Tuesday, 24 January 2012

MATONYA KUMILIKI HOTEL SOON, BONGO FLAVA OYEE!!!



UKIANGALIA historia yake, hakika unaweza kusema amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kampeni za kuuaga umasikini.

Cha kufurahisha zaidi ni kwamba, ameyapata mafanikio hayo kupitia muziki wa kizazi kipya ambao katika miaka ya hivi karibuni umekuwa na mvuto, na pia ni `biashara’ kubwa kwa wanaoweza kuzichanga vyema karata zao.

Tunamzungumzia Seif Shaaban, maarufu kama Matonya ambaye baada ya muongo mmoja wa kupigana kisanii, sasa anaanza kula matunda ya kipaji chake. Leo hii, Matonya wa kwenye muziki ni `milionea’ fulani hivi.

Na umilionea wake hakuurithi, bali ameusotea, akadunduliza na sasa ana jeuri ya kuitwa Mkurugenzi. Anamiliki biashara kadhaa, ikiwamo ya kuuza magari, lakini sasa amekuja na kitu kipya, hoteli yenye hadhi ambayo iko mbioni kuzinduliwa, baada ya kumtafuna msanii huyo zaidi ya Sh milioni 150.

Katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni, Matonya amethibitisha kuwa ndiye mmiliki wa hoteli hiyo iliyopo katikati ya Jiji la Tanga.

“Ni hoteli yangu, mali yangu iliyotokana na jasho la kazi yangu,” anasema mkali huyo ambaye aliwahi kuzushiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya na kukamatwa China, uzushi alioukana na kusema “sifanyi biashara hiyo, sifikirii kuifanya na wala sijawahi kukanyaga China”.

Anasisitiza kuwa, mafanikio yake yanatokana na kukuna kichwa na kutoa tungo na mashairi yenye hisia kali na mvuto kwa mashabiki wake, ndiyo maana ameweza kufanikiwa. “Tangu nianze muziki kazi zangu zimekuwa zikikubalika, nikaongeza idadi ya mashabiki wa ndani na nje ya nchi.

“Ndiyo maana kila kukicha nimekuwa nikipata mialiko ya kutumbuiza sehemu mbalimbali duniani, Ulaya, Marekani na hata Afrika nimezunguka,” anasema na kuhoji katika mazingira ya aina hiyo, kwa nini abaki katika maisha yale yale ya U-Matonya?

Anaongeza kusema: “Ndiyo maana mpaka hoteli yangu inafikia hatua hii, kila pesa imetoka mfukoni mwangu. Hata benki sijapiga hodi kukopa pesa ya biashara yangu hii ambayo natarajia kuizindua wakati wowote kuanzia sasa.”

Na wakati anajipanga kuizindua hoteli hiyo ambayo anaitafutia jina, Matonya yuko katika hatua za mwisho za kutoa kazi yake mpya kisanii, wimbo aliodai utakuwa gumzo unaoitwa Lesbian, yaani `Usagaji’. Katika wimbo huo, amewashirikisha wakali Abdul Naseeb `Diamond’ na Albert Mangweha `Ngwair’.

Kama ilivyo katika nyimbo zake zilizotangulia, nao umeangukia katika `mahaba’. Tofauti na mawazo ya wengi kuwa wasanii wanapaswa kubadilisha mwelekeo na kuachana na nyimbo za mapenzi, Matonya anasema nyimbo za mapenzi ndizo zinazouza.

“Kuna nyimbo nyingi za kusifia nchi, lakini hazifanyi vizuri sokoni ila nyimbo za mapenzi ndiyo zinauza,” anasema kijana huyo wa Kisambaa aliyekulia Barabara ya Tatu mjini Tanga. Miongoni mwa nyimbo za mapenzi zilizompatia umaarufu mkubwa Matonya ni pamoja na Anitha, Violeth, Taxi Bubu na nyingine kadha wa kadha.

Lakini kwa nini anaitwa Matonya? Mwenyewe anajibu: “Kweli kabisa nilikuwa napiga sana `mizinga’ marafiki zangu wakati nataka kurekodi kibao cha Uaminifu mwaka 2000, ndiyo maana wakaamua kunipa jina hilo nami nikalipokea.

Ndiyo, nilishajipanga kimuziki, lakini sikuwa na pesa za kuingia studio kurekodi, sikuona aibu kusaka pesa ya studio.” Anafafanua kuwa, wakati huo alikuwa kidato cha nne Sekondari ya Sahare iliyopo mjini Tanga.

Majibu yake yanatoa majibu mengine, ya kisa cha yeye kuitwa Matonya, jina la ombaomba maarufu nchini ambaye jina lake halisi ni Paulo Mawezi. Mzee huyo alipata umaarufu mkubwa baada ya `kusumbuana’ sana na aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba ambaye licha ya kumtimua mara kadhaa katika jiji hilo.

Staili yake ya kuomba kwa kawaida huwa ni `burudani’. Hulala chali huku mkono akiwa ameunyoosha juu kwa muda mrefu bila ya kutikisika hata kama jua ni kali kupita kiasi.

Huyo ndiye Matonya wa kwenye muziki ambaye baada ya kusota kwa miaka kadhaa, hatimaye ameanza kufungua milango ya mafanikio na sasa anatumia kila anachokipata kwa ajili ya ustawi wa maisha yake na familia yake na mkewe Miriam aliyezaa naye mtoto mmoja, Imran.

