Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID), inafanya utaratibu wa kupokea Paund milioni 29.50 (Sh. bilioni 75) zikiwa ni malipo ya fedha za tozo za rada.
Pia inafanya utaratibu wa kushughulikia akaunti itakayotumika kuhifadhi fedha hizo zitakapoingia nchini.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE.
Alisema utaratibu huo unafanyika baada ya Serikali ya Uingereza kuihakikishia Serikali ya Tanzania kwa maandishi kwamba, italipwa fedha hizo.
Mkulo alisema hayo alipotakiwa na NIPSHE kueleza kama Serikali ya Tanzania imekwisha kupokea fedha hizo au la.
“Tumeshapata barua kutoka Serikali ya Uingereza kwamba, serikali (ya Tanzania) italipwa Paund milioni 29.50,” alisema Waziri Mkulo.
Alisema utaratibu huo unafanywa kati ya serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha na Uchumi, BoT na DFID.
Fedha hizo zinarejeshwa nchini baada ya Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza iliyouzia Tanzania rada hiyo kwa bei kubwa kuliko bei yake halisi, kuamriwa na mahakama nchini humo, kulipa faini hiyo.
Amri hiyo ilitolewa na mahakama, baada ya kampuni hiyo kugundulika kwamba, ilikwenda kinyume katika kuiuzia Tanzania rada hiyo mwishoni mwa miaka ya 1990.
No comments:
Post a Comment