Tuesday, 29 November 2011

VIANDUNJE VYA NIGERIA MMOJA AFUNGA NDOA, AFANYA KUFURU

HIVI karibuni kulikuwa na shangwe, hoihoi nderemo na vifijo pale muigizaji nyota wa filamu wa Nigeria, Chinedu Ikedieze, maarufu kwa jina la Aki (33), alipofunga pingu za maisha na mrembo Nneoma Hope Nwajah (20) katika kitongoji cha Mbano kilichopo katika Jimbo la Imo. 

Aki, mmoja wa mastaa `mbilikimo’ na `pacha wake katika filamu’, Osita Iheme (Ukwa) ni marafiki wakubwa ambao wamefanikiwa kuigiza filamu nyingi na kuliteka soko la tasnia hiyo katika mataifa mbalimbali ya Afrika na nje ya Afrika, Tanzania ikiwemo. 

Harusi hiyo iliyokuwa na vionjo vyote vya kimila ilifanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Theresa lililopo katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Obolo katika kitongoji hicho cha Mbano. 
Haikuwa harusi ya ‘kitoto’ kwani Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan na mkewe walialikwa na kuhudhuria sherehe hiyo. 

Wageni wengine mashuhuri waliokuwa wamethibitisha ni magavana watatu kutoka majimbo ya Kusini Mashariki mwa nchi ya Nigeria. Hao si wengine bali Gavana wa Jimbo la Abia, T.A. Orji, Jimbo la Imo, Rochas Okorocha na wa Jimbo la Anambra, Peter Obi. 

Rafiki mkubwa wa karibu wa Aki kwa zaidi ya miaka kumi sasa, Osita Iheme (Ukwa), ndiye aliyekuwa mwambata (best man) wa bwana harusi. Chanzo cha uchumba wao Staa Aki na Nneoma wamekuwa wachumba kwa miaka mitatu sasa, katika kipindi ambacho wameoneshana mapenzi ya dhati baina yao. 

Hatimaye Aki amepata mwenza na kuweka mambo hadharani namna alivyoweza kukutana na mpenzi wake huyo na kujikuta akitumbukia katika dimbwi kubwa la mahaba mithili ya bahari na kuwa vigumu kwake kuweza kujinasua. Mwenyewe anasema mkewe huyo sasa ni sehemu ya maisha yake yote yaliyosalia hapa duniani. 

“Tumekuwa katika lindi la mahaba kwa miaka mitatu, nilikutana naye Lagos na katika hali isiyoelezeka ghafla tulijikuta tukizama katika ulimwengu wa mapenzi.Yeye sasa ni tumaini la maisha yangu yote, na hakuna zaidi ya kifo kitakachotutenganisha,” Aki aliapa. 

Anapoulizwa mkewe alivutiwa zaidi na nini kwake, Aki alikuwa na haya ya kusema “aliniambia ananipenda kwa vile mimi ni mtu mzima, ni mwelewa, mwenye mvuto, busara na upendo wa dhati.” 

Akijibu swali la ni watoto wangapi angependa kupata na mkewe huyo, Aki anasema “Si zaidi ya watoto watatu bila kujali jinsi yoyote watakayokuwa nayo.” Kuhusu tetesi kwamba alitumbukia kwenye penzi na mrembo huyo kutokana na haiba yake iliyojielekeza zaidi katika kumcha Mungu, Aki anasema hilo pia limechangia kuongeza nafasi ya pendo kwa mkewe. 

Muigizaji huyo ambaye amejinyakulia tuzo nyingi ikiwemo tuzo ya heshima ya Taifa la Nigeria ya MFR mwaka mmoja uliopita, anasema anajisikia mwenye faraja kwa vile tuzo hizo zinamuweka karibu na watu wengi wa kawaida. 

Mke wa Aki, Nneoma, akizungumzia uamuzi wake wa kufunga ndoa na Aki akiwa na umri huo wa miaka 20 huku akionekana kuwa mwanamke mrembo, anasema amechukua uamuzi huo kutokana na kuongozwa na matakwa ya Mungu. 

Machungu katika safari ya mapenzi 

Akiwa katika maumivu makali ya kumsaka mrembo wa kuishi naye kwa maisha yake yote yaliyosalia duniani, Aki alivumilia hali hiyo kwa miaka mingi. Kabla ya kupata mafanikio hayo, muigizaji huyo mwenye utajiri mkubwa wa fedha, akiwa na majumba na magari ya kifahari, alimchumbia ofisa wa benki, aitwaye Nkechi kutoka eneo la Delta, uchumba ambao ulikufa ghafla katika tukio ambalo halijatolewa maelezo yoyote ya maana hadi sasa. 

Haikuchukua muda mrefu baada ya hapo, milionea huyo alianzisha mahusiano mengine ya mapenzi ya nguvu na mwanamke mwingine. Uhusiano huo nao ulikatika ghafla. Sasa hatimaye Aki amekamilisha safari yake hiyo kwa kufunga pingu ya maisha na Nneoma. 

Sherehe hiyo ya harusi ya kimila iliyofanyika karibuni na kuwajumuisha ndugu, jamaa na marafiki ilishuhudiwa na mamia ya wananchi wa kitongoji hicho cha Mbano ambako Nneoma amezaliwa. 

Habari njema zinasema sherehe hiyo ya harusi itafuatiwa na pati babu kubwa iliyofanyika katika Jiji maarufu la Lagos, Desemba 10, mwaka huu. 

Historia ya maisha yake 

Aki, anasema kwa kila filamu yao hulipwa kati ya dola 8,000 na 30,000 (kati ya Sh milioni 15 na milioni 52), alizaliwa Desemba 12 mwaka 1977 katika kitongoji cha Bende katika Jimbo la Abia. Amejipatia umaarufu mkubwa kwa kuigiza filamu mbalimbali zijulikanazo duniani kwa jina la filamu za Aki na Ukwa. 