Je, atafanikiwa zaidi kibiashara? Bila shaka, kama ameweza kufika hapo, huenda akazidi kupaa na hivyo kutoa funzo kwa wasanii wengine nchini kuwa, kuna maisha mengine nje ya jukwaa la muziki.Cha kufurahisha zaidi ni kwamba, ameyapata mafanikio hayo kupitia muziki wa kizazi kipya ambao katika miaka ya hivi karibuni umekuwa na mvuto, na pia ni `biashara’ kubwa kwa wanaoweza kuzichanga vyema karata zao.

Tunamzungumzia Seif Shaaban, maarufu kama Matonya ambaye baada ya muongo mmoja wa kupigana kisanii, sasa anaanza kula matunda ya kipaji chake. Leo hii, Matonya wa kwenye muziki ni `milionea’ fulani hivi.

Na umilionea wake hakuurithi, bali ameusotea, akadunduliza na sasa ana jeuri ya kuitwa Mkurugenzi. Anamiliki biashara kadhaa, ikiwamo ya kuuza magari, lakini sasa amekuja na kitu kipya, hoteli yenye hadhi ambayo iko mbioni kuzinduliwa, baada ya kumtafuna msanii huyo zaidi ya Sh milioni 150.

Katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni, Matonya amethibitisha kuwa ndiye mmiliki wa hoteli hiyo iliyopo katikati ya Jiji la Tanga.

“Ni hoteli yangu, mali yangu iliyotokana na jasho la kazi yangu,” anasema mkali huyo ambaye aliwahi kuzushiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya na kukamatwa China, uzushi alioukana na kusema “sifanyi biashara hiyo, sifikirii kuifanya na wala sijawahi kukanyaga China”.

Anasisitiza kuwa, mafanikio yake yanatokana na kukuna kichwa na kutoa tungo na mashairi yenye hisia kali na mvuto kwa mashabiki wake, ndiyo maana ameweza kufanikiwa. “Tangu nianze muziki kazi zangu zimekuwa zikikubalika, nikaongeza idadi ya mashabiki wa ndani na nje ya nchi.

“Ndiyo maana kila kukicha nimekuwa nikipata mialiko ya kutumbuiza sehemu mbalimbali duniani, Ulaya, Marekani na hata Afrika nimezunguka,” anasema na kuhoji katika mazingira ya aina hiyo, kwa nini abaki katika maisha yale yale ya U-Matonya?

Anaongeza kusema: “Ndiyo maana mpaka hoteli yangu inafikia hatua hii, kila pesa imetoka mfukoni mwangu. Hata benki sijapiga hodi kukopa pesa ya biashara yangu hii ambayo natarajia kuizindua wakati wowote kuanzia sasa.”

Na wakati anajipanga kuizindua hoteli hiyo ambayo anaitafutia jina, Matonya yuko katika hatua za mwisho za kutoa kazi yake mpya kisanii, wimbo aliodai utakuwa gumzo unaoitwa Lesbian, yaani `Usagaji’. Katika wimbo huo, amewashirikisha wakali Abdul Naseeb `Diamond’ na Albert Mangweha `Ngwair’.

Kama ilivyo katika nyimbo zake zilizotangulia, nao umeangukia katika `mahaba’. Tofauti na mawazo ya wengi kuwa wasanii wanapaswa kubadilisha mwelekeo na kuachana na nyimbo za mapenzi, Matonya anasema nyimbo za mapenzi ndizo zinazouza.

“Kuna nyimbo nyingi za kusifia nchi, lakini hazifanyi vizuri sokoni ila nyimbo za mapenzi ndiyo zinauza,” anasema kijana huyo wa Kisambaa aliyekulia Barabara ya Tatu mjini Tanga. Miongoni mwa nyimbo za mapenzi zilizompatia umaarufu mkubwa Matonya ni pamoja na Anitha, Violeth, Taxi Bubu na nyingine kadha wa kadha.

Lakini kwa nini anaitwa Matonya? Mwenyewe anajibu: “Kweli kabisa nilikuwa napiga sana `mizinga’ marafiki zangu wakati nataka kurekodi kibao cha Uaminifu mwaka 2000, ndiyo maana wakaamua kunipa jina hilo nami nikalipokea.

Ndiyo, nilishajipanga kimuziki, lakini sikuwa na pesa za kuingia studio kurekodi, sikuona aibu kusaka pesa ya studio.” Anafafanua kuwa, wakati huo alikuwa kidato cha nne Sekondari ya Sahare iliyopo mjini Tanga.

Majibu yake yanatoa majibu mengine, ya kisa cha yeye kuitwa Matonya, jina la ombaomba maarufu nchini ambaye jina lake halisi ni Paulo Mawezi. Mzee huyo alipata umaarufu mkubwa baada ya `kusumbuana’ sana na aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba ambaye licha ya kumtimua mara kadhaa katika jiji hilo.

Staili yake ya kuomba kwa kawaida huwa ni `burudani’. Hulala chali huku mkono akiwa ameunyoosha juu kwa muda mrefu bila ya kutikisika hata kama jua ni kali kupita kiasi.

Huyo ndiye Matonya wa kwenye muziki ambaye baada ya kusota kwa miaka kadhaa, hatimaye ameanza kufungua milango ya mafanikio na sasa anatumia kila anachokipata kwa ajili ya ustawi wa maisha yake na familia yake na mkewe Miriam aliyezaa naye mtoto mmoja, Imran.

Je, atafanikiwa zaidi kibiashara? Bila shaka, kama ameweza kufika hapo, huenda akazidi kupaa na hivyo kutoa funzo kwa wasanii wengine nchini kuwa, kuna maisha mengine nje ya jukwaa la muziki.

