Tuesday, 23 August 2011

YANGA WAMJIA JUU KOCHA

08_11_uqsk9s.jpgMASHABIKI wenye hasira wa Yanga, juzi walivamia gari la wachezaji pamoja na la kocha wa timu hiyo Sam Timbe wakilalamikia mchezo mbovu uliosababisha timu yao ifungwe na JKT Ruvu bao 1-0.

Mashabiki hao walitoa kauli kali kwa wachezaji na Timbe huku wakisisitiza kuwa mchezo wa Jumatano kati ya Yanga na Moro United ni mtihani mwingine kwa kocha huyo raia wa Uganda.

Timbe ambaye aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita na Kombe la Kagame, alilalamikiwa na mashabiki akidaiwa kushindwa kupanga kikosi na kusababisha kipigo kwa JKT Ruvu katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakizungumza baada ya kumalizika mchezo huo, baadhi ya mashabiki na wanachama wa Yanga , walidai licha ya wachezaji kucheza chini ya kiwango alishindwa kufanya mabadiliko.

Gari la wachezaji pamoja na lililombeba kocha yalipata msukosuko mkubwa, kiasi cha Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kuimarisha ulinzi zaidi ili kuwalinda.

Naye Clecence Kunambi anaripoti kuwa, akizungumzia vurugu hizo jana, Ofisa Habari wa Yanga, Luios Sendeu alisema klabu hiyo itawashughulikia mashabiki na wanachama wake watakaobainika walifanya fujo katika mchezo wa Yanga na JKT Ruvu juzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sendeu alisema wanafuatilia vurugu hizo kupitia mkanda wa video na mashabiki watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu, ingawa hakuzitaja.

Aliwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa wavumilivu pindi timu yao inapofanya vibaya kwani hiyo ni sehemu ya mchezo wa soka na kwamba viongozi wanatambua timu inapita katika kipindi kigumu kwa sasa, lakini aliwatoa hofu kuwa hali itakuwa shwari muda si mrefu.

“Hakuna mtu anayependa kufungwa, lakini hatuna budi kukubaliana na matokeo, tunawaomba watuunge mkono hali itakuwa nzuri punde,” alisema Sendeu.

Licha ya kukubali matokeo hayo, lakini pia alisema kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na ubovu wa Uwanja wa Jamhuri hali iliyowapa shida wachezaji wao kumiliki mpira.

Pia alisema kuwepo na majeruhi wengi ndani ya kikosi cha timu yao ni sababu nyingine ya kupoteza mchezo huo na kuwataja wachezaji majeruhi kuwa ni Kigi Makassy, Davies Mwape, Kenneth Asamoah na Yaw Berko.

Wakati huohuo, Mwandishi Wetu anaripoti kutoka Morogoro kuwa mchezo kati ya Yanga na JKT Ruvu umeingiza kiasi cha Sh milioni 15.3.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro ( MRFA) Hamis Semka , alisema mapato hayo yalitokana na kiingilio cha Sh 3,000 na kwamba kila timu ilipata Sh milioni 3.4 na kilichobakia kiligawanywa kwa taasisi, vyama vya michezo ikiwemo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ( TFF).

No comments:

Post a Comment