WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano ya Kimataifa, Bernard Membe amesema kuanzia sasa, kila mkutano wa kimataifa utakaofanyika nchini, atahakikisha washiriki wake wanatembelea maeneo tofauti ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii watakaoongeza pato la nchi.
Aliyasema hayo jana mjini hapa, baada ya mabalozi zaidi ya 29 wa nchi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini, kutembelea Bonde la Oldupai Gorge na kupata maelezo ya eneo hilo, kuhusu uvumbuzi wa fuvu na nyayo za binadamu wa kwanza.
Waziri Membe alisema lengo la Wizara hiyo kuwapeleka mabalozi kwenye maeneo ya utalii kama hilo, ni kuitaka dunia ifahamu asili ya binadamu, kadhalika na kutangaza utalii uliopo nchini ili kukuza pato litokanalo na sekta hiyo, kutoka asilimia 17 ya sasa hadi kufika 40.
“Tunataka dunia ifahamu na kutambua asili yao kwamba chimbuko la binadamu wa kwanza ni hapa Oldupai Gorge, na ninawaahidi Watanzania kuanzia sasa, kila mkutano wa kimataifa utakaofanywa hapa nchini, nitahakikisha washiriki wake wanatembelea vivutio vyetu”, alisema Membe.
Katika hatua nyingine, Membe alisema ipo haja ya kufungua Chuo Kikuu cha Elimu ya Jamii na masalia ya viumbe wa kale ili kuongeza utafiti na kuwa na taarifa nyingi za mambo ya kale, ambayo ni urithi na sehemu muhimu ya utalii.
Alisema kupitia mabalozi hao, anaamini wakirudi kwenye nchi zao, watakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania, hasa kwa utajiri wa vivutio vya kipekee vilivyopo, ambavyo nao wamevishuhudia.
Baada ya kusikiliza maelezo kuhusu Bonde la Oldupai Gorge na eneo la Laetoli ambalo nyayo za binadamu wa kwanza duniani kuishi alipatikana hapo, Balozi wa Zambia nchini, Mavis Muyunda alihoji kama kuna juhudi zimefanywa kutangaza eneo hilo, na iwapo kuna fursa za wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali Afrika wanaweza kwenda kujifunza kwenye eneo hilo.
Akijibu swali hilo, Meneja wa Kituo cha Makumbusho cha Oldupai Gorge, John Paresso alisema maombi ya wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali Afrika na Duniani yanapokelewa na kupitiwa na wale wanaokuwa na sifa hupata nafasi ya kujifunza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk. Paul Msemwa akizungumzia uwepo wa masalia ya binadamu wa kale kupatikana eneo hilo, alisema nyayo zilizogunduliwa za binadamu wa kwanza katika eneo la Laetoli ni kielelezo dhahiri cha chimbuko la mwanadamu.
Alisema kwa sasa nyayo hizo zimefunikwa hivi sasa, lakini mwaka 2014 zitakuwa wazi baada ya kujengewa nyumba ya makumbusho ili kuzihifadhi kwa kumbukumbu, utalii na hata kwa ajili ya mafunzo ya watafiti.
Eneo la Laetoli zinapopatikana nyayo za binadamu wa kwanza kuishi duniani, ziko umbali wa kilomita 47, Kusini wa Bonde la Oldupai. Leo mabalozi hao watatembelea Bonde la Ngorongoro na baadaye kwenda Zanzibar
No comments:
Post a Comment