INGAWA Pili sio maarufu katika ulimwengu wa sanaa, umahiri wake katika michezo ya mnyumbuliko wa mwili unampadisha chati katika sanaa za majukwaani zenye asili ya Kihindi.
Hivi karibu Pili alikuwa kivutio kikubwa pale alipotokeza jukwaani katika kituo cha Utamaduni wa India akiwa miongoni mwa wasanii wa Kikundi cha Sanaa cha Jumuiya ya Wahindi Dar es Salaam (Banga Sangho) kuadhimisha miaka 150 ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwanafalsafa Rabindranath Tagore.
Pili ambaye alikuwa amevalia mavazi ya Kihindi alicheza kwa umahiri mkubwa wakati wa
onesho lililoambatana na wimbo wa Rabindra Sangeet. Umahiri wake uliwafanya watazamaji
waamini kuwa alikuwa mtu mweusi mwenye asili ya Asia.
Hata hivyo baada ya onesho hilo kiongozi wa kikundi hicho alimtambulisha pili kuwa ni
msanii wa Kitanzania na alialikwa kwenye onyesho hilo ili kuonesha jinsi mwanafalsafa Togore
alivyotabiri juu ya maendeleo na changamoto zinazowakabili Waafrika.
Pili alitumia fursa hiyo kuonesha kipaji chake katika kucheza ngoma na kuimba nyimbo zenye
mahadhi ya Kihindi. Pili ambaye ni msanii katika kundi la Sanaa la Lumumba anasema yupo tayari kujifunza zaidi kuhusu sanaa za maonesho ya jukwaani na utamaduni wa watu wa Asia kwa lengo la kuwafundisha vijana wa Kitanzania wenye shauku ya kucheza ngoma za Kihindi.
“Lengo langu ni kuwa mwalimu wa sanaa za majukwaani kwa kuwafundisha vijana wa
Tanzania ngoma na nyimbo za Kihindi… hii itasaidia kuimarisha uhusiano wa Kiutamaduni kati ya India na Tanzania. Pia itakuwa sehemu ya kupanua soko la ajira katika fani ya sanaa,” anasema Pili.
Anafafanua kuwa sanaa za maonesho ya jukwaani ni miongoni mwa fursa zinazowapatia
wasanii kipato hivyo maonesho na muziki wenye hadhi ya Asia unaweza kuwavutia watu wengi
zaidi.
Ingawa kuna dhana kuwa watu wenye asili ya Asia hawapendi kuchanganyika na Watanzania wenye kipato cha chini, Pili anasema alifuatwa na kiongozi wa kikundi cha sanaa cha Jumuiya ya Wahindi wanaoishi Dar es Salaam na kumuomba ashiriki katika tamasha hilo la kumuenzi Tagore ambalo lilifanyika sanjari na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.
“Sikupenda kupoteza nafasi hiyo hivyo nilikubali ombi hilo na kwenda nyumbani kwao.
“Ingawa nilifanya mazoezi kwa muda mfupi tuliweza kucheza kwa ustadi mkubwa na mwalimu mwenye asili ya Asia anayeitwa Buri Buri ambaye alitufundisha kwa siku tatu kabla ya kujiunga na kundi la sanaa la ….kufanya mazoezi ya pamoja,” anaeleza.
Nyota ya pili katika sanaa ya maonesho ya jukwaani ilianza kuonekana angali mtoto. Alijiunga
na kundi la sanaa mara baada ya kujiunga na Shule ya Msingi Nzasa iliyoko Mbagala, Dar es
Salaam ambapo alishiriki kuimba kwaya ya kucheza ngoma za asili katika kundi la shule.
Baada ya kubaini kuwa shule yake haimpi fursa ya kutosha kuendeleza kipaji chake, aliomba
kuhamia Shule ya Msingi ya Lumumba ambapo alipokelewa bila ya matatizo.
“Awali nilikuwa naimba na kucheza ngoma za asili, lakini nilipohamia Lumumba nilipata fursa za kuongeza ujuzi kwa kujifunza kupiga marimba, gita (solo) na ala zingine za muziki. Pia nilijifunza kucheza dansi,” anasema.
Anasema mafanikio aliyofikia katika sanaa yanatokana na juhudi zake pasipo kuungwa mkono na wanafamilia kwa kuwa wakati yeye alikuwa anaweka mikakati ya kuingia kwenye masuala
ya urembo, familia yake ilitaka awe askari wa Magereza.
“ Familia ilikutana niwe askari wa Magereza, mimi nilikuwa na malengo mengine tofauti hivyo
nilipata wakati mgumu pale nilipoeleza kuwa lengo langu la kujikita katika kwenye masuala
ya sanaa,” anaeleza.
