Tuesday, 20 September 2011

KUWA JASILI USIOGOPE, KAZA BUTI


HUWEZI kufanikiwa kama huthubutu kufanya mambo fulani. Kusoma sana au kidogo, kuwa na rafiki waliofanikiwa au wasiofanikiwa, kwenda nje ya nchi au la, au kuzaliwa familia maskini au tajiri, bado sio tiketi ya kukufanya uwe na maisha bora.
Msingi wa kufanikiwa ni kuthubutu kufanya jambo fulani, kwa mfano kufungua mradi na mambo mengine kama haya. Kuna watu kwa mfano unaweza kuona anakata tamaa kwa sababu labda amezaliwa katika familia maskini, kitu ambacho sio sahihi.
Msingi wa kuwa na maisha bora ni kufanya kazi kwa bidii na zaidi ni kuishi kwa malengo. Usiishi tu ili mradi siku zinakwenda mbele, ishi kwa malengo. Kwa chochote unachokifanya, kifanye baada ya kutafakari na kuangalia faida au hasara yake.
Maisha yanatuhitaji kuwa waangalifu na wanadamu wanaotunguka, kwa sababu walio wengi furaha yao ni kuona unakuwa hauna mafanikio. Kuna wengine kwa mfano kabla ya kufanikiwa anakuwa ni rafiki, lakini ukishafanikiwa, anakuwa mtu mbaya.
Kuna mwingine hata ukimwangalia sura yake anaonekana wazi kabisa kwamba hana furaha, unapomwambia kwamba mambo yangu yanakwenda safi. Furaha ya watu walio wengi ni kusikia unaishi maisha ya kawaida, au unaishi maisha ya shida.
Kwa bahati mbaya sana, siku hizi hadi baadhi ya wazazi wamekuwa wabaya kwa watoto wao, kuna wengine kwa mfano hajui ni kwa vipi unaendesha gari, unaishi nyumba nzuri, badala yake anapokuona unaendesha gari zuri anakuja juu na kulalamika kuwa mbona huwasaidii.
Wanashindwa kujua kuwa kuna wengine wanatembea na magari si yao.
Ambacho nataka kusisitiza katika makala haya ni kwamba mafanikio yako yanatokana na akili yako uliyonayo, ndio maana wengine wamekuwa wakisema kuwa ‘ugumu wa maisha ndio kipimo cha akili’.
Wengi wanapingana na msemo huu, lakini ndio ukweli wenyewe kwamba hali ya maisha ambayo unayo, ndio hasa inayoeleza hali ya uwezo wa kufikiri.
Endapo utatumia akili, hisia na imani yako kwa busara na kufanyia kazi, ni lazima maisha yako yatakuwa na mabadiliko makubwa ya mafanikio.
Lakini kama unaishi na hauna mafanikio, hata kama umesoma sana au una umaarufu, elimu yako haina msaada. Imani ya wengi ni kwamba angalau baada ya kusoma, unaweza kuitumia elimu kuharakisha maendeleo, kwa maana hiyo kama unashindwa kuyapata maendeleo, maana yake ni kuwa hauna uwezo wa kutumia vizuri akili uliyonayo.
Una uhuru wa kuchagua namna unavyofikiri, kwa mfano kama unaamini kulewa ndio maendeleo, hiyo inaweza kuwa ni akili mbaya ambayo maana yake maendeleo yako unayopaswa kuyatarajia ni maisha yaliyo duni.
Huwezi kutupa fedha kwenye vitu visivyo na maana halafu ukatarajia maendeleo. Mtu huvuna kile alichopanda, si ndio jamani? Kama unaelekeza fedha nyingi kwenye kitu fulani, hakuna ubishi kwamba mwisho wa siku utavuna matunda ya kile kitu ambacho umewekeza fedha zaidi.
Kwa mfano kama ukaona kwamba kufanya ngono na wanawake ni suala zuri, kwa hiyo unadharau watoto na mkeo na kujali nyumba ndogo, kwa wasio na akili timamu, kwao hiyo ni hekima, lakini mwisho wa siku tarajia kuvuna faida ambayo ni shida.
Ulinunua kama ni kondom, ulilipia fedha labda kwenye gesti, ulilipia labda ni kuhonga, kwa hiyo subiri faida yake…amini nakwambia hakuna utakachoambulia zaidi ya maumivu…bora wale waliopanda DECI labda wanaweza kuambulia chochote.
Mafanikio au kushindwa kwako inategemea jinsi unavyofikiri. Wakati mwingine kama unafikiri huwezi kuendesha mambo, si mbaya kuomba ushauri kwa watu wengine, watakusaidia kubadilisha mawazo.
Achana na imani potofu kwamba huwezi kufanikiwa, badala yake amini kuwa unaweza kufanikiwa. Wakati wote jiamini, jione wewe ni bora na unaweza.
Uwe mwenye kuwajali watu wengine, ishi katika hali ya uaminifu kwa shughuli unazofanya na kwa familia yako. Usitarajie maisha mazuri yenye amani kama unawadharau watoto wako na mkeo au mumeo. Kuidharau familia yako ni kujitakia laana.
MSINGI WA MAISHA YENYE MAFNIKIO: Kuna siri nyingi lakini yapo mambo matatu, ambayo ni Ukweli, ushindi na ujasiri. Kwa hakika hizo ni silaha kubwa ya mafanikio katika maisha yako, zizingatie, hakika utakuwa wa tofauti.
Achana na wale ambao wamekuwa maarufu wa kukatisha tamaa. Aidha kamwe usiruhusu mawazo ya kukatisha tamaa, wala usipende kuwasikiliza wenye tabia ya kukatisha tamaa.

Ndugu yangu inakuwaje unataka maisha bora halafu unakuwa mwoga wa kujaribu? Acha woga, amini kuwa wewe unaweza, anza kujiwekea mikakati, anza kuangalia namna ya kuitekeleza, hakika utafanikiwa

No comments:

Post a Comment