Saturday, 21 January 2012

CHEKENI MNENEPE, WADAU


Mwizi na Mlegezo

Saggy
Mtindo wa Kata K
Mwizi mmoja hapa London aliyekuwa akijaribu kukimbia baada ya kufanya wizi wake, aliuhisi mkono wa sheria ukimkamata baada ya kuanguka, kwa kuwa alikuwa amevaa suruali yake katika mtindo uitwao mlegezo, au kata K.
Gazeti la Metro limesema John O'Dell alisimamishwa na polisi katika eneo la harringey, kaskazini mwa London siku ya Jumapili, lakini badala yake akaamua kukimbia.
Hata hivyo, kwa kuwa alikuwa amevaa suruali yake bila mkanda na katika mtindo wa mlegezo, suruali hiyo iliteremka na kumfanya adondoke na kukamatwa na polisi mara moja. Tukio hilo lilishuhudiwa na wapita njia. Mpita njia Harry Robbins aliyeshuhudia sakata hilo amesema, kwa kuwa hakuwa amevaa mkanda, ilikuwa ni kichekesho jinsi suruali yake mwenyewe ilivyomuangusha na kusababisha kukamatwa. Wote tuliokuwepo tulibaki tukicheka, amesema Robbins. Mwizi huyo baada ya kukamatwa alikiri kuiba laptop ya karibu dola mia tano -- atafikishwa mahakamani Januari 31.

Mimba ya Mochuari

Mochuari
Mfanyakazi wa mochuari

Mwanamama mmoja nchini Marekani anayefanya kazi mochuari ameingia matatani baada ya kupata uja uzito kwa kujamiiana na mtu aliyekufa. Mtandao wa habari wa dead serious news umesema tukio hilo linadhaniwa kutokea katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Mourning Glory, nje ya Lexington, Missouri.
Polisi wa mjini humo wamemshtaki mama huyo aitwaye Felicity Marmaduke kwa kosa la kunajisi na kuchezea maiti. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na polisi, kiungo cha kiume cha mwili wa mtu aliyekufa kilihamasika wakati mwili ukioshwa. Taarifa zinasema, kwa kuwa mwanamama huyo alikuwa peke yake, aliamua kujamiiana na mwili huo.
Kwa mshangao hata wa mwanamama huyo, maiti huyo alitoa mbegu za kiume. Wiki chache baadaye Bi Marmaduke alijikuta ni mja mzito. Baada ya kumwambia daktari wake mfululizo wa matukio, daktari huyo aliwataarifu polisi.
Bi Marmaduke alikamatwa na polisi akiwa nyumabni kwake, si mbali sana na mochuari anayofanyia kazi. Katika tukio la kushangaza zaidi, mwanamama huyo amesema anapanga kudai urithi kutoka kwa familia ya mtu huyo aliyekufa.

Wasiolia kupewa adhabu?

Kim
Mazishi ya Kim Jong-il
Mamlaka za Korea kaskazini zinadaiwa kuwaadhibu wananchi wake kwa kuwapeleka jela na kazi ngumu-- wale wote ambao hawakulia vya kutosha katika msiba wa kiongozi wao Kim Jong-il.
Gazeti la kila siku lenye makao yake makuu Korea Kusini NK limesema yeyote ambaye hakushiriki misa ya kihistoria ya kumuenzi Kim au ambaye alihudhuria lakini hakulia kiasi cha kutosha au kuonekana kulia kwa uongo, atapelekwa katika kambi maalum na kufanyishwa kazi ngumu kwa miezi sita, limeripoti gazeti hilo.
Gazeti hilo limedai huku likikariri chanzo ambacho haikukitaja kuwa yeyote aliyejaribu kutoka nje ya nchi wakati huo atashtakiwa katika mahakama mbele ya kadamnasi. Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao wa cnews.com, wengine watapelekwa katika kambi na kupewa elimu upya ya utaifa.
Hakuna taarifa rasmi kutoka Korea kaskazini iliyothibitisha taarifa hizi. Hata hivyo shirika la habari la Korea Kaskazini limeripoti wiki iliyopita kuwa kifo cha Kim Jong-il kiliombolezwa hadi na wanyama wa porini.
"Dubu mmoja akiwa na wanae walionekana wakiwa wanalia kwa nguvu" imesema taarifa ya shirika hilo. Madubu hao sio wanyama pekee ambao wameripotiwa kumuomboleza kiongozi huyo.
Shirika hilo liliripoti mwezi uliopita kuwa mamia ya kunguru aina ya Magpies walionekana wakipeperuka kuzunguka sanamu la Rais Kim katika wilaya ya Magyondae.

Polisi mwizi

Police
Polisi wa Moscow

Polisi katika mji wa St Petersburg wamesema wamemkamata afisa wa polisi akiwa anaendesha gari la wizi.
Gazeti la RIA Novosti limeripoti siku ya Alhamis kuwa polisi huyo kapteni Andrei Makononeko alikutwa akiendesha gari ya wizi aina ya Lexus na huenda akafunguliwa mashtaka. Kamati ya uchunguzi ya Urusi imesema polisi huyo alikamatwa Januari 10. Gari hilo liliibiwa mwezi Novemba, wamesema polisi. Uchunguzi unafanyika kutazama iwapo mashtaka yafunguliwe dhidi ya afisa huyo.