Mwaka 2007, Aki alipata mafanikio makubwa katika maisha yake pale alipotwaa taji la Muigizaji Bora wa Afrika, taji linalotolewa na Taasisi ya Filamu ya Afrika (AMA). 

Hadi mwaka 2002 ilipotokea bahati wakakutana katika mojawapo ya matamasha ya sanaa, si Aki wala Ukwa aliyekuwa anajua kwamba wanavyo vipaji na ubunifu ambao kama wataviunganisha kwa pamoja wataweza kuteka soko la filamu duniani. 

Umaarufu wao umewafanya waigizaji hao wafupi lakini wenye makeke mengi kupata mialiko mingi na yenye malipo makubwa kutoka nchi mbalimbali duniani. 

Aki ni msomi wa Shahada ya Mawasiliano kwa Umma aliyotunukiwa na Taasisi ya Uongozi na Teknolojia (IMT) ya Enugu wakati Ukwa hivi sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Kozi ya Mawasiliano kwa Umma katika Chuo Kikuu cha Serikali cha Enugu. 

Ingawa wamejipatia mafanikio makubwa katika tasnia ya filamu, lakini magwiji hao wa vichekesho wamebaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wao na dunia kwa ujumla na hivyo kuamua kuongeza viwango vyao vya elimu.

“Nilizaliwa katika familia ya Mzee Michael Ikedieze Ogbonna. Nimekulia katika kijiji cha Iluoma Nzeakoli ndani ya eneo la Bende katika Jimbo la Abia. Baada ya kuhitimu elimu ya msingi na sekondari , niliendelea na elimu ya juu katika Taasisi ya IMT Enugu, ambako nilihitimu kozi ya Mawasiliano kwa Umma. 

“Uigizaji ni kipaji nilichopewa na Mungu tangu nikiwa mtoto. Kwa mfano nikiwa sekondari nilikuwa mwanachama wa kikundi cha sanaa na uigizaji cha shule. Nafasi muhimu ilijitokeza wakati nikiwa mwaka wa kwanza Chuo cha IMT, Agosti mwaka 1998, siku ambayo nilikutana na rafiki ambaye nilimfahamisha kuhusu lengo langu la kuwa muigizaji. 

“Nilipomwambia kuhusu hilo na kwamba napenda kuona siku moja ninashiriki katika uigizaji wa filamu zinazozalishwa nchini mwangu Nigeria, aliniahidi kunichukua kesho yake hadi katika Hoteli ya Ogui hapa katika mji wa Enugu, ambako kulikuwa na tamasha la kuwasaka wasanii nyota ili kutengeneza filamu ya ‘Evil Men’. Waandaaji waliniona na kunichagua kuingia kushiriki katika filamu ile, hapo ndipo nilipoanzia,” anasema Aki. 

Jamii inazitazama vipi filamu zao? 

Kasheshe kubwa ilizuka hivi karibuni pale baadhi ya wazazi wa nchini Nigeria walipotishia kuzipiga marufuku filamu zilizochezwa na Aki na Ukwa kwa madai kuwa, zinatoa mafundisho mabaya kwa watoto wao. 

Wazazi hao wanasema, filamu nyingi zinazochezwa na waigizaji hao zinaonesha dharau kwa watu wazima na kuwafundisha wizi vijana. “Vijana wengi wamekuwa wakiiga matukio yanayofanywa na Aki na Ukwa kwenye filamu wanazocheza, hivyo kuathirika,” amesema mmoja wa wazazi hao, aliyehojiwa na mtandao wa Nigeriafilms. 

Mzazi mwingine anasema, matukio ya wizi yamekuwa yakiongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, wahusika wakuu wakiwa vijana wa umri mdogo kutokana na kuiga tabia za wacheza filamu hao. 

Wazazi hao wamedai kuwa, vijana wengi wa umri mdogo nchini Nigeria wanapenda kuishi maisha yanayofanana na yale ya Aki na Ukwa bila kujua kuwa ni ya uigizaji. 

Baadhi ya wazazi wamehoji ni kwa nini filamu zote wanazoshiriki kucheza vijana hao, zinaonesha vitendo vya uovu katika jamii badala ya mafundisho mema. “Kama huoneshi matendo mazuri kwa vijana wako nyumbani, lazima watakuiga,”anasema mmoja wa wazazi hao. 

Mzazi huyo anasema wanawapa changamoto waandaaji wa filamu wa Nollywood, kubadili mwelekeo kwa kuandaa sinema, ambazo haziwezi kuathiri maisha ya vijana wao. “Wanapaswa kutengeneza filamu zenye mwelekeo chanya. Vijana ni wepesi wa kuiga na wakifanya hivyo, wanaonesha picha mbaya ya Wanigeria,” anaongeza. 

Hata hivyo harusi ya Aki inaelezwa kwamba itamaliza kabisa hisia mbaya za wazazi wa Nigeria kwamba waigizaji hao si kioo kizuri kwa jamii kutokana na visa na mikasa ikiwemo ya usaliti katika mapenzi wanayoiigiza katika filamu zao. 

Ndoa ya Aki inatajwa kuwa mfano wa kuigwa ambao utaibua mwanzo wa mapinduzi mapya ya fikra za vijana wa Nigeria kuhusu ndoa na familia kwa ujumla katika misingi ya kuheshimu mila, desturi na Mungu. 

Huyo ndiye muigizaji Aki ambaye ameiaga rasmi kambi ya ukapera kwa kumuoa mrembo mbichi, Nneoma baada ya miaka mingi ya tabu, shida, mateso, na kero za mapenzi.

No comments:

Post a Comment