Hakuwa tayari kujiunga na Jeshi la Magereza kwa sababu alikuwa ameshaonja matunda
yanayotokana na kazi ya sanaa ya maonesho ya jukwaani. Wakati akiwa wanafunzi wa shule ya
msingi alikuwa akipata Sh 20,000 hadi 30,000 kwa mwezi kutokana na ushiriki wake katika kazi za sanaa.
Kila alipopata fedha alimpelekea mama yake na kuamini zingeweza kumshawishi mama yake ili amuunge mkono katika mikakati yake ya kujiendeleza katika fani ya sanaa.
Hata hivyo mambo yalikuwa tofauti, kwa kuwa mama yake hakuwa tayari kumuunga mkono hali ambayo ilisababisha kukabiliana na wakati mgumu kutokana na mvutano uliojitokeza mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi.
Anasema, “nilipata wakati mgumu hasa wakati wa kuaga kwa ajili ya kwenda kwenye mazoezi…. hakuna aliyeamini sanaa ni kitu chema na kinachoweza kumpatia mtu ajira…. nilichofanya ni kuhakikisha natekeleza mapema majukumu yangu ya nyumbani,” anasema.
Kwa kuwa alilazimika kufanya kazi za nyumbani kwa wakati alilazimika kusonga ugali wa mchana saa nne asubuhi na kuuweka katika chombo kinachohifadhi joto na kisha kuondoka
kwenda mazoezini.
Pili aliendelea kujikita katika sanaa na hivi karibuni alifanikiwa kuwa miongoni mwa washiriki 14 walioingia kwenye fainali za shindano la dansi la Serebuka. Pili ni mahiri katika mchezo
wa kunyumbulisha mwili hasa kuchezesha mabega, mikono na miguu, kucheza muziki wa dansi
wa asili ya Afrika, India pamoja na ngoma za makabila mbalimbali nchini Tanzania.
Anasema mwaka huu alikuwa miongoni mwa walimu waalikwa aliyepata nafasi ya kuwafundisha washiriki wa shindano la Tikisa katika mnyumbuliko wa mwili.
Pili alijiunga na kundi la Lumumba baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2005 anasema kuwa fani hiyo imempa mafanikio makubwa sana katika maisha yake, ikiwa ni pamoja na kufanya ziara katika nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya kushiriki sanaa za maonesho ya jukwaani.
“ Sanaa imeniwezesha kutembelea nchi za Denmark, Uganda, Kenya Msumbiji kushiriki katika
shughuli mbalimbali za sanaa ambazo zote zimeniingizia kipato kilichonifanya nibadilishe maisha yangu,” Pili anafahamisha.
Hata hivyo anasema hakuna kazi rahisi kwa kuwa anakumbana na changamoto mbalimbali
ikiwa ni pamoja na dhana potofu ambayo husababisha kazi za sanaa kudharauliwa badala ya
kuiangalia kama kazi ngingine.
“Unaweza kupata kazi, lakini linapokuja suala la malipo, wanataka wakulipe kidogo bila
kujali thamani ya kazi, hawajui hata wasanii tunatumia akili, muda na vifaa vinavyohitaji ukarabati kila kukicha,” Pili analalamika.
Changamoto nyingine inayomkabili Pili inatokana na baadhi ya watu wenye dhana potofu
kuwahusisha wanawake wasanii na ukahaba.
“Wakati mwanamke anapofanya onesho zuri jukwaani anaweza kujitokeza mwanamume na kwenda kumtunza kisha kutumia nafasi hiyo kumtomasatomasa …wengine kuandika kwenye vikaratasi kuomba miadi ya kufanya mapenzi na pia wapo wanaoomba namba za simu ili kuweka miadi ya mapenzi,” anaeleza.
Anasema jambo hili linamkwaza na siku zote huwa anajiuliza,” hivi hawa watu wananiona
mimi malaya?” Anawasihi watu wenye dhana potofu juu ya wasanii wa kike waache vitendo vya udhalilishaji na hasa kutumia nafasi ya kumtunza msanii kama mwanya wa kuwashikashika wasanii wanapokuwa majukwaani.
Hata hivyo anasisitiza kuwa changamoto hizo hazitamshawishi kubadilisha fani na badala
yake atasonga mbele ili kufikia lengo la kuwa mwalimu wa sanaa na hasa kuwafundishwa watoto ngoma za asili kutoka ndani na nje ya nchi.
Pili ambaye hivi leo anasherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwake aliyezaliwa mwaka 1988
akiwa mtoto wa nne kati ya saba. Ingawa hakubahatika kuendelea na elimu ya sekondari amebahatika kujiunga na kozi za Kiingereza, utamaduni na sanaa ya maonesho ya jukwaani ambapo ilimchukua miaka mitano kufuzu kozi ya sanaa ya kunyumbulisha mwili.
No comments:
Post a Comment