Usipige 999 hovyo

Police
Polisi wa Uingereza
Polisi wa Uingereza wamewataka wananchi wake kutotumia hovyo namba ya dharura, baada ya mtu mmoja kupiga simu na kuripoti ugomvi uliokuwa ukitokea kwenye TV.
Mtandao wa MSN umesema bwana mmoja alipiga simu polisi baada ya ugomvi kuzuka katika tamthilia aliyokuwa akitazama kwenye TV.
Taarifa zinasema bwana huyo alikuwa akitazama tamthilia maarufu Uingereza iitwayo EastEanders, na kipande hicho chenye mzozano kilirekodiwa mwaka 2009. Taarifa za polisi zimetolewa ili kuwafahamisha wananchi umuhimu wa kutumia simuza dharura, na kuainisha zipi ni dharura na zipi sio dharura.

WANAWAKE WAPIGWA KWA KUVAA SURUALI, MALAWI



 20 Januari, 2012 - Saa 13:07 GMT
Rais Bingu wa Mutharika
Takriban watu 3,000 wamekusanyika Blantyre nchini Malawi kupinga mashambulio dhidi ya wanawake wanaovaa suruali.
Baadhi ya wachuuzi wa kike wiki hii walipigwa na kuvuliwa nguo kwenye mitaa ya mji mkuu, Lilongwe, na Blantyre kwa kutovaa mavazi ya asili.
Mmoja aliyeandaa maandamano hayo ameiambia BBC amewasihi wanawake kujitokeza wakiwa wamevaa suruali na fulana nyeupe kuonyesha kukasirishwa kwao.
Rais Bingu wa Mutharika alisema kupitia redio ya taifa kuwa wanawake wana haki ya kuvaa wanachotaka.
Alikana taarifa kuwa aliamuru wanawake waache kuvaa suruali.
Mpaka mwaka 1994, wanawake kwenye nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye misimamo mikali walikatazwa kuvaa suruali au sketi fupi chini ya uongozi wa kidikiteta wa Hastings Banda.
Wanaume pia walikatazwa kuwa na nywele ndefu.
Wanawake pia wameshambuliwa kwa kuvaa suruali katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Zimbabwe katika miaka ya hivi karibuni.

'Kukatishwa tamaa kutokana na hali ya uchumi'

Mwandishi wa BBC aliyopo Blantyre Raphael Tenthani alisema makamu wa Rais Joyce Banda, waziri wa jinsia, wabunge kadhaa, wahadhiri wa chuo kikuu na wanaharakati walihudhuria maandamano ya Ijumaa.
Seodi White, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za wanawake na aliyeandaa maandamano hayo, alisema wanawake hao hawakuvaa mavazi yasiyo ya heshima.
"Ndio Malawi ni nchi yenye msimamo mkali. Lakini tumekuwa tukivaa tunavyotaka, kwa kiwango cha heshima inayotakiwa, ambayo ni kiwango cha watu wote duniani, kwa miaka 18. Na hakuna anayeweza kusimama akasema ni kinyume na Wamalawi, " alikiambia kipindi cha Network Afrika cha BBC.
Alisema wanawake walikuwa wakilengwa na vijana ambao hawafurahishwi na hali ya kiuchumi nchini humo.
"Wachuuzi unaowaona mitaani si watu wazima. Hawa ni vijana, wadogo wa kuwa hata umri wa watoto wangu.
"Wananieleza mimi kuhusu utamaduni? Wananiambia mimi namna ya kuvaa?
"Hivi hili suala kweli ni kuhusu utamaduni au kitu kingine kinachohusiana na hali ngumu ya uchumi wanayokubaliana nayo watu wakitafuta namna ya kutoa hasira zao?
Awali, Bi Banda pia alilaumu mashambulio hayo kutokea kutokana na uchumi nchini Malawi, ambapo kwa sasa kuna upungufu mkubwa wa mafuta na fedha za kigeni.

MILIPUKO YATIKISA MJI WA KANO, NIGERIA

Mji wa Kano
Milipuko ilitokea katika mji wa Kano


Watu kadhaa wameripotiwa kuuawa kwenye milipuko iliyotokea katika mji wa Kano, kaskazini mwa Nigeria.
Vituo vya Polisi pamoja na makao makuu ya Polisi eneo hilo ni miongoni mwa sehemu zilizolengwa katika mashambulizi hayo.
Milio ya risasi pia imesikika katika sehemu kadhaa.
Kundi la kiislamu la Boko Haram limesema ndilo lililotekeleza mashambulizi hayo.
Kundi hilo ndilo limekuwa likiendesha ghasia katika siku za hivi karibuni, kwenye eneo la kaskazini mwa Nigeria, lililo na Waislamu wengi.
Utawala katika jimbo la Kano umetangaza amri ya kutotoka nje ya muda wa saa 24.
Walioshuhudia walisema watu wawili waliuawa.
Lakini taarifa zingine ambazo hazikuthibitishwa zilisema idadi ya waliokufa ni kubwa zaidi.
Mwandishi wa BBC mjini Kano anasema kulikuwa na vurumai katika mji, huku moshi mkubwa ukitanda angani.
Mwandishi wetu anasema mbali na makao makuu ya Polisi yaliyoko magharibi mwa mji huo, vituo vingine vya Polisi kwenye eneo la katikati na kusini vililengwa.
Pia ufyataulianaji wa risasi uliripotiwa kwenye jengo muhimu la Polisi mashariki mwa mji.
Mkazi mmoja karibu na mji huo aliambia BBC kwamba aliona miili ikibebwa kutoka kituo cha Polisi karibu na eneo la kati kati mwa mji, lakini hakujua watu hao walikuwa wamekufa au kujeruhiwa.
Walioshuhudia walisema mlipuaji aliyeshambulia makao makuu ya Polisi alikaribia jengo hilo akiendesha pikipiki, akashuka na kukimbia ndani ya jengo akibeba mfuko.
Mlipuko mwingine ulikuwa katika afisi ya kutoa paspoti ya Kano.
Boko Haram limekiri kuhusika pia.
Msemaji wa kundi hilo Abul Qaqa, aliambia BBC akiwa kaskazini mwa mji wa Maiduguri ambao ndio ngome yao kwamba walitekeleza mashambulizi hayo kwa sababu serikali imekataa kuwaachia huru wafuasi waliokamatwa mjini Kano.
Kundi hilo linataka kuwepo utawala wa Kiislamu nchini Nigeria.
Lilianzisha ghasia mwaka 2010 mjini Maiduguri, zaidi likilenga taasisi za serikali.
Wadadisi wanasema shambulio la Ijumaa ni mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutekelezwa na Boko Haram, na kubwa zaidi mjini Kano.

