa rumande kwa kuwadanganya wananchi kwamba wametumwa na Mkuu wa mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa wakate miti saba aina ya mivule kutoka kwenye Pori la Akiba la Manta ili kupata mbao za kupaulia jengo la Zahanati na vyumba vya madarasa. 

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkunguni, Festo Nyika, Katibu wa Kamati ya 
Ulinzi na Usalama katika kijiji cha Mkwakwani, Joseph Kimako, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Manyirizi Method na Mlinzi wa Msitu (pori) wa Manta, Ayubu Nyika. 

Kukamatwa kwa viongozi hao waandamizi katika serikali ya kijiji hicho kunafuatia agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa mara baada ya kufanya ziara ya kushitukiza kijiji hapo. 

Taarifa zinasema viongozi wa serikali ya kijiji hicho walidai kwamba wametumwa wakate 
miti hiyo ambayo baada ya kuipasua walipata mbao zaidi ya 300 ambazo walizisafisha na 
kutelekeza 40 kijijini hapo. 

“Ziara yangu ya leo hapa kijijini ni mahsusi kwa ajili ya viongozi wenu waliowadanganya kuwa 
nimewatuma mimi pamoja na mkuu wa Wilaya, Erasto Sima waje kuvuna miti ya mbao hapo 
msituni, taarifa hizo si za kweli na hao watu ni waongo, siwafahamu na sijawahi kuwatuma kwenu. 

“Kutokana na udanganyifu na uhalifu uliofanywa na viongozi wenu hao nataka kamati ya ulinzi 
na usalama ya wilaya ihakikishe inawasaka hadi kuwakamata na kuwaweka chini ya ulinzi tena 
ndani ya saa 48 kuanzia sasa hivi (jana) ili hatua nyingine za kinidhamu na kisheria ziweze 
kuchukuliwa dhidi yao”, aliagiza Gallawa. Walikamatwa baadaye na kuswekwa rumande.

No comments:

Post a Comment