JWTZ waitwa kukabili majangili
20th August 2011
B-pepe
Chapa
Maoni
Vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vitapelekwa kwenye maeneo ya magharibi mwa Tanzania kufanya kazi maalum ya kukabiliana na ujangili katika hifadhi na mapori katika mikoa hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, alisema vikosi hivyo vitapelekwa haraka kuanzia sasa kutokana kasi ya matukio ya ujangili katika maeneo hayo yanayofanywa na watu kutoka nchi jirani.
Waziri Maige alitangaza uamuzi wa serikali kulitumia JWTZ jana asubuhi wakati akizungumza katika kipindi cha ‘Tuongee’ kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Star TV.
Alisema wizara yake inachukua hatua hiyo kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete wakati alipotembelea Wizara yake mwaka huu ambapo alielekeza kuwa kama inaonekana askari wa wanyamapori hawawezi kukabiliana na majangili, yupo tayari kutoa askari wa JWTZ kwenda kufanya kazi hiyo.
Maige alisema mchakato wa kuanza kazi hiyo upo katika hatua ya mwisho na kwamba vikao vinavyojumuisha wataalamu kutoka wizara yake na JWTZ vinaendelea kufanyika.
Alitaja mikoa ambayo operesheni hiyo itatekelezwa kuwa ni Kagera eneo la Biharamulo, Kigoma kwenye maeneo yote ya mapori tengefu na Hifadhi ya Katavi iliyopo katika mkoa wa Rukwa.
“Nataka kuwaeleza Watanzania kuwa wizara imekubali ofa ya Rais Kikwete kwa kupeleka askari wa Jeshi la Wananchi kule mikoa ya magaharibi,” alisema na kuongeza: “Hili tunalifanya kwa nia njema ya kuhakikisha majangili wanatoweka.”
Alisema awali walisita kukubali kutumia Jeshi ili kuangalia njia nyingine bora ya kutumia askari wa wanyamapori kukabiliana na vitendo hivyo, lakini kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya kwenye hifadhi na mapori, wameamua kukubaliana na Rais Kikwete.
Waziri Maige alisema hivi karibuni walikamata kontena moja lenye uzito wa kilo 30 likiwa limejaa bunduki za kivita aina ya SMG pamoja na risasi zake ambazo zilikuwa zinatumiwa na majangili kuua wanyama.
Waziri huyo aliongeza kuwa hata askari wa wanyapori wanaonekana kuzidiwa na majangili kutoka nchi jirani katika maeneo hayo.
“Hatuwezi tena kuwatumia askari wetu, wale watu wanatumia silaha za kivita na nadhani ujangili wao umevuka mipaka, haiwezekani kutembea na kontena la silaha tena kwenye hifadhi zetu na sisi tukalala,” alisema.
Hata hivyo, alisema vikosi vya JWTZ havitapelekwa katika hifadhi za mikoa ya kaskazini na kusini ili kuepusha usumbufu watakaopata wananchi wanaozunguka hifadhi hizo na mapori.
Kwa mujibu wa Waziri Maige, wanajeshi kwa kawaida wanapokuwa kwenye shughuli hizo hawafanyi kazi kama wanavyofanya askari wa wanyamapori kitu ambacho kinaweza kuwagharimu wananchi wanaoingia kwenye hifadhi na mapori kwa bahati mbaya.
Aliongeza kuwa katika kukabiliana na mapambano dhidi ya majangili, wizara yake kwa kupitia Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro, Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) wameamua kununua helkopta itakayotumika kwa ajili ya kufanya doria kwenye mbuga hizo.
Rais Kikwete katika ziara yake ya kutembelea Wizara ya Maliasili na Utalii mapema mwaka huu, alimweleza Waziri Maige kuwa kama askari wa Wanyamapori wameshindwa kukabiliana na ujangili, atoe ombi la kutumia JWTZ na yeye yupo tayari kuliamuru.
Alisema sio mara ya kwanza kwa JWTZ kufanya kazi kama hiyo na kukumbushia miaka ya sabini kuwa lilitumika katika operesheni maalum ya kupambana na majangili na kupunguza vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment