RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali ina mpango wa kuendelea kujenga vyuo vikuu vingi vya ukubwa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kupanua sekta ya elimu ya juu nchini.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Kikwete alisema Serikali itatoa mchango mkubwa katika ujenzi wa vyuo hivyo pamoja na
kwamba uwekezaji katika eneo hilo ni mgumu kutokana na gharama.
“Nawaahidi tutavijenga vyuo hivi kama tulivyoijenga UDOM, ujenzi wa chuo kile uliigharimu
sana Serikali, lakini hili halituzuii kujenga zaidi. “Tayari tumeanza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Tengeru, ambacho muundo wake na kila kitu utakuwa kama wa UDOM, na kitaitwa Mandela,” alisema Rais Kikwete.
UDSM na Uganda
Wakati Rais Kikwete akisema hayo, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliwataka Watanzania kujivunia matunda ya UDSM kutokana na mchango mkubwa ambao chuo hicho umetoa ndani na nje ya Tanzania.
Aliwapongeza Watanzania kwa kutimiza miaka 50 ya Uhuru wao na wa Chuo hicho na kuelezea kuwa, wahitimu wa chuo hicho wengi si tu wameisaidia Tanzania, bali hata Uganda.
Alisema viongozi wengi wa Uganda walisoma hapo na kutoa mfano wa Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Amanya Mushega na mkewe Janet Museveni ambaye pia ni Waziri nchini humo.
“Mbali na mimi kule nchini kwangu madaktari, mawakili na viongozi wengi wamesoma hapa UDSM na wanatoa mchango mkubwa wa maendeleo, ni vyema Watanzania wakajivunia chuo hiki na kuhakikisha kinapanuka na kuzaa vyuo vingi zaidi kwa faida ya vizazi vijavyo,” alisema.
Elimu ya Juu Akifafanua juhudi za kupanua sekta ya elimu ya juu nchini, Rais Kikwete alisema tayari Serikali imeanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu (HEDP) wa mwaka 2010
hadi 2015.
Mpango huo kwa mujibu wa Rais, utatoa mafunzo kwa wahadhiri, kukarabati na kujenga zaidi vyuo vikuu, kusambaza vifaa vya kufundishia kama vile kompyuta na vitabu na kusimamia ipasavyo masuala ya utafiti.
“Kwa nchi masikini kama Tanzania ambayo pato lake la Taifa kwa mwaka ni dola za Marekani bilioni 25, mpango huo utekelezaji wake ni mgumu lakini Serikali imedhamiria kuudhamini
kama ilivyodhamini miradi mingine ya maendeleo ya shule za msingi na sekondari,” alisema.
Akizungumzia historia ya elimu, Rais Kikwete alisema tangu Uhuru hadi sasa mafanikio makubwa yamepatikana ambapo kwa sasa asilimia 97 ya wanafunzi wa shule za msingi wana nafasi ya kusoma elimu hiyo ikilinganishwa na asilimia mbili tu miaka 50 iliyopita.
Mbali na mafanikio hayo, pia fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu zimepanda kutoka Sh bilioni 6.1 mwaka 2005/2006 hadi Sh bilioni 317.9 mwaka huu.
Alisema kwa sasa kuna shule zaidi ya 15,816 za msingi ikilinganishwa na shule 3,000 mwaka 1961 na shule za sekondari 4,367 ikilinganishwa na 41 wakati wa Uhuru.
Alitaja idadi ya wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza kuwa ni milioni 1.6 ikilinganishwa na miaka 50 iliyopita ambapo walikuwa 11,832.
Kwa upande wa vyuo vikuu, Rais alisema baada ya Uhuru kulikuwa na chuo kimoja cha UDSM kilichokuwa chini ya Chuo Kikuu cha London kikiwa na wanafunzi 14, kati yao 13 Watanzania na mmoja Mganda, lakini kwa sasa kuna vyuo zaidi ya 40 vyenye wanafunzi 135,367 huku
UDSM pekee ikiwa na wanafunzi 19,563.
“Tunajua kuwa bado tunahitaji kupambana zaidi ili kupanua sekta ya elimu nchini na kufanikisha kukabiliana na idadi ya watu inayokua kila siku, ili kufikia hatua ambayo wenzetu
wamefikia,” alisema.
Alisema nchi nyingine duniani zina wahitimu wa elimu ya juu wengi zaidi na wahadhiri ikilinganishwa na nchi za Afrika ambapo wakati nchi za Kiarabu zina wahitimu milioni 6.5, Marekani milioni 14.6 Afrika kama Afrika Kusini zina wahitimu milioni 3.3, Kenya 108,407, Uganda 88,360 na Tanzania 42,948.
“Na hapa sijutii hata kidogo, uamuzi wa kuongeza bajeti kila mwaka katika sekta ya elimu ili kukabiliana na hali hii,” alisema Rais Kikwete.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema UDSM ni chuo cha kwanza nchini na kimezalisha wataalamu, viongozi na kufanya utafiti wa masuala mbalimbali yanayowakabili Watanzania na hivyo kusaidia maendeleo ya Taifa.
Maadhimisho hayo ambayo awali yalianza kwa vurugu baada ya wanafunzi wa chuo hicho kukusanyika na kumpokea Rais Kikwete na mgeni wake kwa mabango na nyimbo, pia yalihudhuriwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba.
Aidha, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alitoa zawadi kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mkuu wa Kwanza wa Chuo hicho, Profesa Robert Pratt.
Zawadi zingine zilitolewa kwa Mkuu wa Kwanza wa Chuo hicho ambaye ni mzawa, Dk. Wilbert Chagula; aliyehusika kutafuta eneo chuo hicho kilipo sasa, Chifu George Kunambi; Mkuu wa Kwanza wa Kitivo cha Sheria, Arthur Weston na mwanafunzi wa kwanza wa kike chuoni hapo, Jaji Julie Manning.
No comments:
Post a Comment