Friday, 20 January 2012

KOMBE LA MATAIFA YA AFRICA 2012.


Uwanja wa Bata
Equatorial Guinea na Libya kufungua dimba
Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yanaanza wikendi hii, mechi ya ufunguzi ikichezewa Bata kati ya waandalizi Equatorial Guinea (wakishirikiana na Gabon) dhidi ya Libya.


Bila shaka Libya itajaribu kuonyesha picha mpya, kufuatia mabadiliko ya kisiasa.
Libya iliwashangaza wengi ilipofuzu kuingia katika mashindano hayo, baada ya kutofungana mabao (0-0) ilipocheza na Zambia.
Hii nafasi kwa timu ya Libya kuanza upya, na baada ya kuitupa bendera yake iliyokuwa na msitari wa kijani kibichi, na kuanza kutumia iliyo na rengi nyekundu na nyeupe, na kuipatia timu jina jipya la Mediterranean Knights.
Hakuna anayeweza kusema kwamba maandalizi ya michuano hii ni kazi rahisi.
Ingawa Equatorial Guinea na Gabon ni mataifa jirani, kiutamaduni na kisiasa yana tofauti kubwa.
Equatorial Guinea ni taifa ambalo limeongozwa na Teodoro Obiang, ambaye ni kati ya marais wa Afrika ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu sana barani Afrika.
Kifedha, ni taifa ambalo linanawiri kutokana na utajiri wake mkubwa kwa kutoa mafuta.
Hata hivyo, nchi hiyo inalaumiwa na wengi kwa kukosa uhuru wa kujielezea, na kwa kutozingatia haki mbalimbali za binadamu.
Nchini Gabon, rais Ali Bongo ndio tu ameweza kuwa imara zaidi, baada ya kupata kuungwa mkono na wengi katika bunge la nchi hiyo, kufuatia uchaguzi wa mwezi Desemba, ambao baadhi ya viongozi wa upinzani walitaka ususiwe.
Lugha ya taifa nchini Gabon ni kifaransa, lakini kihispania kunazungumzwa Equatorial Guinea.
Miji itakayochezewa mechi iko mbalimbali, na baya zaidi, mji mkuu wa Equatorial Guinea, Malaba, upo katika kisiwa cha Bioko, karibu na Cameroon.
Mashirika mapya ya vyombo vya habari yamechukizwa na ukiritimba na ugumu katika kupata vibali vya kuingia nchini humo na kutangaza moja kwa moja mechi zitakazochezwa katika mataifa hayo.
Vile vile kuna wasiwasi hali ya usalama itakuwa vipi, katika kuwapokea mamia ya waandishi wa habari, na vikundi mbalimbali vya wafanyikazi wa mashirika ya redio na televisheni.
Mashabiki wa soka barani Afrika wanauhusudu sana kandanda.
Lakini ni wangapi watasafiri, kwa mfano, kutoka Zambia hadi Bata?
Hata hivyo, licha ya matatizo ya usafiri, kuna matumaini kwamba michuano itakuwa ya kuvutia, na mataifa kama Niger na Botswana, yaliyofuzu kushiriki kwa mara ya kwanza, yataonyesha mchezo wa kusisimua.
Wengi wataitazama Niger, hasa kwa kuwa majirani Nigeria walishindwa kufuzu; lakini watapambana na ushindani mkali kutoka kwa Gabon, Tunisia na vile vile Morocco.
Muhimu pia katika mashindano haya ni suala la ni nani hayupo.
Sio tu Nigeria, lakini miamba mingine ya soka, Afrika Kusini, Cameroon na wachezaji hodari wa Misri, wote walishindwa kufuzu.
Je, kukosekana kwao kutakuwa na athari gani katika ubora wa mechi zitakazochezwa?
Ama labda mashabiki wengi watayageuzi mashindano kisogo kwa kukosekana miamba hiyo?
Lakini pasipo majina hayo makubwa, hii ni nafasi kwa wageni pia kuondoka na kombe.
Ivory Coast wanatazamiwa na wengi kuondoka na ushindi, lakini mataifa ya Ghana na Senegal pia yana nafasi nzuri.
Kutokuwepo kwa Misri ni matumaini kwa mabingwa hapo zamani, Morocco au Tunisia, kutazamiwa na mashabiki wa Afrika ya Kaskazini kulifikisha kombe huko.

Thursday, 12 January 2012

NHIF YANG'ARA AFRICA KWA UKOMBOZI WA WANYONGE!!


Image
TANGU kuanzishwa kwake mwaka 2001 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepitia milima na mabonde. 

