Thursday, 6 October 2011

JK AELEZWA HALI TETE YA KIDATU

HALI ya uzalishaji umeme Kidatu mkoani Morogoro ni mbaya kutokana na kulazimika kupunguza uzalishaji kutoka megawati 200 hadi 40.

Rais Jakaya Kikwete ambaye alisimama kwa muda katika bwawa hilo na kujionea hali halisi,
alielezwa na Kaimu Meneja wa Uzalishaji Umeme Kidatu, Joseph Lyaruu kuwa hali hiyo
imesababishwa na kupungua kwa kiwango cha maji katika bwawa hilo.

Kabla ya kusimama kwa muda katika bwawa hilo, Rais Kikwete alifunga mafunzo ya Uchunguzi
na Upelelezi wa Maofisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi katika Chuo cha Polisi kilichoko hapo hapo Kidatu.

Hata hivyo, kwa sasa Serikali haitegemei sana umeme wa maji na badala yake inafua umeme kwa kutumia mitambo ya gesi asilia na ifikapo Desemba makali ya mgawo wa umeme yanatarajiwa kupungua kabisa.

Kwa sasa katika mipango ya muda mfupi ambayo inatekelezwa, ifikapo Jumatatu ijayo Megawati 137 za umeme zinatarajiwa kuingizwa katika gridi kutoka mitambo ya gesi asilia ya
kampuni za kufua umeme za Simbion na Agreco.

Lyaruu alimweleza Rais kuwa hata uzalishaji umeme katika bwawa la Mtera, bado ni mdogo
sana kwa sababu bwawa hilo linazalisha kiasi cha megawati 30 tu kati ya megawati 80 zinazoweza kuzalishwa kwenye bwawa hilo kama yapo maji ya kutosha.

“Hali bado mbaya,” Rais Kikwete alisema baada ya kupata maelezo kutoka kwa Lyaruu kuhusu hali hiyo iliyosababisha mgawo mkubwa wa umeme nchini kwa miezi kadhaa sasa na kuilazimu Serikali kuchukua hatua za dharura za kuzalisha umeme kutoka vyanzo vingine.

Wakati Rais Kikwete akishuhudia hali hiyo Kidatu, Brazil imeahidi kuisaidia Tanzania kuondokana moja kwa moja na shida ya umeme kwa kuisaidia teknolojia.

Waziri wa Madini na Nishati wa Brazil, Edson Lobao alitoa ahadi hiyo katika mazungumzo rasmi ofisini kwake mjini Brasilia na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye yuko nchini humo kwa ziara ya kikazi.

Lobao alisema Brazil ina uzoefu mkubwa katika teknolojia ya kufua umeme na akaahidi kuliagiza Shirika la Nishati ya Mafuta la Brazil (PETROBRAS), kuangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika eneo hilo.

Petrobras, pia inashughulikia uzalishaji wa umeme kwa nguvu ya maji, tayari ipo nchini na
inatafuta mafuta na gesi kwenye pwani ya Mtwara.

Brazil pia imeonesha nia ya kuisaidia kiufundi Tanzania katika ujenzi wa kinu kikubwa cha kufua umeme kwa nguvu ya maji kwenye eneo la Stegler’s Gorge katika Mto Rufiji mkoani Pwani.

*Ahadi za JK zatimia
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliyeko ziarani mkoani Mogororo, akiwa njiani kwenda
Ifakara kutoka Kidatu, alisimama kwa muda katika Kijiji cha Mkula kupata maelezo kuhusu skimu ya umwagiliaji ya kilimo cha mpunga, ambayo aliifungua mwaka 2008.

Akiwa hapo, Rais Kikwete aliambiwa kuwa baada ya kujengwa kwa skimu hiyo kwa Sh milioni
276 za Serikali, wananchi wa kijiji hicho sasa wameongeza uzalishaji wa mpunga hadi kufikia tani 7.6 kwa ekari moja kutoka tani 1.5 iliyokuwa inavunwa kabla ya kuanza umwagiliaji.

“Tumesikia unapita na tukaamua kujikusanya kukushukuru kwa msaada wako. Uliahidi kutupatia power tillers tano na tayari tumekwishapokea nne.

“Tulikuwa tunalima ekari 12 tu kabla ya skimu ya umwagiliaji kujengwa na sasa tunalima ekari 100 kati ya ekari 254 za eneo hili. Tunakushukuru sana kwa sababu yote uliyotuahidi ulipofika hapa mwaka 2008 yametimizwa,” wananchi hao walisema katika risala iliyosomwa kwa niaba yao.

Risala hiyo ilieleza kuwa kipato cha wananchi hao kimeongezeka kiasi kikubwa, wana chakula
cha kutosha na ziada kubwa ya kuuza.

“Tunaweza sasa kulipa ada ya wanafunzi wa shule yetu, tuna chakula cha mwaka mzima, tunazo fedha za matibabu na tuna uwezo wa kuchangia miradi mbali mbali ya maendeleo,” ilieleza risala hiyo.

Wananchi hao walisema ni viongozi wachache sana wanaoahidi kuwatembelea tena
wanavijiji na kutimiza ahadi hiyo; “tena kututembelea sisi kwenye hii vumbi. Kama ungekuwa mchezaji wa mpira, hakuna shaka kuwa ungenunuliwa kwa bei mbaya.”

Naye Waziri Mkuu Pinda nchini Brazil, mbali na kutafuta fursa za kuondoa kero ya nishati, pia alifanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Mifugo wa Brazil, Jorge Alberto Portanova Mendes Ribeiro Filho na Waziri wa Maendeleo Vijijini, Afonso Florence.

Baada ya mazungumzo hayo, alitembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha EMBRAPA na leo
atatembelea mji mwingine mkubwa wa Brazil, Rio de Janeiro.

Tayari amekwishatembelea Sao Paulo ambako, pamoja na mambo mengine alitembelea Makao
Makuu ya Kampuni ya ABIMAQ inayotengeneza zana za kilimo

No comments:

Post a Comment