Hivi karibuni Taasisi ya kimataifa ya Hifadhi ya Jamii Duniani imeupatia mfuko huo tuzo ya kuwa mshindi wa kwanza wa ujumla barani Afrika kwa Taasisi na Mashirika yanayotoa huduma
za Hifadhi ya Jamii.
Katika mahojiano maalumu na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Emmanuel Humba,
anaeleza siri ya mafanikio na mikakati ya kuboresha huduma.
Humba anakiri kuwa NHIF imepitia katika hatua nyingi hadi kuwa mfuko wa mfano kuigwa barani Afrika kutokana na nchi mbalimbali kutuma wataalamu wake kuja kupata uzoefu wa namna ya kuendesha mifuko kama hiyo nchini mwao.
Humba anasema pamoja na ushindi huo wa jumla, Mfuko pia umetunukiwa vyeti vitatu vya heshima kwa umahiri na jitihada za kuboresha huduma bora katika maeneo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) hasa kuhusu kasi ya kuongezeka kwa wanaohudumiwa katika kipindi kifupi
tangu Serikali ikabidhi jukumu hilo kwa Uongozi wa NHIF Julai, 2009.
Huduma ya vifaa tiba kwa watoa huduma na utoaji wa huduma uliowezesha kuboresha huduma na kupunguza ukubwa wa tatizo la dawa na vifaa tiba hivyo kutoa mchango muhimu katika maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Umefanikiwa pia katika utoaji wa mafao na kusogeza huduma za Mfuko karibu na wanachama wake kupitia ufunguzi wa Ofisi za Kanda. Anafafanua kwamba tuzo hiyo kwa NHIF ilitolewa mjini Arusha na Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii Duniani (ISSA), Errol Frank
Stoove.
Tuzo hiyo ilitolewa katika mkutano wa wakuu wa mashirika ya pensheni na Bima za Afya Kanda ya Afrika uliofanyika Desemba mwaka jana mjini Arusha. Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) walikuwa waandaaji na waratibu wakuu huku Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uliwakilishwa na Mkurugenzi wake wa Uendeshaji, Eugen Mikongoti.
Kwa mujibu wa ISSA jumla ya Mashirika 21 ya Pensheni na Bima za Afya barani Afrika kutoka nchi 19 yaliwania tuzo hizo ambapo mshindi wa ujumla ilikuwa ni Tanzania kupitia NHIF.
Tanzania pia ilifanya vyema kwa kupata jumla ya tuzo nyingine tano za vyeti vya heshima ambazo tatu zilitwaliwa na NHIF, na nyingine mbili zilitolewa kwa Mfuko wa Akiba kwa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF) na Mfuko wa Pensheni wa PPF.
“Tuzo hizi hutolewa kila baada ya miaka mitatu na utaratibu huu ulianza mwaka 2008 katika Mkutano uliofanyika Kigali ambako Mfuko wa NHIF ulishiriki na kupata tuzo ya Heshima,” anasema Humba.
Anaendelea kusema, “Maeneo yaliyoshindaniwa yalikuwa ni pamoja na eneo la utawala bora, usimamizi wa majanga, mifumo habari, matekelezo, kuongeza wigo wa walengwa wa huduma na kujiandaa na mabadiliko na mahitaji yatokanayo na ukuaji wa idadi ya watu”.
Katika kuelezea mantiki ya tuzo hiyo, anasema ina maana kubwa kwao na kwa nchi nzima kwa kuwa imedhihirisha kuwa wamethubutu na kuweza. “Hii ni heshima kubwa kwa nchi na Mamlaka inayosimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA),” anasema.
Mfuko unaamini kuwa tuzo ambayo Tanzania imepata inatokana pia na mazingira na utamaduni wa Watanzania wa kujadiliana juu ya changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja na hivyo kuwa kivutio kwa mataifa mengine barani.
Anasema matarajio ya NHIF ni kuendelea kuzifanyia kazi changamoto za uboreshaji wa huduma. Matarajio ni kwamba baada ya tuzo hizo, watakuja wageni wengi watakaotaka kuja kuona na kujifunza zaidi kutoka Tanzania.
“Fundisho tunalolipata hapa ni kuwa nchi zetu zinazoendelea zina nafasi na fursa ya kutoa mafundisho kwa wenzetu wa mataifa mengine na hata kwa nchi zilizoendelea,” anasema.