Hivi karibuni Taasisi ya kimataifa ya Hifadhi ya Jamii Duniani imeupatia mfuko huo tuzo ya kuwa mshindi wa kwanza wa ujumla barani Afrika kwa Taasisi na Mashirika yanayotoa huduma 
za Hifadhi ya Jamii. 

Katika mahojiano maalumu na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Emmanuel Humba, 
anaeleza siri ya mafanikio na mikakati ya kuboresha huduma. 

Humba anakiri kuwa NHIF imepitia katika hatua nyingi hadi kuwa mfuko wa mfano kuigwa barani Afrika kutokana na nchi mbalimbali kutuma wataalamu wake kuja kupata uzoefu wa namna ya kuendesha mifuko kama hiyo nchini mwao. 

Humba anasema pamoja na ushindi huo wa jumla, Mfuko pia umetunukiwa vyeti vitatu vya heshima kwa umahiri na jitihada za kuboresha huduma bora katika maeneo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) hasa kuhusu kasi ya kuongezeka kwa wanaohudumiwa katika kipindi kifupi 
tangu Serikali ikabidhi jukumu hilo kwa Uongozi wa NHIF Julai, 2009. 

Huduma ya vifaa tiba kwa watoa huduma na utoaji wa huduma uliowezesha kuboresha huduma na kupunguza ukubwa wa tatizo la dawa na vifaa tiba hivyo kutoa mchango muhimu katika maendeleo ya sekta ya afya nchini. 

Umefanikiwa pia katika utoaji wa mafao na kusogeza huduma za Mfuko karibu na wanachama wake kupitia ufunguzi wa Ofisi za Kanda. Anafafanua kwamba tuzo hiyo kwa NHIF ilitolewa mjini Arusha na Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii Duniani (ISSA), Errol Frank 
Stoove. 

Tuzo hiyo ilitolewa katika mkutano wa wakuu wa mashirika ya pensheni na Bima za Afya Kanda ya Afrika uliofanyika Desemba mwaka jana mjini Arusha. Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) walikuwa waandaaji na waratibu wakuu huku Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uliwakilishwa na Mkurugenzi wake wa Uendeshaji, Eugen Mikongoti. 

Kwa mujibu wa ISSA jumla ya Mashirika 21 ya Pensheni na Bima za Afya barani Afrika kutoka nchi 19 yaliwania tuzo hizo ambapo mshindi wa ujumla ilikuwa ni Tanzania kupitia NHIF. 

Tanzania pia ilifanya vyema kwa kupata jumla ya tuzo nyingine tano za vyeti vya heshima ambazo tatu zilitwaliwa na NHIF, na nyingine mbili zilitolewa kwa Mfuko wa Akiba kwa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF) na Mfuko wa Pensheni wa PPF. 

“Tuzo hizi hutolewa kila baada ya miaka mitatu na utaratibu huu ulianza mwaka 2008 katika Mkutano uliofanyika Kigali ambako Mfuko wa NHIF ulishiriki na kupata tuzo ya Heshima,” anasema Humba. 

Anaendelea kusema, “Maeneo yaliyoshindaniwa yalikuwa ni pamoja na eneo la utawala bora, usimamizi wa majanga, mifumo habari, matekelezo, kuongeza wigo wa walengwa wa huduma na kujiandaa na mabadiliko na mahitaji yatokanayo na ukuaji wa idadi ya watu”. 

Katika kuelezea mantiki ya tuzo hiyo, anasema ina maana kubwa kwao na kwa nchi nzima kwa kuwa imedhihirisha kuwa wamethubutu na kuweza. “Hii ni heshima kubwa kwa nchi na Mamlaka inayosimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA),” anasema. 

Mfuko unaamini kuwa tuzo ambayo Tanzania imepata inatokana pia na mazingira na utamaduni wa Watanzania wa kujadiliana juu ya changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja na hivyo kuwa kivutio kwa mataifa mengine barani. 

Anasema matarajio ya NHIF ni kuendelea kuzifanyia kazi changamoto za uboreshaji wa huduma. Matarajio ni kwamba baada ya tuzo hizo, watakuja wageni wengi watakaotaka kuja kuona na kujifunza zaidi kutoka Tanzania. 

“Fundisho tunalolipata hapa ni kuwa nchi zetu zinazoendelea zina nafasi na fursa ya kutoa mafundisho kwa wenzetu wa mataifa mengine na hata kwa nchi zilizoendelea,” anasema. 

Anasema mfuko utakabidhi Tuzo hizo kwa Serikali (Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii) ambayo ndio wizara mama na ambayo wanaamini kuwa mambo mengi wanayofanya 
wanafanikiwa kwa sababu ya uongozi na ulezi wao. 

“Tunatarajia Serikali na Mamlaka ya kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini watakuwa na mambo ya kuelezea zaidi kwenye suala hili ambalo sisi tunaliona kuwa ni alama ya ushindi kwa nchi yetu na kutupa nguvu na ari ya kushughulikia changamoto zinazowakabili wanachama wetu na wananchi wa ujumla,” anasema Humba. 

Anasema mfuko sasa unajiandaa kushiriki kinyang’anyiro cha dunia mwakani ambapo mkutano mkubwa wa ulimwengu utafanyika nchini Qatar. Akiwashukuru wanachama na 
Watanzania kwa ujumla, Humba anatoa mwito uwepo ushirikiano kwa kuwa katika juhudi za kuboresha huduma za matibabu kila mmoja ni mshindi. 

“Hakuna anayeshindwa au aliyeshinda,” anasisitiza. Humba anasema mfuko umekuwa ukiongeza wanachama kwa wastani wa asilimia 14.5 kila mwaka na hadi kufikia Septemba mwaka jana, wanachama wameongezeka mara tatu zaidi ikilinganishwa na waliokuwepo mwaka 2001. 

