MWANAMKE mkazi wa kijiji cha Ikandamoyo, wilayani hapa, Veronica Saleh ‘Mama Kaela’ (50), amefanya uamuzi adimu wa kuolewa na wanaume wawili ambao anaishi nao kijijini hapo.
Kijiji hicho kipo umbali wa takribani kilometa 30 kutoka mjini hapa katika Jimbo la Katavi linalowakilishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Pamoja na ndoa hiyo iliyowezeshwa na mume mkubwa kukubali kuishi na mume mdogo, imeelezwa kuwa mwanamke huyo ndiye ‘aliyewaoa’ wanaume hao kwa zaidi ya miaka saba sasa, huku akiwa na amri kuu katika nyumba, kama ilivyo katika ndoa za kawaida.
Wanaume hao ni Paulo Sabuni ‘Baba Kaela’ (60) ambaye ndiye mume mkubwa na Arcado Mlele (45) ambaye ni mume mdogo.
Taarifa za kuwapo kwa ndoa hiyo ya aina yake, zililifikia gazeti hili na kufanyiwa uchunguzi kwa zaidi ya wiki tatu, na hatimaye katikati ya wiki hii, wahusika walikubali wao wenyewe kuzungumzia suala hilo. Kwa mujibu wa maelezo ya mwanamke huyo ambaye alionekana kuwa msemaji wa familia hiyo, yeye na mumewe mkubwa, walifika kijijini hapo miaka 24 iliyopita, wakitoka kijiji cha Usumbwa mpakani mwa Chunya, Mbeya na Tabora.
Wakiwa kijijini hapo mume wake aliendelea kufanya kazi ya ukulima wakati yeye mama (Veronica), pamoja na kilimo hujihusisha na upishi na uuzaji wa pombe ya kienyeji ya iitwayo kayoga.
Mwanamke huyo ambaye amesema ana watoto wanne, Alfred (20), binti mwenye miaka 16 (ambaye ameolewa) na wengine wawili wa kiume, mmoja akisoma darasa la sita na mdogo ana miaka saba, amesema hana shida na waume wake.
No comments:
Post a Comment