Anasema mfuko utakabidhi Tuzo hizo kwa Serikali (Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii) ambayo ndio wizara mama na ambayo wanaamini kuwa mambo mengi wanayofanya
wanafanikiwa kwa sababu ya uongozi na ulezi wao.
“Tunatarajia Serikali na Mamlaka ya kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini watakuwa na mambo ya kuelezea zaidi kwenye suala hili ambalo sisi tunaliona kuwa ni alama ya ushindi kwa nchi yetu na kutupa nguvu na ari ya kushughulikia changamoto zinazowakabili wanachama wetu na wananchi wa ujumla,” anasema Humba.
Anasema mfuko sasa unajiandaa kushiriki kinyang’anyiro cha dunia mwakani ambapo mkutano mkubwa wa ulimwengu utafanyika nchini Qatar. Akiwashukuru wanachama na
Watanzania kwa ujumla, Humba anatoa mwito uwepo ushirikiano kwa kuwa katika juhudi za kuboresha huduma za matibabu kila mmoja ni mshindi.
“Hakuna anayeshindwa au aliyeshinda,” anasisitiza. Humba anasema mfuko umekuwa ukiongeza wanachama kwa wastani wa asilimia 14.5 kila mwaka na hadi kufikia Septemba mwaka jana, wanachama wameongezeka mara tatu zaidi ikilinganishwa na waliokuwepo mwaka 2001.
Humba anasema ongezeko hilo limetokana na Mfuko kuendelea kujumuisha makundi mengine kama vile wastaafu, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, majeshi ya polisi, magereza, uhamiaji na zimamoto.
Anasema mfuko una wanufaika wapatao 5,947,297 idadi ambayo ni sawa na asilimia 17.3 ya Watanzania wote. Asilimia 7.3 ni ya wanachama wa Bima ya Afya (NHIF) na asilimia 10.0 ya wanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Mlinganisho huo unazingatia idadi ya watu kama iliyotolewa na sensa ya mwaka 2002 yenye idadi ya watu wapatao 34.4 milioni.
Mkurugenzi huyo anasema hata hivyo, kwa kulinganisha na ukuaji wa idadi ya watu hadi kufikia Septemba mwaka jana, Tanzania inakisiwa kuwa na jumla ya Watanzania wapatao milioni 44.5.
Hivyo Mfuko unakadiriwa kutoa huduma kwa wanachama wapatao 5,947,297 ambayo ni sawa na asilimia 13.4 ya Watanzania wote. Anasema kati ya wanufaika 5,947,297 asilimia 42 ni wa NHIF na asilimia 58 ni wa CHF.
Anatoa mwito kwa wanachama waliosalia wapatao 58,945, ambao ni sawa na asilimia 13 ya wachangiaji wote wajaze fomu za uandikishaji ili wapatiwe vitambulisho. “Ni muhimu kujaza fomu hizo kwa sasa badala ya kusubiri mpaka waugue ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima,” anasema.
NHIF imeendelea kupanua wigo wa utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuongeza idadi ya vipimo. Pia idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma kwa wanachama wa mfuko huo vimekuwa vikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Awali, wakati mfuko huo unaanzishwa mwaka 2001, kulikuwa na upinzani mkali kutoka kwa
wanachama wa mfuko ambao pengine kwa kutokufahamu faida zake walikuwa wakipinga kukatwa fedha za kuchangia mfuko huo.
“Mimi sikukubali kabisa na nilikuwa napinga kukatwa mshahara wangu kwa ajili ya NHIF, kuna wakati nilikuwa nashawishi wenzangu kupiga vita mfuko huu lakini wote sisi leo ukituuliza nani hataki NHIF hakuna hata mmoja atakayekubali kutoka kwenye mfuko huu,” anasema.
Anashuhudia kauli za kuusifu zinazotolewa na watu wa kada tofauti kutokana na ambavyo wamekuwa wakinufaika kutokana na uwepo wake. Anahitimisha kwa kusisitiza kuwa NHIF itaendelea kukabili changamoto za uboreshaji huduma kuhakikisha kwamba mfuko unaendelea kuwa tegemeo la Watanzania wengi na mkombozi wa wanyonge.
No comments:
Post a Comment