Humba anasema ongezeko hilo limetokana na Mfuko kuendelea kujumuisha makundi mengine kama vile wastaafu, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, majeshi ya polisi, magereza, uhamiaji na zimamoto. 

Anasema mfuko una wanufaika wapatao 5,947,297 idadi ambayo ni sawa na asilimia 17.3 ya Watanzania wote. Asilimia 7.3 ni ya wanachama wa Bima ya Afya (NHIF) na asilimia 10.0 ya wanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Mlinganisho huo unazingatia idadi ya watu kama iliyotolewa na sensa ya mwaka 2002 yenye idadi ya watu wapatao 34.4 milioni. 

Mkurugenzi huyo anasema hata hivyo, kwa kulinganisha na ukuaji wa idadi ya watu hadi kufikia Septemba mwaka jana, Tanzania inakisiwa kuwa na jumla ya Watanzania wapatao milioni 44.5. 

Hivyo Mfuko unakadiriwa kutoa huduma kwa wanachama wapatao 5,947,297 ambayo ni sawa na asilimia 13.4 ya Watanzania wote. Anasema kati ya wanufaika 5,947,297 asilimia 42 ni wa NHIF na asilimia 58 ni wa CHF. 

Anatoa mwito kwa wanachama waliosalia wapatao 58,945, ambao ni sawa na asilimia 13 ya wachangiaji wote wajaze fomu za uandikishaji ili wapatiwe vitambulisho. “Ni muhimu kujaza fomu hizo kwa sasa badala ya kusubiri mpaka waugue ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima,” anasema. 

NHIF imeendelea kupanua wigo wa utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuongeza idadi ya vipimo. Pia idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma kwa wanachama wa mfuko huo vimekuwa vikiongezeka mwaka hadi mwaka. 

Awali, wakati mfuko huo unaanzishwa mwaka 2001, kulikuwa na upinzani mkali kutoka kwa 
wanachama wa mfuko ambao pengine kwa kutokufahamu faida zake walikuwa wakipinga kukatwa fedha za kuchangia mfuko huo. 

“Mimi sikukubali kabisa na nilikuwa napinga kukatwa mshahara wangu kwa ajili ya NHIF, kuna wakati nilikuwa nashawishi wenzangu kupiga vita mfuko huu lakini wote sisi leo ukituuliza nani hataki NHIF hakuna hata mmoja atakayekubali kutoka kwenye mfuko huu,” anasema. 

Anashuhudia kauli za kuusifu zinazotolewa na watu wa kada tofauti kutokana na ambavyo wamekuwa wakinufaika kutokana na uwepo wake. Anahitimisha kwa kusisitiza kuwa NHIF itaendelea kukabili changamoto za uboreshaji huduma kuhakikisha kwamba mfuko unaendelea kuwa tegemeo la Watanzania wengi na mkombozi wa wanyonge.

NYOKA WA AJABU MWENYE PEMBE AONEKANA TANZANIA!!!


Image
WATAALAMU wanaoshughulika na hifadhi ya mazingira nchini Tanzania wamegundua 
kipiribao (nyoka mwenye sumu kali) mwenye pembe ambaye wanasema yuko katika hatari ya kutoweka. 

Nyoka huyo mwenye rangi za kupendeza za njano na nyeusi ameelezwa kufanana na nyoka 
anayepatikana katika milima ya Usambara na hata Uluguru anayekwenda kwa jina la Usambara. 

Nyoka huyo mpya ambaye makazi yake bado kuelezwa kiusahihi anapatikana katika nyanda za juu kusini mwa Tanzania na alibainika wakati wa tathmini za kibaiolojia kwa mwaka 2010 na 2011 katika maeneo hayo. 

Wataalamu wanaohusika na utafiti huo wamekataa kuelezea eneo halisi wanakopatikana nyoka hao kwa hofu ya wapenzi wa wanyama kwenda kuwawinda na kuwatwaa wakati viumbe hao inaonekana wapo katika kundi la wanaotoweka duniani. 

Kipiribao huyo ambaye alielezwa kwa undani katika jarida la utafiti la Zootaxa la Desemba 6,2011 anaonekana kama mwindaji wa usiku na chakula chake kikuu ni vyura ambao huwapata kandoni mwa mito. 

Kwa mujibu wa maelezo nyoka huyo anafanana na kipiribao mwingine anayejulikana kama Usambara ambaye inaaminika hupatikana pia katika milima ya Uluguru. 

Matilda ambaye kwa jina la kibaolojia anajulikana pia kama Atheris matildae, alipewa jina hilo kwa heshima ya binti wa Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la hifadhi ya wanyama Tim Davenpor, ambaye pia ni mwandishi mwenza wa taarifa hiyo ya utafiti kuhusu nyoka iliyochapishwa katika jarida hilo la kimataifa. 

Ukimwangalia nyoka huyo rangi za njano na nyeusi zimekosa na kuonekana waziwazi na ama hakika huna sababu ya kuhoji rangi aliyopakwa na Mungu. Nyoka huyu mpya ana urefu wa 
futi 2.1 na ana pembe zilizotengenezwa kwa magamba juu ya macho yake yaliyojitokeza kama ya kinyonga. 

Hakuna mtu kwa uhakika anayejua kwanini nyoka hawa wana pembe ingawa kuna watu wanabuni maelezo kwa kuzingatia mazingira ya nyoka hao walipoonekana. Lakini wengi wanakubaliana na nadharia kwamba zinahami macho au hata ya kujitambulisha miongoni 
mwa nyoka wenyewe wakati wa kutafuta wapenzi. 

Inawezekana kabisa kuwa pembe hizo zina kazi mbalimbali; lakini katika hilo Davenport na wenzake hawajishughulishi nalo. Wao hasa kinachowashughulisha ni uwezekano wa majangili kuwanasa nyoka hao na kuwauza kwa watu wengine na ndio maana watafiti hao mpaka sasa hawataki kusema kwa yakini wapi wanapatikana nyoka hao. 

Lakini pamoja na kutosema walieleza kuwa wanapatikana katika eneo dogo na tayari limeshaharibiwa vibaya na watengeneza mkaa na wakata mbao. Davenport na wenzake 
wanaamini kwamba aina hii ya nyoka itawekwa katika daraja la wanaotishia kutoweka kabisa duniani. 

Pamoja na tatizo hilo wameanzisha eneo dogo kwa ajili ya kuzaliana kwa nyoka hao. Tofauti ya Matilda na Usambara labda ni katika rangi na urefu. Usambara (Atheris ceratophora) ni kipiribao anayepatikana katika safu chache za milima nchini Tanzania na ambaye hukua kufikia sentimeta 54 huku wa kike wakiwa wakubwa kuliko wa kiume. 

Urefu wa kipiribao dume wa Usambara ni kama sentimeta 42 na mkia wake ni kama sentimeta nane. Rangi ya kipiribao wa Usambara ni njano inayoelekea katika ukijani na wakati mwingine akiwa na rangi ya kijivu.Tumbo lake kama rangi ya chungwa. 

Pamoja na kwamba wanasema nyoka matilda anafanana na Usambara bado ana tabia zake ambazo wataalamu wanaanza kujifunza lakini wakati wanajifunza wanatafuta njia mbadala za kumwezesha kuendelea kuwapo katika eneo ambalo linaharibiwa mazingira yake kwa kasi. 
Nyoka aina ya Atheris matildae anavyoonekana kwa mbele.

Tuesday, 10 January 2012

MKATABA WA UJENZI DARAJA LA KIGAMBONI WASAINIWA!!


Hatimaye ujenzi wa daraja la Kigamboni unatarajiwa kuanza hivi karibuni, baada ya jana Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na mkarandasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo, kutia saini mkataba wa makubaliano.
Ujenzi huo utatekelezwa na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group Co. Ltd kwa kushirikiana na China Major Bridge Co. Ltd na utagharimu Sh. 214,639,445,523.80 kwa kipindi cha miaka mitatu.
MAGUFULI: TUFANYE KAZI, TUACHE SIASA
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alimtaka mkandarasi kukamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo hata kabla ya muda uliowekwa, lakini azingatie ubora wa kazi.
“Sioni sababu ya kusubiri muda huo kwa sababu pesa zipo; nataka mradi huu ukamilike kabla ya muda uliopangwa ili Rais Jakaya Kikwete auzindue kabla hajamaliza muda wake,” alisema.
Dk. Mgufuli, aliwaasa viongozi na wananchi kwa ujumla kuacha siasa kwenye masuala yanayohusu maendeleo kwa kuwa siasa inakwamisha mipango mbalimbali.
“Watanzania sasa wamechoka na maneno wanataka utekelezaji, tufanyekazi tuache siasa, zitatupotezea muda na zitatupeleka pabaya,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza: “Ifike mahali tuache kusimamia siasa tupambane kuwaletea Watanzania maendeleo.”
Kuhusu miradi mingine, alisema serikali inatekeleza miradi mingi ya ujenzi wa barabara na madaraja na kwamba makandarasi wamekuwa wakituma maombi kila siku.
Alisema serikali imejipanga kupanua barabara ya Morogoro kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze na ya kutoka Arusha-Himo, mkoani Kilimanjaro; pamoja na ile ya mabasi ya mwendokasi kutoka Kimara hadi Kivukoni, jijini Dar es Salaam.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, alisema daraja hilo litakuwa la njia sita za lami za magari na njia za waenda kwa miguu.
Aliishukuru serikali kwa kukubali kuchangia asilimia 40 ya gharama za ujenzi na kuahidi kwamba shirika lake litaendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali yenye manufaa kwa taifa.
AJIRA 2,000 KUZALISHWA
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema mradi huo utazalisha ajira za muda mfupi zaidi ya 2,000 na kuwataka wananchi hususani vijana kuzichangamkia na kuhakikisha wanafanyakazi kwa bidii na uadilifu.
Hata hivyo, aliwaonya watu wenye tabia za wizi kutothubutu kwenda kwenye mradi huo kwa kuwa ataimarisha ulinzi kwenye eneo hilo: “Hata ikiwezekana tutaweka kituo cha polisi pale, vijana wa Dar es Salaam changamkieni ajira hizi, lakini msiwe wazembe au wadokozi.”
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya wataalam wanaosimamia ujenzi huo, alisema kamati yake itafanyakazi kwa uadilifu ili kuhakikisha kuwa daraja hilo linajengwa kwa ubora wa kimataifa.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali akiwemo Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, ambaye alisema mradi huo utazalisha pia ajira za kudumu takribani 1,000.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Hubert Mrango, Wenyeviti wa Bodi mbalimbali ikiwemo ya makandarasi, wahandisi, wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi na maofisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya Ujenzi na NSSFMkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ramadhani Dau, akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Shi Yuan kutoka kampuni ya ujenzi ya China Railways Constructin Engineering Group, kwa pamoja wakiweka saini